Tafuta/Search This Blog

Thursday, May 12, 2011

MAKOMANDOO VHM WAICHOMA MOTO AIRPORT YA WACHAWI HANDENI TANGA!!!!

Salaam sana katika jina la Yesu Kristo.

Ama kwa hakika Mungu anatenda mambo ya ajabu sana.

Huduma ya VHM Tanzania kupitia kikosi chake cha mashambulizi wiki hii, kilitua na kupiga kambi katika wilaya ya Handeni mkoani Tanga katika moja ya vijiji sugu vilivyo jaa nguvu za giza, uchawi na mambo ya kishirikina. Ilikuwa ni wiki la mapambano makali sana katika ulimwengu wa roho na katika ulimwengu wa mwili pia.

Roho za uchawi, uasherati na uzinzi zimekandamiza sana vijiji hivi vya Handeni na kuwafanya wakazi wake kuishi kwa shida bila matumaini yeyote.

Hili lilikuwa ni wiki la kufunga na kuomba pamoja na kupambana na mkuu wa anga la vijiji hivi ili tutakapokwenda kuhubiri, watu wawe wamelainishwa mioyo yao tayari kwa kupokea injili ya Bwana wetu Yesu Kristo.



KAMBI YA WAEBRANIA VIJIJI VYA HANDENI




Hapa ndipo mahali ambapo jeshi la Bwana kikosi cha wakata “network za shetani” kilipoweka kambi katika kijiji hiki hapa handeni. Hawa ni watu wenye kazi zao na biashara zao za maana tu, lakini hawakujali kuacha nyumba zao nzuri na kuja kuishi hapa chini ya miti na kulala chini ili kufunga na kuomba kwa ajili ya kupambana na mkuu wa anga ili aweze kuwaachia huru watu wa Mungu katika vijiji hivi.

Mkuu wa anga huwa hafanyi kazi peke yake, ameweka ma agent wake ili kukamilisha kazi zake. Katika kampeni hii ya kuvunja kazi za shetani tulifanya utafiti na tukagundua maeneo mbalimbali ambayo mkuu wa anga anafanya kazi kupitia ma agent wake alio waweka kuifanya kazi yake.

Tulifanikiwa kupenya katika nyumba zote za waganga na wachawi maarufu kijijini hapo na kufanya maombi ndani ya nyumba zao bila wao kujua. Tuliingia kwa wachawi na tulijifanya kama wateja wanaotafuta kufanyiwa ramri ili tuweze kupata tiba na kuwajua wabaya wetu. Ilikuwa patashika nguo kuchanika.



HII NDIYO AIRPORT YA KUPOKEA NA KURUSHA NDEGE ZA KICHAWI



Hii inayoonekana katika picha hizi hapo juu, inajulikana kama AIRPORT ya wanga na wachawi. Katika msitu huu, hapa ndipo ndege zote za ungo zinapotua na kupaa kutoka na kwenda sehemu mbalimbali hapa nchini na hata nje ya nchi kwa kutumia ungo na vifaa vya kichawi.

Kwa kawaida, msitu huu ambao wanakijiji wameupa jina la airport, mali na shughuli za usafiri wa kichawi, eneo hili lenye ukubwa wa zaidi ya hekali mia moja, hutumika pia kwa shughuli za matambiko ya kimizimu pamoja na shughuli za kichawi. Mti unaoonekana katika picha ya juu hutumika kuhifadhi mimba za wanawake ambao mara tu baada ya kupata ujauzito mimba zao huchukuliwa kichawi na kufungwa juu ya mti huu. Wanawake hao hubakia na matumbo makubwa lakini ndani yake hakuna kitu. Tulikutana na wanawake wajawazito ambao mimba zao zimechukua zaidi ya miaka miwili na bado hawana dalili zozote za kujifungua.

Picha hiyo ya mwisho hapo juu, ni picha ya kaburi ambalo limechimbwa kichawi. Kazi ya kaburi hilo ni kuwavuta watu kimazingara na kuwazika humo kichawi na huyo mtu aliyezikwa humo kichawi ndio atakuwa amepotea ghafla au kuanguka ghafla na kufa, lakini katika hali halisi atakuwa amehamia katika ulimwengu mwingine.

Tumekutana na mambo makubwa sana na ya ajabu ya kushangaza. Tangu tumeanza huduma hatujakutana na maruweruwe kama tuliyoyaona katika kambi hii ya maombi.



USIKU WA UVAMIZI KWENYE UWANJA WA WACHAWI



Huu ni usiku ambao huwenda sitausahau katika maisha yangu yote. Ulikuwa ni usiku wa kuwavamia wachawi na wanga wakiwa wametua katika uwanja wao huo kufanya shughuli zao kisha kuruka kuelekea katika miji tofauti walikotoka. Ilikuwa ni kama MOVIE ya kinaijeria, lakini ilikuwa ni kweli na LIVE, maana mimi mwenyewe nilikuwepo katika msafara huo.

