Tafuta/Search This Blog

Tuesday, July 31, 2012

Papaa On Tuesday......Ukitaka Kukubalika na Kila Mtu Utaboa.


Wakati Walimu Wakiwa Wanaingia Katika siku ya pili ya Mgomo Wao Usiokuwa na Kikomo siku ya Leo, Bungeni kunatarajiwa kulipuka kwa hoja ya kuhusiana na mgomo wa Madaktari sababu Wizara ya Afya na Ustawi Wa jamii iliwasilisha Makadirio ya Mapato na Matumizi jana pamoja na mdahalo wa kuchangia siku ya leo.

Ninawasalimu Wasomaji Wangu wa ndani na nje ya nchi, nimefarijika sana baada ya kupokea simu za Waheshimiwa Wabunge Wanaofatilia Blog yangu hususan Papaa On Tuesday, siku si nyingi nitakuwa nanyi Mjengoni na kuandika Papaa On Tuesday nikiwa Bungeni, yote ni heri na Kila Jambo na Majira yake.

 Zangu salamu leo nazipeleka kwa wasomaji wangu walio kule hydom, maeneo ya Mbulu, Babati, Dongobesh na maeneo ya Jirani. Miaka michache iliyopita nakumbuka nilipita Kiteto nikaenda Mbulu, Kutoka Mbulu nilichukua landrover mpaka Dongobesh ambako nilifanya makazi yangu kwa Mchungaji wa KKKT Zakayo Malekwa. Ni safari yenye kukumbukwa sana. Siku chache zijazo nitakuwa huko Hydom kwa project mpya ya Blog nikishirikiana na Mwenyeji wangu Amani Paul Mzee Wa Kambi Popote.

Katika muda mchache nilioishi hapa duniani zaidi ya miaka 30 nimebaini huwezi kukubalika na kila mtu hata wale unaodhani ungetaka wakukubali katika kile unachokifanya. Kuna wakati nilikuwa na wakati mgumu sana kutaka kila mtu anielewe katika kila ninachofanya mwisho wa siku nilikua naumia hata baada ya kutaka kuwapendeza nikagundua bado kuna watu hawanikubali katika ninachokifanya.

Mara kadhaa nimefadhaika baada ya kuona hata lile ninalofanya kwa ajili ya Jamii kwa gharama zangu na muda wangu bado pia watu hawakukubali, mmoja wa marafiki zangu wa jinsia ya kike mara zote ninapokuwa niko disappointed huwa ananiambia maneno machache lakini yenye kunifikirisha kwanza huwa ananiambia "Think Positive and Take It Positive" na wakati mwingine huniambia "Nini sababu ya wewe kufanya, unataka kukubalika ama kutimiza kusudi?". Utakuwa unajisikia vibaya zaidi iwapo ulikuwa unataka kufanya ili ukubalike na kama kila kitu watu wanachosema unachukulia negative/hasi basi jua utavunjika moyo.
Mwana wa Mungu, Yesu Kristo hakukubalika na kila mtu sembuse wewe mtoto wa Filikunjombe?Duniani kuna watu wanamakwazo sana na kuna mtu mwingine yaani hakukubali hata kama haujafanya lolote. Maofisini kwetu ama hata makanisani na Jamii kwa ujumla kuna mtu inatokea tu hakukubali na pengine mpaka mtagombana, au anakukasirikia bila hata sababu na unaooteza muda kutafuta suluhu lakini haipatikani mwisho wa siku utasikia "damu yake na yangu haziendani".

Ukifanya mema duniani kuna watu watakukubali na kuna watu hawatakukubali wataona unatafuta tu sifa, ukifanya mabaya kuna watu watakukubali na kuna watu hawatakukubali, maana kila uovu una wafuasi wake. Ukitafuta kukubalika utaboa kwenye maisha yako.

 
Chochote ambacho unafanya kwa nia njema na una amani ya moyoni ambacho si uovu basi fahamu kuwa huwezi kukubalika na kila mtu. Mambo mangapi umefanya ambayo watu hawakukuelewa hata ulipowaelewesha lakini yamkini jambo hilo Mungu ameliruhusu kwenye maisha yako. Take it Positive kuna kujifunza katika kila shutumu ama lawama toka kwa watu wasiokukubali, yamkini wanachokiongea ukikitendea utakuwa bora zaidi. Katika kutimiza ndoto za maisha yako huwezi kupata wa kukupigia makofi kuna wakukuzomea pia na kukung`ong`a ili uweze kujitahidi. Biblia inasema jitahidi kwa bidii kuwa na amani na kila mtu suala la wao kukubali ama kuto kukubali ni uamuzi wao, usipoteze muda kumpendezesha mtu na kumkwaza Mungu, wanadamu wana yao. Ukitaka kila mtu akupigie makofi katika yale unayofanya basi jua kuna uwezekano mkubwa usitimize ndoto yako ukawa unatimiza ndoto za wengine.

Ukiwa mfugaji mkubwa watasema, ukiwa mfugaji mdogo watasema,ukiwa tajiri watasema, ukiwa masikini watasema, ukiwa mrefu watasema ukiwa mfupi watasema, Ukiwa mwembambaaaa watasema, Ukiwa Umejazia jazia Watasema, na hata usipokuwa chochote watasema.


Kila Mtu ameumbwa kwa namna ya tofauti, Kuna watu watakuchukia tu sababu unaweza kufanya wao hawawezi, Kuna watu watakuchukia sababu ya kazi yako, Kuna Watu watakuchukia sababu Cheo Chako anaona yeye ndiye anastahili, Kuna Watu Watakuchukia Sababu wewe huwa huchukii, Kuna watu leo hauna relationship ni ma best zako siku ukiwa na relationship utaona watu wanakuchukia, ukisema leo unaenda kuishi nje ya Tanzania kuna watu watakuchukia, Ukiamua leo Kuwa Mtakatifu kuna watu watakuchukia. Huwezi Kumpendeza Kila Mtu Utaboa

Mungu alituumba tofauti tofauti Kwa Sababu, Mungu akatupa utashi tofauti kwa Kila Mtu Kwa Sababu, Ukianza kuishi ili Kumpendeza fulani ama group fulani utaishia kupoteza Identity yako. Uliumbwa Kwa Sababu haukuumbwa kama boya, uko duniani kwa makusudi maalum wewe ni Project Manager wa Mungu duniani, Kuna Kitu Mungu anataka kufanya duniani kupitia wewe. Kulazimisha baadhi ya mambo kwenye maisha ni kupoteza kile ambacho Mungu anataka, Samaki hafundishwi kuogelea, Wala hakuna kisu kinachoenda Kujifunza Kukata, Kuna vitu vimo ndani yako hauhitaji Kujitahidi ili kuweza kufanya, huwa situmii Msuli Mkubwa Kuandika Papaa On Tuesday, Huwa Situmii Msuli kuongea, sababu ni Kama Samaki yuko baharini Kuogelea ni lazima, ninatambua kuna watu hawapendi vile nilivyo, Lakini Siishi Wao Watakavyo, Ila naishi nitakavyo.


