Naomba nianze kwa kuomba radhi kwa kutoa hotuba ya mwisho wa mwezi wa saba, leo tarehe 01 Agosti, 2012 badala ya jana tarehe 31 Julai, 2012. Hii ni kwa sababu ya msiba uliotukuta katika familia na mimi kwenda Lindi kushiriki maziko ya marehemu wetu. Tofauti na miezi iliyopita leo, pamoja na hotuba ya kawaida ya mwisho wa mwezi nimetoa fursa kwa Wahariri wa vyombo vya habari nchini kuniuliza maswali nami kujibu. Kwa upande wangu nina mambo matatu ambayo nitayazungumzia leo.
Ajali ya Kuzama kwa Meli ya MV SKAGIT
Ndugu Wananchi;Jambo la kwanza ni ajali ya Meli ya MV SKAGIT iliyotokea tarehe 18 Julai, 2012. Meli hiyo ilikuwa na watu290, wakiwemo mabaharia 9, abiria watu wazima 250 na watoto 31. Juhudi za uokoaji zilianza mara baada ya taarifa ya kuzama kwa meli hiyo kupatikana. Maofisa na askari wa JWTZ, Polisi na KMKM walishiriki pamoja na meli na watu binafsi katika uokoaji. Waokoaji walifanikiwa kuwapata ndugu zetu 146 wakiwa hai na maiti 126 hadi tarehe 27 Julai, 2012. Kwa maana hiyo basi, watu 18 hawajulikani walipo na inahofiwa kuwa nao pia hawako hai. Huenda wamezama pamoja na meli au walizama baharini lakini miili yao haikuweza kupatikana.
Ndugu Wananchi;
Napenda kutumia nafasi hii kurudia kutoa mkono wa rambirambi na pole nyingi kwa wale wote waliopoteza ndugu, jamaa na marafiki katika ajali ile. Nampongeza sana Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Mheshimiwa Dkt. Ali Mohamed Shein na viongozi wenzake wa Serikali ya Mapinduzi Zanzibar (SMZ) kwa kazi kubwa na nzuri waliofanya kuongoza juhudi za uokoaji pamoja na huduma walizotoa kwa waliokolewa, waliojeruhiwa na waliofariki. Kwa wale ambao walikuwa wenyeji wa Unguja na Pemba, SMZ ilitoa sanda na usafirishaji wa maiti mpaka makwao kwa mazishi. Kwa wale wasiokuwa na ndugu Serikali ilibeba jukumu la kuwazika kule Kama, Kusini Unguja.
Natoa pongezi za pekee kwa wale wote walioshiriki katika uokoaji kwani juhudi zao ziliwezesha ndugu zetu wengi kusalimika na maiti nyingi kupatikana.
Ndugu Wananchi;
Kutokea kwa ajali ile kumetonesha jeraha la huzuni, majonzi na mashaka makubwa yaliyolipata taifa letu miezi 11 iliyopita kufuatia ajali ya kuzama kwa meli ya MV Spice Islander. Katika mkutano maalum wa Baraza la Usalama wa Taifa niliouitisha tarehe 20 Julai, 2012 kuzungumzia ajali ya MV SKAGIT tulifanya mapitio ya utekelezaji wa maagizo yetu ya mkutano wa tarehe 11 Septemba, 2011 kufuatia ajali ya MV Spice Islander. Kwa ujumla tumeridhika kuwa utekelezaji umekuwa mzuri kwa upande wa mamlaka zinazohusika na usafirishaji majini yaani SUMATRA, Zanzibar Maritime Authority na mamlaka za Bandari za nchi zetu mbili. Ushirikiano baina ya mamlaka hizo sasa ni mzuri kwa mambo yote muhimu ambayo Baraza liliagiza wafanye hivyo. Pamoja na hayo Baraza limetaka ushirikiano huo uzidishwe na kuimarishwa.