Tulivamia airport hiyo usiku wa saa nane kabla hawajaruka kurudi walikotoka. Lengo letu ilikuwa ni kuwakamata na kuwapeleka katika kambi yetu ya maombi ili tuweze kuwashughulikia vizuri. Katika operation hii tuliteua makomandoo kama 11 kufanya uvamizi huu usiku wa manane. Tulipoingia katika msitu huo, tulikuwa tukitembea kwa kunyata mithiri ya mwizi anayetaka kuiba bila kusikika. Tulikokuwa tumekaribia uwanja huo, wachawi hao walihisi uvamizi huo na ndipo lilipotimia lile neno linalosema adui watakuja kwa njia moja na watatawanyika kwa njia saba. Hivyo ndivyo ilivyokuwa. Wachawi hao walitimua mbio na kupepea kama karatasi na kutokomea.

Kwa sababu tulikuwa tumewakurupusha, waliacha baadhi ya vifaa vyao walivyokuwa wakivitumia hapo airport yao. Hapo ndipo tulipopata wasaa kukusanya kila kitu chao kilichokuwepo hapo kwenye airport yao, usiku huo huo tulikwenda kutafuta moto na tukavipiga moto na kuvisimamia vikiteketea kwa moto mpaka vilipomalizika vyote ndipo tuliporudi kwenye kambi yetu na kuendelea na maombi. Picha ya tatu kutoka kushoto ni kaburi la kichawi ambalo hutumika kupotezea watu, kaburi hilo nalo tulilichoma moto. Katika vijiji hivyo kuna taarifa nyingi za watoto wengi na baadhi ya watu wazima kupotea katika mazingira tata na mpaka leo hawajawahi kupatikana.



KUZAMIA


Unaweza kuona na kuhisi jinsi ambavyo kikosi chetu cha mashambulizi kilivyokuwa kikiomba kwa uchungu na mzigo dhidi ya mambo ambayo shetani anayafanya katika vijiji hivyo. Ilikuwa ni wiki la kazi moja tu kuomba na kushambulika ngome na vichaka vya shetani. Tuliweza kuona jinsi shetani anavyowatesa watu na kuwadhalilisha watu. Tuliona waganga wakiwachukuwa watu wazima na kuwapeleka kwenye vidimbwi na kuwavua nguo na kuwaogesha wakiwa uchi tena hadharani mchana peupe ili kuwaondoa nuksi. Hii ndiyo sababu tulikuwa tukiomba kwa uchungu kwa ajili ya ukombozi wa watu hawa


KUFUTURU

Baada ya mfungo huo mzito wenye misukosuko mingi, huu ulikuwa wakati wa kufungulia na kupata chochote kwaajili ya tumbo maana ulikuwa ni mfungo mzito sana lakini Mungu alitutia nguvu sana. Tuliziona nguvu zisizo za kawaida ndani yetu na ndipo tulipoungana na mtume Paulo pale aliposema “sio mimi ninayeishi bali Kristo ndani yangu” Wanakijiji walikuwa wanatuhurumia sana kwani msitu huo huwa hauingiwi na watu wa kawaida na kama mtu asiyehusuka akiingia hata kama ni kwa bahati mbaya, basi atakuwa kichaa au akiingia na viatu atapata matende na wakati mwingine atauwawa kichawi kabisa. Hayo ndiyo wanakijiji waliyoyategemea kuyaona yakitokea kwetu kwani hatukuiheshimu mizimu yao. Pamoja na mambo yote hayo Mungu ametutetea hakuna aliyejikwaa wala hata mafua. TUPO NGANGALI KATIKA BWANA YESU KRISTO.

Wiki hii tunapeleka kikosi kingine kule KILWA mahali tulipokuwa tumefanya huduma wiki chache zilizopita ili kwenda kuimarisha kazi tuliyoianzisha na kuwatia moyo kondoo waliompa yesu maisha wakati wa misheni hiyo.

Tunahitaji sana uwezesho ili kazi hii iweze kusonga mbele.


If you would like to support this Ministry and Mission:

THE VOICE OF HOPE MINISTRIES

NBC VICTORIA BRANCH

A/C NO. 074103001247

M-pesa 0767 56 39 39

Tigo-Pesa 0713 18 39 39

In Christ

Peter Mitimingi.



NB: Tunamfahamu vyema kaka Peter Mitimingi ambaye ni mratibu wa hii huduma. SBP tunaipongeza sana hii huduma na wote waliojitolea kuifanya kazi ya Mungu na tutaendelea kuwapatia taarifa wananchi/wapendwa.

1 comment:

Anonymous said...

Mungu awatiee Nguvu mnakaribishwa kuweka na kambi Dodoma maaan Dodoma ikipona Tanzania Imepona