Think Differently and Make a Difference.

Wanafunzi wamshushia kipondo mwalimu aliyeasi mgomo

Kufuatia mgomo huo, baadhi ya shule wanafunzi wake waliingia mitaani kuandamana
Na Gideon Mwakanosya, Songea.

MWALIMU mmoja wa jinsia ya kike aliyefahamika kwa jina moja la Kahimba wa shule ya msingi ya Kambarage iliyopo Kata ya Msamala katika Halmashauri ya Manispaa ya Songea Mkoani Ruvuma amajeruhiwa vibaya kwa kupigwa sehemu mbalimbali za mwili na kundi linalodaijwa kuwa ni la wanafunzi wa shule hiyo ambao wanadaiwa kuwa na hasira baada ya walimu wengi wa shule hiyo kutoonekana eneo la shule kufuatia mgomo wa chama cha Walimu (CWT).

Akizungumuza na waandishi wa habari hizi Mjini Songea mwalimu mkuu wa shule ya msingi Kambarage Adolfina Ndunguru alithibitisha kutokea kwa tukio hilo ambalo alidai kuwa ni udhalilishaji mkubwa kwa mwalimu kupigwa na wanafunzi.

Ndunguru alisema kuwa yeye pamoja na walimu wenzake hawakuweza kufika kwenye eneo la shule kwa kuwa wao ni walimu ambao wamekubaliana kugoma kutokana na Serikali kushindwa kutimiza ahadi yao wanayodai.

Alifafanunua kuwa inadaiwa kundi la wanafunzi lilipomuona mwalimu Kahimba kwenye eneo la shule hiyo lilimvamia na kuanza kumpiga mawe sehemu mbalimbali za mwili na baadaye alifanikiwa kukimbia.

Kwa upande wa baadhi ya walimu wa shule za msingi, Sekondari na Chuo cha Ualimu cha Songea kilichopo Manispaa ya Songea ambao wameomba majina yao yahifadhiwe walisema kuwa mgomo utaendelea mpaka Serikali itakapo ridhia kuwalipa madai yao hasa ikizingatiwa kuwa wao wanafanyakazi katika mazingira magumu.


hawa kwa upande wao, waliona ni heri kubakia darasani wafundishane wenyewe kile wanachokijua

Waandishi wa habari walifanikiwa kutembelea baadhi ya shule za Msingi na sekondari ambazo zilikuwa hazina walimu kabisa na kwamba wanafunzi wa shule hizo wakiwa wamezagaa mitaani huku wakiinung`unikia Serikali kwa kuto watendea haki walimu wao ambao alikuwa wakiwaandaa wanafunzi katika Mitihani ya kumaliza Elimu ya Msingi na sekondari.
Shule zilizotembelewa na waandishi wa habari ambazo hazikuwa na walimu kabisa ni Shule za Msingi za Matarawe, Mwembechai, Sabasaba, Mkombozi, Kawawa, Mfaranyaki, Majengo, Songea, Kambarage, Msamala na Majimaji na shule za sekondari za matarawe, Mfaranyaki, Shule ya wavulana

Songea na Shule ya wasichana songea.
Kwa upande wake mmoja wa wanafunzi wa shule ya msingi Majimaji Tamimu Ajali anayesoma darasa la tano ameiomba Serikali kuharakisha kutekeleza madai ya walimu wanayodai kwani bila kufanya hivyo kunauwezekano mkubwa wa kushuka kwa kiwango cha Elimu hasa ikizingatiwa kuwa wanafunzi wapo kwenye maandalizi ya kufanya mitihani.

Tamimu alisema kuwa ni vyema serikali ikatambua umuhimu wa mwalimu kwa kumuuongezea mshahara sawa na taaluma zingine muhimu kwa mfano. Wanajeshi, Madaktari,Wauguzi na wahudumu wa afya.

Afisa Elimu wa halmashauri ya Manispaa ya Songea Fulgensi Mponji amethibitisha kuwepo kwa mgomo huo wa walimu amabapo alisema Manispaa hiyo ina shule 72, Sekondari za Serikari 23, Shule za seskondari za binafsi 13 ambazo idadi kubwa ya walimu hawakuwepo kwenye maeneo yao ya kazi.
Alisema kuwa tayari ameshawaagiza walimu wakuu wa shule za msingi na waratibu Elimu kata wote kukutananao katika shule ya msingi Mfaranyaki kwa lengo kuwakutanisha walimu ili kuzungumzia namna ya kutatua tatizo hilo.

Naye Katibu wa chama cha walimu mkoa wa Ruvuma Luya Ng`onyani alisema kuwa mgomo huo ni halali na umezingatia sheria ya ajira na mahusiano kazini ya mwaka 2004 kifungu cha 80 (1) ambapo hatua ya kwanza CWT kwa niaba ya wanachama tayari imetekeleza kutangaza mgogoro wa siku 30 kwa kujaza fomu CMA No: 1.

…imenakiliwa kutoka wavuti…

Friday, July 27, 2012

Napinga Ukweli...

Napinga Ukweli kuwa Titi la mama ndio tamu hata kama la mbwa....
Huyu dogo hataki kabisa kunyonya kwa mamaye... amevutiiwa na titi hili............

HOTUBA YA KAMBI RASMI YA UPINZANI; WIZARA YA NISHATI NA MADINI Friday, July 27, 2012

HOTUBA YA MSEMAJI WA KAMBI RASMI YA UPINZANI BUNGENI WIZARA YA NISHATI NA MADINI JOHN JOHN MNYIKA (MB) KUHUSU MAONI YA KAMBI RASMI YA UPINZANI JUU YA MAPITIO YA UTEKELEZAJI WA BAJETI YA MWAKA 2011/2012 NA MAKADIRIO YA MATUMIZI YA WIZARA YA NISHATI NA MADINI KWA MWAKA WA FEDHA 2012/2013


UTANGULIZI

Mheshimiwa Spika,
awali ya yote niungane na wote wenye mapenzi mapema katika kuomba ulinzi wa Mwenyezi Mungu wakati tukitimiza wajibu wa kibunge kwa mujibu wa ibara ya 63 ya Katiba ya Jamhuri wa Muungano wa Tanzania na Kanuni Kudumu za Bunge (Toleo la mwaka 2007) kifungu cha 99 (7) wa kuishauri na kuisimamia serikali; kwa kuwasilisha maoni ya Kambi Rasmi ya Upinzani kuhusu mapitio ya utekelezaji wa bajeti ya mwaka 2011/2012 na makadirio ya matumizi ya Wizara ya Nishati na Madini kwa mwaka wa fedha 2012/2013.