Kwa mfano, Baraza limefurahishwa na kupongeza kitendo cha mamlaka hizo kutumia Dar es Salaam Maritime Institute kwa ushauri kuhusu ubora wa meli na huduma za usafirishaji majini. Baraza limeagiza vyombo hivyo viwe na hadidu za rejea zinazofanana kwa vigezo vya ubora ili nchi yetu iwe na viwango vinavyofanana vya ubora wa meli na huduma za usafirishaji baharini kwa pande zetu mbili za Muungano. Bahari ni moja na vyombo vinahudumia watu wale wale, kuwa na vigezo tofauti vya ubora wa meli na viwango vya huduma ni jambo lisilostahili kuwepo tena, ni la hatari. Baraza pia limeagiza pawepo na ukomo wa umri wa meli zilizokwishatumika zinazoruhusiwa kutumika hapa nchini.
Aidha, Baraza limerudia kuagiza pawepo na usimamizi makini zaidi kuhusu upakiaji wa mizigo na abiria. Mamlaka husika, yaani SUMATRA, ZMA na maofisa wa bandari wahakikishe kuwa uwezo wa meli uliohakikiwa na kutambuliwa unaheshimiwa ipasavyo. Pia, meli zikaguliwe mara kwa mara na vigezo vifanane.
Ndugu Wananchi;
Pamoja na hayo, Baraza la Usalama wa Taifa limeona kuwa wakati umefika kwa Serikali yetu kuwa na Coast Guards, yaani kikosi maalum cha uokoaji na usalama majini. Aidha, Baraza limetaka hatua za makusudi zichukuliwe kuimarisha KMKM na Police Marines. Mwisho, Baraza lilipongeza uamuzi wa SMZ wa kuunda Tume ya kuchunguza ajali ile kama ilivyofanya wakati wa ajali ya MV Spice Islander.
Utafutaji na Uchimbaji Gesi Nchini
Ndugu Wananchi, Jambo la pili ninalopenda kulizungumzia leo ni kuhusu maendeleo ya sekta ya gesi asili nchini. Juhudi za kutafuta mafuta nchini zilianza mwaka 1952 na mwaka 1954 wakati kampuni ya BP ilichimba kisima cha kwanza kule Mafia. Bahati mbaya kisima hicho hakikuzaa matunda yaliyotarajiwa na juhudi za utafutaji mafuta zikafifia kabisa mwanzoni mwa miaka ya 1960. Miaka kumi baadae, juhudi hizo zilianza upya na kuendelea kwa kiwango na kasi za namna mbalimbali hadi sasa. Katika miaka ya hivi karibuni juhudi zimekuwa kubwa na kuhusisha makampuni kadhaa ya kimataifa yakiwemo makubwa na madogo.
Ndugu Wananchi;
Tangu mwaka 1954, mpaka sasa visima 61vimechimbwa, kati ya hivyo, gesi asili imegunduliwa katika visima 22, visima 14 vya nchi kavu na maeneo ya maji mafupi na visima 8 vya bahari ya kina kirefu. Hatujabahatika kupata mafuta lakini tumefanikiwa kupata gesi asili katika maeneo kadhaa baharini na nchi kavu katika mikoa ya Mtwara, Lindi na Pwani.
Kwa mujibu wa taarifa zilizopo kutokana na visima vilivyochimbwa mpaka sasa, akiba ya gesi asili iliyopo nchini inakadiriwa kuwa kati ya futi za ujazo trilioni 25.4 – 28.9. Yapo matumaini makubwa ya gesi nyingi zaidi kugundulika katika miaka michache ijayo. Hii ni kutokana na ukweli kwamba shughuli za utafutaji mafuta na hasa gesi baharini zilizoanza mwaka 2004 kukiwa na kampuni moja sasa zipo 18. Baada ya ugunduzi wa kwanza wa gesi mwaka 2010, shughuli za utafutaji sasa zimepamba moto na zimekuwa na mafanikio. Naamini gesi nyingi zaidi itaendelea kupatikana.
Fursa za Maendeleo
Ndugu Wananchi;Kwa kiasi cha gesi asili kilichokwishagunduliwa na kwa matumaini yaliyopo ya gesi zaidi kupatikana kunaifanya Tanzania kuwa moja ya nchi za kutumainiwa duniani kwa upatikanaji wa gesi asili miaka michache ijayo. Hali hiyo inaipa nchi yetu fursa kubwa ya kuweza kujiletea maendeleo makubwa ya kiuchumi na kijamii muda si mrefu kutoka sasa.