Mheshimiwa Spika, nitumie pia nafasi hii kuwashukuru Watanzania wenzangu wa kada, hadhi na ngazi mbalimbali katika taasisi na maeneo mengi ndani na nje ya nchi waliouniunga mkono kwa hali na mali katika kipindi chote cha misukosuko ya kusimamia ukweli na uwajibikaji: katika kuifuatilia serikali na kuunganisha wadau wengine kuwezesha maendeleo katika jimbo la Ubungo; wakati wa kesi ya kupinga matokeo ya ushindi wetu; wakati wa operesheni za 2

kuhamasisha mabadiliko katika maeneo mengine nchini na katika uwakilishi wa wananchi bungeni. Utaratibu wa kupokea maoni na kutoa taarifa za mara kwa mara za maendeleo kupitia mikutano na wananchi pamoja na katika mtandao wa http://mnyika.blogspot.com tutaendelea nao. Kaulimbiu yetu ni ile ile: AMUA; Maslahi ya Umma Kwanza.
Mheshimiwa Spika; Sekta za Nishati na Madini zina umuhimu maalum katika uchumi wa nchi na maisha ya wananchi katika kipindi cha sasa na muda mrefu ujao. Wakati nishati ikiwa nyenzo ya kuendesha maisha ya kiuchumi, kisiasa na kijamii ya wananchi na nchi kwa ujumla; madini ni mtaji na ni kati ya mitaji mikubwa ya kuwezesha maendeleo ya haraka ya taifa. Hata hivyo, pamoja na Tanzania kujaliwa rasilimali hizi nyingi ikiwemo watu, ardhi yenye rutuba, maji (bahari, mito na maziwa), kuwa katika eneo la kimkakati la kijiografia kwa biashara na maliasili, bado takwimu za hali ya uchumi kwa mwaka 2011 zinaonyesha sehemu kubwa ya Watanzania wako kwenye lindi la umaskini.

Mheshimiwa Spika, tunajadili sekta za nishati na madini wakati taifa likiwa kwa mara nyingine tena kwenye tishio la mgawo wa umeme pamoja na serikali kukanusha kwamba hakutakuwa na mgawo wa umeme. Tunajadili mapitio ya utekelezaji wa bajeti ya mwaka 2011/2012 wakati kwa mara nyingine tena kukiwa na mvutano 3

baina ya watendaji waandamizi wa Wizara ya Nishati na Madini na Taasisi zake wakiwa katika mvutano ambao umeambatana na kutuhumiana hadharani kupitia vyombo vya habari juu ya tuhuma za ubadhirifu na matumizi mabaya ya madaraka. Tunajadili makadirio ya mapato na matumizi ya Wizara ya Nishati na Madini kwa mwaka 2012/2013 wakati kukiwa na tuhuma za vigogo wa serikali kuingiziwa fedha kifisadi katika akaunti zao za nchini Uswisi na makampuni ya nje ya utafutaji na uchimbaji wa madini, mafuta na gesi asili huku viongozi wa dini wakiwa wamezindua ripoti juu ya ukwepaji kodi na upotevu wa mapato kwa serikali unaogusa pia makampuni kwenye sekta za nishati na madini (The One Billion Dollar Question).
Mheshimiwa Spika, namuomba kila mmoja wetu atafakari kwa ukweli wa nafsi na nafasi yake tumefikaje hapa kama taifa na kwa pamoja tukubaliane kuwa wabunge tuwajibike kuisimamia serikali kuhakikisha maazimio yote ya bunge kuhusu sekta za nishati na madini ya miaka mbalimbali yanatekelezwa kwa haraka na kwa ukamilifu. Naamini iwapo maazimio ya Bunge juu ya Mkataba baina ya TANESCO na Kampuni ya Richmond Development Company LLC yangetekelezwa yote na kwa wakati toka mwaka 2008, maazimio ya bunge juu ya uendeshaji wa sekta ndogo ya gesi asili ya mwaka 2011 yangezingatiwa yote na kwa haraka, maazimio kuhusu uhalali wa utaratibu wa Wizara ya Nishati na Madini kuchangisha fedha kwa ajili ya kupitisha bajeti bungeni ya mwaka 2011 yangechukuliwa 4

kwa uzito unaostahili; taifa lingeepushwa kurudia mijadala ile ile kuhusu Wizara hii hii mara kwa mara. Aidha, kambi rasmi ya upinzani inatoa mwito kwa bunge kupitisha maazimio ya kutaka uwajibikaji wa serikali kwa kushindwa kutekeleza maazimio ya bunge kwa ukamilifu na kwa wakati.
Mheshimiwa Spika, kwa mujibu wa Katiba ya Nchi Ibara ya 52 (1) Waziri Mkuu ndiye mwenye madaraka juu ya udhibiti, usimamiaji, utekelezaji wa siku hata siku wa kazi na shughuli za Serikali ya Jamhuri ya Muungano na ndiye kiongozi wa shughuli za Serikali Bungeni. Ni muhimu basi, badala ya kupokea majibu ya Wizara ya Nishati na Madini pekee ambayo imeendelea kugubikwa na lundo la tuhuma mbalimbali, Waziri Mkuu atoe kauli bungeni kuhusu kujirudia rudia kwa madai ya ufisadi na uzembe katika sekta za nishati na madini.

Aidha, pamoja na mabadiliko ya Mawaziri, Manaibu waziri, Makatibu wakuu na Wakurugenzi wa Wizara ya Nishati na Madini na taasisi zake ya mara kwa mara, Rais ashauriwe kutumia nguvu zake za kikatiba za ibara ya 33, 34, 35 na 36 kuwezesha hatua za kisheria kuchukuliwa kwa wote waliotuhumiwa kwa ufisadi, uhujumu uchumi na matumizi mabaya ya madaraka kwa mujibu wa maazimio ya bunge na taarifa mbalimbali za serikali ili kurejesha misingi ya uadilifu na uwajibikaji katika sekta za nishati na madini. 5

Mheshimiwa Spika, hivyo kwa ujumla mjadala wa mapitio ya utekelezaji wa bajeti kwa mwaka wa fedha 2011/2012 na makadirio ya matumizi ya Wizara ya Nishati na Madini kwa mwaka wa fedha 2012/2013 ulenge katika kuliepusha taifa letu kuendelea kutumbukia katika ‘laana ya rasilimali’ kama ilivyojitokeza katika mataifa mengine. Tuhakikishe tunalinda uhuru wa taifa letu dhidi ya uporaji wa ardhi na rasilimali zake yakiwemo madini, mafuta na gesi asili ulio katika tishio la ubeberu mamboleo, ufisadi na udhaifu wa kimifumo. Aidha, kupitia mchakato wa katiba mpya wananchi watoe maoni ya kuhakikisha kuwa rasilimali za muhimu ikiwa ni pamoja na madini, mafuta na gesi zinawekewa mfumo wa kunufaisha watanzania wote na pia mikataba kuhusu rasilimali hizo inaridhiwa na Bunge.

Tuchangie mjadala wa sekta hizi nyeti tukikumbuka maneno ya hayati Mwalimu Nyerere katika kitabu chake cha TUJISAHIHISHE cha mwaka 1962, nanukuu: "Lakini woga unaweza kutokana na tamaa ya kila binadamu kupendwa na binadamu wenzake. Sisi wote tunayo tamaa hii, au sivyo tusingekuwa binadamu. Woga huu huweza ukamfanya mtu kuvumilia maovu, hasa kama maovu yale yanatendwa na walio wengi kwa walio wachache, au yanatendwa na wakubwa kwa wadogo. Kwa kuogopa kuwaudhi wengi tunawaacha watende makosa bila kuwasahihisha, wasije wakatuchukia. Huu ni ubinafsi mbaya sana" 6

MAPITIO YA UTEKELEZAJI WA BAJETI YA MWAKA 2011/2012

Mheshimiwa Spika,
tarehe 15 Julai 2011 niliwasilisha bungeni maoni ya Kambi Rasmi ya Upinzani kuhusu mapitio ya utekelezaji wa bajeti ya mwaka 2010/2011 na makadirio ya matumizi ya Wizara ya Nishati na Madini kwa mwaka wa fedha 2011/2012. Kufuatia maoni hayo, yapo masuala machache ambayo Serikali imeyazingatia kwenye utekelezaji na mengine mengi serikali haikuyazingatia pamoja na umuhimu wake kwa maslahi ya nchi na maisha ya wananchi. Hivyo kupitia mapitio haya ya utekelezaji, Kambi Rasmi ya Upinzani inaitaka serikali ieleze hatua ilizochukua juu ya maoni hayo ambayo baadhi yalijitokeza pia kwenye maoni ya Kamati za Kudumu za Bunge na michango ya wabunge kwa nyakati mbalimbali. Hakuna sababu ya kutumia muda mrefu kutoa na kujadili maoni mapya ikiwa hakuna mfumo thabiti wa kuhakikisha maoni na maazimio yanatekelezwa kwa wakati na kwa ukamilifu.

Mheshimiwa Spika, Kambi Rasmi ya Upinzani ilipitia kitabu cha pili cha matumizi ya kawaida ya Wizara ya Nishati na Madini (Volume II Supply Votes) Fungu la 58 kwa mwaka wa fedha 2011/2012 na kubaini kwamba ilikuwa ni bajeti ya mgawo mkubwa wa posho na ufujaji ya zaidi ya shilingi bilioni 7.9 ya posho na matumizi mengine yasiyo ya lazima. Kambi Rasmi ya Upinzani iliitaka serikali ifanye marekebisho kwenye bajeti ili fedha hizo zipunguzwe na kuelekezwa kwenye kuongeza ujenzi wa miundombinu wa Chuo Cha Madini Dodoma na kuongeza kiwango cha fedha katika mfuko wa 7

wachimbaji wadogo wa madini. Aidha, yako matumizi mengine ya ujenzi wa maofisi na gharama kubwa za kisheria yaliyopaswa kuhamishiwa katika miradi muhimu ya maendeleo ikiwemo ya umeme vijijini. Kwa kuwa Wizara iliahidi kuufanyia kazi ushauri wa kupunguza matumizi yasiyokuwa ya lazima, Kambi Rasmi ya Upinzani inaitaka Serikali kueleza kiwango cha fedha kilichookolewa kutokana na kutekeleza ushauri huo na kutoa pia maelezo ni kwanini katika makadirio ya mwaka 2012/2013 pamejitokeza kwa mara nyingine tena matumizi yasiyokuwa ya lazima.
Mheshimiwa Spika, Kambi Rasmi ya Upinzani ilitaka kiwango cha bajeti ya Wizara ya Nishati na Madini kuongezwa ili vipaumbele vifuatavyo viweze kuzingatiwa kwa uzito unaostahili: Kuwekeza fedha za kutosha kwenye sekta ya umeme na Gesi ili kumaliza kabisa tatizo la nishati ya Umeme na kupunguza gharama za maisha. Hatua hizo ziambatane na kuwekeza katika Bomba la Gesi, pamoja na ujenzi wa mtambo wa kutengeneza Gesi (LPG extraction Plant) ili kuwezesha gesi kutumika kwenye magari, viwandani na majumbani; kuhakikisha tunazalisha 360MW za umeme kila mwaka ili kufikia malengo ya Mpango wa Maendeleo wa miaka Mitano na kumaliza tatizo la mgawo wa umeme na mwisho kutenga fedha za kutosha kwa ajili ya usafirishaji na usambazaji wa umeme vijijini ili kuchangia katika ukuaji wa uchumi vijijini.

Kusuasua kwa utekelezaji wa mpango wa dharura wa umeme 8

Mheshimiwa Spika, ili kushinikiza nyongeza hiyo ya bajeti na utekelezaji wa vipaumbele hivyo, Kambi Rasmi Bungeni ilipendekeza bunge kupitisha azimio la kutangaza kwamba ukosefu wa nishati ni janga la taifa na kupitisha mpango wa dharura na maamuzi ya hatua za haraka ambazo serikali inapaswa kuzichukua kwa uwajibikaji wa pamoja. Tarehe 18 Julai 2011 Waziri Mkuu Mizengo Pinda alikubaliana na mapendekezo yetu na hivyo wakati anatoa hoja ya kuahirisha majumuisho ya mjadala wa makadirio ya mapato na matumizi ya Wizara ya Nishati na Madini akaahidi kwenda kukata fedha kwenye posho na matumizi mengine yasiyokuwa ya lazima katika bajeti ya serikali ili kuelekeza fedha kwenye mradi wa dharura wa umeme.