Gesi asili ni rasilimali inayoweza kutumika kuzalisha mbolea na hivyo kusaidia katika kuendeleza kilimo nchini kwa kurahisisha upatikanaji wake na kuwa ya bei nafuu. Gesi asili inaweza kutumika kuzalisha umeme na hivyo kuiwezesha nchi kupata umeme wa kutosha na kuwepo ziada ya kuuza nje. Hivi sasa, katika gridi ya taifa megawati 350 za umeme zinatokana na gesi asili na hata lengo letu la kuzalisha megawati 3,500 ifikapo maka 2015 tunategemea zaidi gesi asili kuwezesha hilo kutimia. Ujenzi wa bomba la gesi kutoka Mtwara kuja Dar es Salaam una shabaha hiyo.
Ndugu Wananchi;
Vile vile, gesi asili inaweza kutumika kutoa nishati viwandani badala ya kutumia mafuta na hivyo kupunguza gharama za uzalishaji. Watu majumbani wanaweza kutumia gesi asili kupikia hivyo kupunguza matumizi ya umeme, mafuta, mkaa na kuni. Inapunguza gharama za maisha na kusaidia kuhifadhi mazingira kwa kupunguza ukataji wa miti. Ni kutokana na kutambua ukweli huo ndiyo maana TPDC inatekeleza mradi wa kutengeneza gridi ya mabomba ya kusambaza gesi majumbani katika jiji la Dar es Salaam.
Jambo lingine muhimu kuhusu rasilimali hii ni kwamba tukiuza nje gesi nchi yetu itapata mapato mengi tena ya fedha za kigeni. Kwa vile gesi ni nyingi mapato ya Serikali yataongezeka sana, hivyo kuijengea uwezo wa kutimiza majukumu yake vizuri zaidi. Kama matumizi yatakuwa mazuri, gesi asili itakuwa kichocheo kikubwa cha kukuza uchumi wa nchi. Maendeleo ya haraka yatapatikana na hivyo kusaidia kuwaondoa wananchi wengi kutoka katika lindi la umaskini tulionao sasa.
Changamoto Muhimu
Ndugu Wananchi;Pamoja na ukweli kwamba kuwa na gesi asili nyingi kunaipa nchi yetu fursa kubwa ya kujiletea maendeleo, zipo pia changamoto zake. Hatuna budi kuzitambua na kuzitafutia ufumbuzi ili gesi iweze kunufaisha ipasavyo nchi yetu na watu wake. Changamoto zipo nyingi lakini kubwa zipo za namna tatu.
Changamoto ya kwanza ni ile ya kujenga uwezo wetu wenyewe wa kudhibiti shughuli zinazofanywa na makampuni ya mafuta ili tuhakikishe kuwa tunapata malipo yanayostahili. Inatulazimu tuwe na wataalamu wetu wazalendo wa fani za taaluma zihusuzo gesi kama vile uhandisi, kemia, jiofizikia, uhasibu, ukaguzi na sheria. Tusipojenga uwezo wetu wenyewe kwenye maeneo hayo kuna hatari ya kudhulumiwa na kupata hasara. Pengine ipo haja ya kuwa na chombo maalum kwa ajili hiyo kama tulivyofanya kwa mafanikio kwa upande wa dhahabu.
Changamoto ya pili ni ile ya kupata Watanzania wengi wenye ujuzi na taaluma zinazohitajika na soko la ajira la sekta ya gesi. Tusipofanya hivyo makampuni yataajiri watu hao kutoka nje na hivyo kufanya Watanzania kutokunufaika na fursa za ajira zilizopo.
Ndugu Wananchi,
Kwa changamoto hizi mbili, jawabu lipo kwenye elimu na mafunzo tunayotoa kwa vijana wetu katika shule, vyuo vya ufundi na vyuo vya elimu ya juu. Kwanza kabisa lazima tuboreshe elimu ya sayansi na hisabati katika shule zetu za msingi na sekondari. Katika vyuo vya ufundi tutoe mafundi mchundo wa taaluma zinazohitajika na tasnia ya gesi na mafuta. Hivyo hivyo kwa upande wa vyuo vikuu nako wafundishe wataalamu wa fani zinazohitajika kama vile utafutaji wa gesi na mafuta, uendelezaji wa mafuta na gesi, uchumi na biashara ya mafuta na gesi, uhasibu na ukaguzi wa mafuta na gesi pamoja na sheria za mafuta na gesi na mikataba ya utafutaji na uendelezaji wa mafuta na gesi.