Mheshimiwa Spika, hata hivyo inaelekea ahadi hiyo ilikuwa hewa kwani tarehe 13 Agosti 2011 Serikali ikageuka na kuleta mpango wa dharura tofauti ambao ulijikita katika serikali kuidhamini TANESCO kwenda kukopa kwenye mabenki ya kibiashara zaidi ya bilioni 400. Pamoja na kuikumbusha serikali bungeni kutekeleza ahadi hiyo ya Waziri Mkuu, serikali ilipuuzia ushauri uliotolewa. Matokeo yake mpaka sasa Shirika la Umeme (TANESCO) halikuwezeshwa kupata kiwango cha fedha kilichopangwa na utekelezaji wa mipango husika kusuasua.

Mheshimiwa Spika, ikumbukwe kwamba Mpango wa Dharura 9

ulipowasilishwa bungeni tarehe 13 Agosti 2011 serikali ilieleza kuwa imepanga kuongeza MW 572 ifikapo mwezi Disemba 2011. Kati ya hizo, MW 150 ilikuwa zizalishwe kupitia makubaliano baina ya Shirika la Hifadhi ya Jamii (NSSF) na TANESCO; ilitarajiwa kuzalishwe MW 50 Septemba, MW 50 Oktoba na MW 50 Novemba 2011. Kimsingi, kauli iliyotolewa bungeni kuwa mitambo ilikuwa imepatikana haikuwa ya kweli. Hivyo, ahadi ya kupata umeme huo ilikuwa hewa. Mpaka sasa hakuna hata MW moja ambayo imezalishwa kwa ushirikiano kati ya NSSF na TANESCO. Ujumbe ulipotumwa Marekani kwenda kuona mitambo iliyokuwa inaelezwa kwamba ipo haikukuta mitambo yoyote, walikuta kampuni ambayo haikuwa na uwezo kama ilivyokuwa kwa Richmond Development LLC; timu hiyo ya wataalamu ilibidi kwenda Ufaransa nako ikakosa mitambo ya dharura. Hivyo, fedha nyingi za umma zimetumika kufuatilia ahadi hewa na umeme mpaka sasa haujapatikana na taifa limerejea kwenye utegemezi wa mitambo ya kukodi ya gharama kubwa ya umeme kwa sababu ya udhaifu na uzembe wa kiutendaji. Hivyo, si kweli kwamba mpango wa dharura wa umeme umetekelezwa kwa mafanikio ya asilimia 64.5 kama inavyodaiwa na Serikali kwa kupunguza lengo lilopitishwa bungeni, bali mpaka sasa umetekelezwa kwa asilimia 47.6 tu; katika muktadha huo, serikali inabidi ieleze kwa ukweli ni kwa vipi mgawo wa umeme utaepukwa kwa kuzingatia pia barua ya Mwenyekiti wa Bodi ya TANESCO kwa Rais yenye kueleza uwepo wa tishio la mgawo wa umeme. 10

Mheshimiwa Spika, kwa upande mwingine upungufu wa umeme unaojirudia rudia matokeo ya serikali kushindwa kutekeleza kwa wakati mpango wa kuweka mitambo ya MW 100 Ubungo (Dar es salaam) na MW 60 Nyakato (Mwanza) ambayo iliwekwa kwenye mpango wa umeme wa mwaka 2009 ambao ulicheleweshwa na hatimaye wakati wa Bajeti ya mwaka fedha 2010/2011 Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati na Madini wote waliahidi kukamilisha uwekaji wa mitambo hiyo mapema mwaka 2011. Hata hivyo pamoja na miradi hiyo kuingizwa kwenye mpango wa dharura tarehe 13 Agosti 2011 hakukuwa na usimamizi thabiti wa kufanya ikamilike kwa wakati. Kuzinduliwa kwa mtambo wa MW 100 Ubungo katika mwaka wa fedha 2012/2013 ni hatua ndogo kwa kuzingatia kwamba, ilipaswa mwaka wa fedha 2011/2012 pekee taifa liongeze jumla ya MW 360 toka kwenye mitambo ya kununua na si ya kukodi ili kuendana na malengo ya mpango wa taifa wa miaka mitano. Kambi Rasmi ya Upinzani inaitaka serikali ieleze sababu za kuchelewa kutekelezwa kwa miradi hiyo na hatua za uwajibikaji zilizochukuliwa kutokana na udhaifu huo.

Kashfa ya Ununuzi wa mafuta ya kufua umeme

Mheshimiwa Spika,
Kambi Rasmi ya Upinzani tulitahadharisha kwamba mpango wa dharura wa umeme na ununuzi wa mafuta 11

kwa ajili ya kufua umeme isitumike kama mwanya wa ufisadi na kuzalisha "Richmond nyigine". Inaelekea kansa hii ndani ya Serikali inayoongozwa na CCM ya kuachia dharura ziendelee kwa manufaa ya wachache imesambaa kwa kiwango cha kuwa vigumu kutibika isipokuwa kwa mabadiliko ya mfumo mzima wa utawala. Katika siku za karibuni kumekuwapo na malalamiko kutoka kwa wazabuni ambao wamekosa zabuni ya kuiuzia TANESCO mafuta ya kuendeshea mitambo ya kufua umeme ya IPTL kutokana na uamuzi wa Katibu Mkuu wa Wizara ya Nishati na Madini, Eliakim Maswi, wa kuipatia zabuni kampuni ya PUMA Energy (Tz) Ltd. (zamani ikiitwa BP (Tz) Ltd.) ambayo inamilikiwa na Serikali kwa asilimia 50. Licha ya malalamiko ya wazabuni hao, Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni inafahamu kwamba kuna kampeni kubwa imefanywa na inaendelea kufanywa ndani na nje ya Bunge hili tukufu ili uamuzi huu wa Katibu Mkuu Maswi ubatilishwe kwa maslahi ya makampuni hayo na wapambe wake wa ndani na nje ya Bunge lako tukufu. Aidha, wanaoendesha kampeni hiyo wanashinikiza Katibu Mkuu Maswi ajiuzulu kwa kile kinachoitwa kitendo chake cha kukiuka Sheria ya Manunuzi ya Umma.
Mheshimiwa Spika, kwa mujibu wa nyaraka ambazo Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni inazo, tarehe 10 Juni, 2011 aliyekuwa Mkurugenzi Mkuu wa TANESCO William Mhando alimwandikia Mtendaji Mkuu wa Wakala wa Ufilisi, Vizazi na Vifo (RITA) – iliyokuwa 12

inasimamia ufilisi wa IPTL – kumtaka aendeshe mitambo ya IPTL ili kufua MW 100 za umeme ili kuweza kuondoa mgawo wa umeme uliokuwa unaendelea sehemu mbalimbali nchini. Nyaraka hizo zinaonyesha kwamba mara baada ya kupata barua hiyo, tarehe 24 Juni 2011, Mtendaji Mkuu wa RITA alimwandikia barua Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Udhibiti wa Manunuzi ya Umma (PPRA) akimwomba mwongozo na ushauri juu ya utaratibu wa manunuzi ya mafuta ya kuendeshea mitambo ya IPTL kwa dharura.

Mkurugenzi Mkuu wa PPRA alitoa mwongozo kwa RITA kwa barua yake ya tarehe 28 June, 2011 ambapo aliielekeza RITA itumie mamlaka yake chini ya kanuni ya 42 ya
Kanuni za Manunuzi ya Umma zinazohusu Bidhaa, Kazi na Huduma zisizokuwa na Ushauri Elekezi na Mauzo ya Mali za Umma kwa Tenda, Gazeti la Serikali Na. 97 la mwaka 2005 (Public Procurement (Goods, Works, Non-Consultant Services and Disposal of Public Assets by Tender) Regulations, Government Notice No. 97 of 2005). Kanuni hiyo inamruhusu Afisa Masuhuli kuamua namna ya kufanya manunuzi kwa dharura bila kujali mipaka ya mamlaka yake endapo kwa kufanya hivyo kutahakikisha uchumi na ufanisi wa manunuzi hayo na endapo ataona ni kwa manufaa ya umma kwamba bidhaa au kazi zenye thamani inayozidi mamlaka yake zinunuliwe kama suala la dharura. 13

Mheshimiwa Spika, baada ya kupata mwongozo huo wa PPRA, Mtendaji Mkuu wa RITA alimwandikia Katibu Mkuu Maswi barua ya tarehe 18 Julai, 2011 kumweleza kwamba katika makampuni matano yaliyoonyesha nia ya kuiuzia IPTL tani 500 za mafuta kwa siku zilizokuwa zinahitajika kuendeshea mitambo yake kwa mwezi Julai, 2011, kampuni za OilCom na Shell hazikuwa na akiba ya mafuta wakati ambapo kampuni ya Mogas ilikuwa na lita laki tatu tu. Kwa upande mwingine, kampuni ya Oryx ilikuwa na tani 6,000 lakini ilikuwa inauza mafuta hayo kwa dola za Marekani 1,069.30 au shilingi 1,668,456.02 kwa tani. Aidha, kampuni ya BP (sasa Puma Energy) ilikuwa na tani 9,000 na ilikuwa tayari kuuza mafuta hayo kwa dola za Marekani 901.02 au shilingi 1,405,864.77 kwa tani. Kwa kuzingatia maelezo hayo, Katibu Mkuu Maswi alitoa ridhaa kwa RITA kununua mafuta ya kuendeshea mitambo ya IPTL kutoka kwa kampuni ya BP kwa bei iliyotajwa hapo juu.

Mheshimiwa Spika, licha ya ukweli kwamba mafuta ya BP yalikuwa na bei ndogo ikilinganishwa na bei ya Oryx, tarehe 27 Septemba, 2011 Mkurugenzi Mtendaji wa TANESCO alisaini mkataba wa kununua mafuta kutoka Oryx kwa bei ya dola za Marekani 926.98 au shilingi 1,501,707.60 kwa tani. Aidha, wiki moja kabla ya hapo, yaani tarehe 21 Septemba, Mkurugenzi Mtendaji huyo alikwishasaini mkataba mwingine na kampuni ya Camel Oil kwa bei ya dola za Marekani 905.24 au shilingi 1,466,488.80 kwa tani. Kama 14

inavyoonekana, mikataba yote miwili ilikuwa na gharama kubwa zaidi kwa tani kuliko bei ya BP. Hata hivyo, mkataba wa BP ulikatishwa na TANESCO ikaanza kununua mafuta ya kuendeshea mitambo ya IPTL kutoka kwa makampuni ya Oryx na Camel Oil.
Mheshimiwa Spika, kitu cha ajabu ni kwamba licha ya mikataba ya makampuni ya Oryx na Camel Oil kuonyesha bei za shilingi 1,501.70. na shilingi 1,466.49 kwa lita, TANESCO ilianza kununua mafuta ya makampuni hayo kwa shilingi 1,850 kwa lita! Kwa maana hiyo, kwa mikataba ya kununua jumla ya lita 16,110,000 kwa mwezi kutoka kwenye makampuni hayo, TANESCO ilikuwa inayalipa makampuni hayo jumla ya shilingi 29,803,500,000 kwa mwezi. Kwa ulinganisho, mafuta yaliyouzwa na BP kwa mkataba na RITA yaliigharimu Serikali shilingi bilioni 13,140,000,000 kwa bei ya shilingi 1,460 kwa lita. Hii ndio kusema kwamba kama TANESCO ingeendeleza mkataba na BP badala ya kuuvunja, gharama ya mafuta ya kuendeshea mitambo ya IPTL ingekuwa shilingi 23,520,600,000 na hivyo TANESCO ingeliokolea taifa shilingi 6,282,900,000 kila mwezi!

Mheshimiwa Spika, kwa upande mwingine kumekuwa na taarifa nyingi kwenye vyombo vya habari kwamba Mkurugenzi Mtendaji Mhando hakutendewa haki aliposimamishwa kazi ili kupisha uchunguzi juu ya utendaji kazi wake. Nyingi ya taarifa hizo zimetolewa bila kuwa na faida ya kuangalia nyaraka zinazohoji 15

uadilifu na uaminifu wa Mkurugenzi Mtendaji Mhando.
Mheshimiwa Spika, Mkurugenzi Mkuu Mhando ni mkurugenzi na mwanahisa wa kampuni binafsi inayoitwa Santa Clara Supplies Co. Ltd. ya Dar es Salaam. Wakurugenzi wengine ni mke wake Eva Martin William, ambaye ni Mkurugenzi Mtendaji, na watoto wao. Kwa mujibu wa taarifa ambazo Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni inazo, mnamo tarehe 20 Desemba, 2011, Santa Clara Supplies iliingia mkataba na TANESCO ambapo Santa Clara Supplies ilikubaliwa kuwa mgavi wa vifaa vya ofisini vya TANESCO kwa gharama ya shilingi 884,550,000. Mkataba huu ulisainiwa na Mkurugenzi Mtendaji Mhando kwa niaba ya TANESCO na mkewe Eva Martin William kwa niaba ya Santa Clara Supplies. Aidha, barua ya TANESCO iliyoitaarifu Santa Clara Supplies kwamba imepatiwa zabuni hiyo iliyoandikwa tarehe 24 Novemba, 2011 ilisainiwa na Mkurugenzi Mtendaji Mhando.