Ndugu Wananchi;
Napenda kuwahakikishia kuwa tayari tumejipanga kutafuta ufumbuzi wa changamoto hizo. Chuo Kikuu cha Dar es Salaam kinajiandaa kuanza kutoa mafunzo yaChemical and Environmental Lab for Oil and Gas na fani yaExploration and Production Software Technology katika mwaka huu wa masomo. Chuo cha Madini Dodoma kitaanza kutoa mafunzo ya diploma ya Petroleum Geoscience kuanzia Septemba mwaka huu. Chuo Kikuu cha Dodoma, Chuo cha Sayansi na Teknolojia cha Nelson Mandela Arusha, na Chuo cha Teknolojia cha Mbeya na kile cha Dar es Salaam pia wameanza kufundisha mitaala hiyo. Aidha, VETA Makao Makuu na VETA Mtwara nao wanafundisha masomo yahusuyo gesi. Wizara ya Nishati na Madini itawadhaminiwanafunzi 50 kutoka Mkoa wa Mtwara kwenda kupata mafunzo hayo ya gesi asili katika chuo cha VETA Mtwara.
Ndugu Wananchi;
Wizara ya Nishati na Madini pia inatekeleza mpango mkakati wa kuwapata wataalamu wa sekta hiyo kati ya 40-50 kati ya sasa na mwaka 2016. Taaluma zinazotiliwa mkazo ni Petroleum Geoscience, Petroleum Geophysics, Petroleum Geochemistry, Petroleum Engineering, Petroleum Modeling, Oil and Gas economics, Oil and Gas Accounting and Auditing na Oil and gas Legal Regimes and Contract Negotiations. Kwa upande wake, Serikali itatoa upendeleo maalum kwa kulipia gharama zote za mafunzo ili tuweze kuwapata wataalamu hawa mapema iwezekanavyo. Nawaomba vijana wetu wachangamkie fursa hizi za masomo na watakapohitimu mafunzo wawe tayari kuitumikia nchi yetu kwa bidii.
Kujenga Uwezo Wetu wa Kutumia Mapato ya Gesi
Ndugu Wananchi,Changamoto nyingine kubwa sana ni ile ya kuhakikisha kuwa mapato yatokanayo na gesi yanatumika vizuri na kwa manufaa ya taifa na watu wake. Lazima tuanze sasa kufikiria na kujipanga kwa ajili hiyo. Si vyema tukangojea mpaka hapo mapato yatakapoanza kupatikana ndiyo tufikirie na kutengeneza mfumo mzuri wa kusimamia na kutumia mapato yatokanayo na gesi. Tutakuwa tumechelewa, watu laghai na waovu watakuwa wameanza kunufaika hivyo watakuwa wagumu kutengeneza mfumo utakaowanyima fursa ya kuliibia taifa.
Jambo hili ni muhimu sana kufanya kwani ipo mifano hai ya nchi zenye rasilimali nyingi za mafuta na gesi lakini nchi na wananchi wake hawanufaiki sawia. Mauzo yanafanyika na fedha nyingi kupatikana lakini manufaa kwa nchi na watu wake ni madogo au hayapo kabisa. Wanaonufaika ni viongozi na baadhi ya maofisa wa umma wanaohusika na usimamizi wa shughuli zihusuzo rasilimali hizo. Na, hata sisi tunaweza kujikuta katika hali hiyo kama tusipojipanga vizuri sasa ambayo badala ya rasilimali kuwa baraka zinageuka kuwa balaa au hata laana.
Ndugu Wananchi;
Zipo nchi duniani ambazo zina usimamizi mzuri wa mapato ya rasilimali za mafuta na gesi na kuleta baraka na neema kwa taifa na watu wake. Nchi hizo zimeweza kuhifadhi na kutumia vizuri mapato yake kukuza uchumi wa nchi kwa jumla na kuboresha upatikanaji wa huduma za kiuchumi na kijamii kwa watu. Matokeo yake ni watu wa nchi hizo kuishi maisha yaliyo bora kuliko walivyokuwa kabla ya kupatikana kwa rasilimali hizo. Lakini, hii imewezekana kutokana na usimamizi mzuri na matumizi mazuri ya mapato yatokanayo na mafuta na gesi.