Mheshimiwa Spika, Sheria ya Maadili ya Viongozi wa Umma inaelekeza kwamba "… kiongozi wa umma hatajiweka katika hali ambayo maslahi yake binafsi yatagongana na wajibu wake kama kiongozi wa umma." Aidha, "… kuhusiana na uwazi kwa wananchi, viongozi wa umma watawajibika kutekeleza wajibu wao kwa umma na kuendesha shughuli zao binafsi kwa namna ambayo itaonekana na kuthibitika kuwa ni wazi na umma na haitatosheleza kwao 16

kutekeleza wajibu wao kwa kufuata sheria tu." Vile vile, "… kuhusiana na utoaji wa maamuzi, viongozi wa umma watatekeleza wajibu wao kufuatana na sheria na kwa maslahi ya umma." Zaidi ya hayo, "… kuhusiana na maslahi binafsi, viongozi wa umma hawatakuwa na maslahi binafsi ambayo yanaweza kuathiriwa na maamuzi ya serikali wanayoshiriki katika kuyafanya." Mwisho, "… kuhusiana na maslahi ya umma, pale wanapochaguliwa au kuteuliwa, viongozi wa umma watapanga masuala yao kwa namna itakayozuia migongano ya maslahi ya wazi, iliyojificha au inayoonekana kuwepo na pale ambapo migongano hiyo inatokea kati ya maslahi binafsi na maslahi ya umma basi itatatuliwa kwa kuangalia zaidi maslahi ya umma."

Mheshimiwa Spika, kwa kuzingatia ushahidi huu wa maandishi, Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni inamtaka Mbunge yeyote wa chama chochote cha siasa chenye uwakilishi ndani ya Bunge lako tukufu, anayefuata imani yoyote ya dini aseme kama, kwa mujibu wa vifungu hivi vya Sheria ya Maadili ya Viongozi wa Umma, Mkurugenzi Mtendaji Mhando ana sifa za kuitwa kiongozi mwadilifu wa umma. Hivyo, pamoja na uchunguzi wa kawaida unaoendelea, Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni inamtaka Mkurugenzi wa Mashtaka aamuru hatua za uchunguzi wa kijinai zichukuliwe dhidi ya Mkurugenzi Mtendaji Mhando kuhusu tuhuma za ufisadi na matumizi mabaya ya madaraka. 17

Mheshimiwa Spika; hata hivyo hatua hizo dhidi ya Mkurugenzi wa TANESCO na watendaji waliohusika zisigeuzwe kuwa kafara ya kuficha uzembe na udhaifu wa Serikali kwa ujumla wake kwa kuwa taarifa za utendaji wa TANESCO kuhusu mpango wa dharura wa umeme pamoja na ununuzi wa mafuta uliokuwa ukifanyika zilikuwa zikiwasilishwa kwenye vikao vya Wizara ya Nishati na Madini na hata vikao vya baraza la mawaziri. Hivyo, ili ukweli wa kina uweze kujulikana Kambi Rasmi ya Upinzani inapendekeza kuwa bunge liazimie kuunda Kamati Teule ya Bunge kuchunguza masuala yote ya ukiukwaji wa sheria, matumizi mabaya ya madaraka na tuhuma za ufisadi katika utekelezaji wa mpango wa dharura wa umeme na ununuzi wa mafuta wa ajili ya mitambo ya umeme. Uchunguzi huo uhusishe pia mkaguzi mkuu kufanya ukaguzi wa kiuchunguzi (Forensic Audit) kwa malipo yaliyofanywa na makampuni ya BP (Sasa PUMA Energy), Oryx na Camel Oil ili kubaini iwapo kuna vigogo zaidi wa serikali waliojinufaisha kwa kisingizio cha dharura ya umeme. Izingatiwe kwamba masharti ya ibara ya 27(2) ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania inamtaka kila mtu "… kutunza vizuri mali ya Mamlaka ya Nchi na ya pamoja (na) kupiga vita aina zote za uharibifu na ubadhirifu….".

Mheshimiwa Spika; Kambi Rasmi ya Upinzani tuliitaka Serikali katika mwaka wa fedha 2011/2012 itoe taarifa kuhusu utekelezaji wa 18

mpango wa uboreshaji wa utendaji wa Shirika la Umeme (TANESCO) sanjari na kutoa ripoti ya tathmini ya utekelezaji wa mpango maalum wa kurekebisha hali ya kifedha ya shirika (2006-2010). Hata hivyo, katika mwaka husika wa fedha utendaji wa TANESCO na hali yake ya kifedha imeendelea kususua huku ukigubikwa na tuhuma za ubadhirifu na udhaifu wa kiutendaji hali ambayo imepelekea pia mkurugenzi mtendaji na maafisa wengine waandamizi kusimamishwa na kuchunguzwa. Kambi Rasmi ya Upinzani inaona kwamba hali hii ni matokeo ya udhaifu katika uteuzi na usimamizi wa serikali kwa mashirika ya umma na inataka uwajibikaji kutokana na hali hiyo kudumu kwa muda mrefu. Kambi Rasmi ya Upinzani inaitaka serikali iwaeleze watanzania ni mikataba mingapi mibovu yenye kuipa mzigo mkubwa wa kifedha TANESCO na kuongeza gharama kwa wananchi imefanyiwa mapitio katika mwaka wa fedha 2011/2012.
Mheshimiwa Spika, kwa upande mwingine, udhaifu wa kutokutekeleza mipango ya uzalishaji wa gesi na makaa ya mawe kwa wakati umesababisha utegemezi mkubwa kwenye matumizi ya mafuta katika mitambo ya kuzalisha umeme wa dharura. Takribani nusu ya umeme unaozalishwa nchini hivi sasa unazalishwa kwa kutumia dizeli, mafuta ya ndege na mafuta mazito hali ambayo imeongeza mahitaji makubwa ya uagizaji wa mafuta toka nje ya nchi. Hii imesababisha mahitaji makubwa ya fedha za kigeni kwa ajili 19

ya kuagiza mafuta na hivyo kuchangia katika kuporomoka kwa thamani ya shilingi. Aidha, ongezeko kubwa la uagizaji toka nje limeathiri urari wa biashara na hivyo kuchangia katika mfumuko wa bei. Hivyo, Watanzania hivi sasa wanabeba mzigo wa kupanda kwa bei za bidhaa na gharama za maisha kwa ujumla kutokana na ufisadi kwenye mikataba, ubadhirifu katika matumizi, uzembe katika uongozi na upungufu katika utekelezaji wa mipango mbalimbali ya serikali kwenye sekta ya nishati.
Mheshimiwa Spika, mzigo huu usingekuwa mkubwa iwapo Serikali ingetekeleza katika mwaka wa fedha 2011/2012 maoni ya Kambi Rasmi ya Upinzani ya kuhakikisha nyongeza ya fedha kwenye bajeti ya Wizara ya Nishati na Madini kwa upande wa sekta ndogo ya Gesi kwa ajili ya mitambo ya umeme na kuharakisha kuwekeza katika Bomba la Gesi pamoja na ujenzi wa mtambo wa kutengeneza Gesi (LPG extraction Plant).