Tumeamua kujifunza kutoka nchi za wenzetu waliofanikiwa ili na sisi tunufaike. Na sisi tunajiandaa kutengemeza Sera ya Gesi Asili na kurekebisha Sheria ya Utafutaji na Uzalishaji wa Mafuta na Sheria ya Menejimenti ya Mapato ya Serikali yatokanayo na gesi zitakazotoa majibu hayo na kuliwezesha taifa kuwa na mfumo mzuri wa usimamizi wa utafutaji na uchimbaji wa gesi asili pamoja na usimamizi na matumizi mazuri ya mapato yatokanayo na gesi hiyo. Wapo wenzetu kwa mfano, wanacho kitu kinachoitwa Sovereign Funds ambapo mapato yote huhifadhiwa na baadae hutolewa kwa utaratibu maalum. Tunataka tujifunze kutoka kwao ili na sisi tutengeneze chombo chetu cha namna hiyo ili tunufaike.
Ndugu Wananchi;
Mambo hayo tumeshaanza kuyafanyia kazi. Katika mazungumzo yangu na baadhi ya wakuu wa nchi rafiki na mashirika ya maendeleo ya kimataifa, nimewasilisha maombi ya kusaidiwa na kushirikiana kwa mambo mawili. Kwanza kwa kuwawezesha Watanzania kupata mafunzo ya haraka kwa wataalamu watakaosaidia kusimamia shughuli za utafutaji, uendelezaji na biashara ya gesi asili nchini. Pili, watusaidie kupata watu wenye ujuzi na uzoefu ili watushauri kuhusu namna ya kutengeneza mifumo bora ya kusimamia na kutumia mapato ya gesi kwa mujibu wa mifano ya wenzetu waliofanikiwa. Nafurahi kwamba maombi yetu yamepokelewa vizuri na nchi zote na mashirika yote ya kimataifa tuliozungumza nao. Baada ya muda si mrefu kazi itaanza.
Mgomo wa Walimu
Ndugu Wananchi;Jambo la tatu na la mwisho ni mgomo wa walimu. Pengine ni mapema kusema kwa vile kesho Mahakama itaamua kuhusu shauri hilo. Lakini napenda kuwahakikishia walimu kuwa tunawajali, tunawathamini na kutambua mchango wao muhimu kwa taifa letu. Wakati wote tumekuwa tunashughulikia madai ya haki zao na malimbikizo mbalimbali. Madai ya safari hii ni makubwa mno, yametuzidi kimo. Athari za kuyatimiza yalivyo yataifanya bajeti ya Serikali kutumia asilimia 75 kwa ajili ya mishahara ya watumishi wa Serikali na kubakiza asilimia 25kwa kuendeshea Serikali na kutimiza majukumu ya maendeleo kwa wananchi. Haitakuwa sawa. Ndiyo maana tumeshindwa kuelewana walipokataa rai hiyo na wao kusisitiza kugoma.
Wakati tunaendelea kusubiri uamuzi wa Mahakama, nina maombi mawili kwa walimu: Moja, wasiwalazimishe walimu wasiotaka kugoma wafanye hivyo, wawaache waendelee na kazi. Pili, wasitumie watoto isivyostahili kujenga hoja zao. Nawasihi warudi kwenye meza ya mazungumzo.
Ndugu Wananchi;
Kabla ya kumaliza hotuba yangu naomba nitumie fursa hii kuwatakia Waislamu wote nchini kheri na baraka tele kwa swaumu ya mwezi mtukufu wa Ramadhan. Wakati wote, mjiombee wenyewe kwa Mwenyezi Mungu awajaalie toba na malipo mema katika mfungo huu. Mkumbuke pia kuiombea nchi yetu amani, upendo na mafanikio mema.
Baada ya maneno hayo, naomba sasa niishie hapo. Nawashukuru sana kwa kunisikiliza. Sasa nipo tayari kujibu maswali ya Wahariri kama yapo. Ndugu Wahariri mliopo hapa, karibuni.
No comments:
Post a Comment