Kutokana na hatimaye Serikali kuzindua ujenzi wa Bomba la gesi katika mwaka wa fedha 2012/2013 na ahadi ya Wizara ya Nishati na Madini kuwa ujenzi huo utakamilika katika kipindi cha miezi kumi na nane ijayo, Kambi Rasmi ya Upinzani inataka serikali kutoa kauli ya uhakika kwa taifa; je, katika kipindi hiki cha mpito imeweka mikakati gani ya kuhakikisha mitambo ya kufua umeme iliyopo inayotumia gesi itapata gesi inayohitajika kuliondoa taifa katika upungufu wa 20

umeme.
Mheshimiwa Spika, katika mwaka wa fedha 2011/2012 tuliitaka Serikali iache kutoa kisingizio cha ‘ufinyu wa bajeti’ katika kutekeleza maoni na mapendekezo ya kuongeza fedha za Miradi ya maendeleo ya sekta za nishati na madini na tulipendekeza vyanzo vya nyongeza vya mapato kwa ajili ya sekta tajwa ikiwemo: kupunguza misamaha ya Kodi ikiwemo kuondoa msamaha wa ushuru wa mafuta kwa Kampuni za Madini peke hatua ambayo ingeongeza mapato ya mapato ya shilingi bilioni 59; Kutoka Vyanzo vipya vya mapato tulivyovianisha; kwa upande wa sekta ya madini kwa kurekebisha kodi sekta ya madini peke yake tungeweza kukusanya shilingi bilioni 240 katika mwaka wa fedha 2011/2012. Kambi rasmi ya Upinzani inataka maelezo toka kwa Serikali ni kwa kiwango gani ushauri huo umezingatiwa.

Mheshimiwa Spika, uchambuzi wa Kambi Rasmi ya Upinzani kuhusu makadirio ya bajeti ya mwaka wa fedha 2011/2012 ulionyesha uwezo mdogo na kasi ndogo ya kufikisha umeme vijijini kwa upande wa Wakala wa Umeme Vijijini (REA). Kasi ndogo ya kusambaza umeme ilielezwa pia mijini kutokana na idadi kubwa ya maombi ya wananchi wanaotaka kufungiwa umeme huku Shirika la Umeme (TANESCO) likiwajibu kuwa halina uwezo kwa sasa mpaka lipate miradi. Kambi Rasmi ya Upinzani ilitaka ufanyike ukaguzi wa kiufanisi kuhusu utekelezaji wa miradi ya usambazaji wa umeme; hivyo, 21

serikali inapaswa kueleza iwapo ukaguzi husika ulifanyika na hatua zilizochukuliwa na serikali katika kuongeza kasi ya usambazaji wa umeme.
Mheshimiwa Spika, Kambi Rasmi ya Upinzani inaitaka Serikali ieleze katika mwaka wa fedha 2011/2012 imetekeleza kwa kiwango gani mkakati wa kupunguza gharama za manunuzi na pia kupunguza kiwango cha uagizaji wa nguzo na vifaa vingine kutoka nje ili kutumia rasilimali za ndani ili kuchangia katika kukuza uzalishaji na uchumi wetu. Izingatiwe kwamba malalamiko yameendelea kuhusu mazingira ya kupitishwa kwa zabuni za ununuzi wa nguzo, transforma na nyaya za umeme kwa kiwango kikubwa toka nje ya nchi huku viwanda vya ndani mathalani TANALEC ABB, East African Cables (hususani kampuni tanzu ya Tanzania Cables) na vingine vikididimia. Hali hii imesababisha pia kukwama kwa utekelezwaji wa miradi mbalimbali ya kusambaza umeme kutokana kwa kile kinachoelezwa kuwa ni vifaa kutokupatikana kwa wakati toka nje ya nchi.

Mheshimiwa Spika, Kambi Rasmi ya Upinzani imesikitishwa na kasi ndogo ya serikali wakati wa utekelezaji wa bajeti ya mwaka wa fedha 2011/212 kuhusu kupunguza gharama wanazotozwa wananchi za kuunganishiwa huduma ya umeme suala ambalo linapunguza kasi ya uunganishwaji wa umeme. Bado tumeendelea kupokea malalamiko toka kwa wananchi wanaotakiwa na TANESCO kulipia nguzo na gharama nyingine za kuunganishwa 22

umeme kwa viwango ambavyo ni vigumu kwa wananchi wa kawaida kumudu. Hivyo, tunaitaka Serikali ieleze hatua za ziada inazokusudia kuchukua pamoja na kutekeleza maoni yetu ya kutaka TANESCO ibadili mfumo wa ankara ili kuruhusu kuingiza kwa mteja gharama hizo kidogo kidogo katika kipindi hiki cha mpito. Aidha, Kambi Rasmi ya Upinzani inawahimiza wananchi kutumia Kanuni za Sheria ya Umeme zilizotolewa kwenye gazeti la Serikali tarehe 4 Februari 2011 (GN 63) ambazo kifungu cha nne kinaeleza namna mteja atakavyofidiwa na kampuni ya usambazaji pale ambapo mteja anajigharamia mwenyewe kuvutiwa umeme ili fursa hiyo iweze kutumika ipasavyo; hata hivyo kanuni hizo zinahitaji pia kufanyiwa marekebisho kwa kuwa zimeweka mkazo katika fidia kutolewa kutokana na malipo ya wateja wengine badala ya mapato ya Shirika kwa ujumla wake.

Gesi Asilia

Mheshimiwa Spika,
tarehe 15 Julai 2011 Kambi Rasmi ya Upinzani kuwa nchi yetu imejaliwa utajiri wa gesi asilia katikati ya lindi la umasikini wa wananchi na kwamba taifa letu lina fursa ya kuwa nchi kiongozi katika gesi Afrika na kushindana kimataifa ikiwa tutaweka mstari wa mbele upeo, umakini na uadilifu katika sekta ya nishati kuepusha laana ya rasilimali. Hata hivyo, mapitio ya utekelezaji kwa mwaka wa fedha 2011/2012 yanaonyesha bado serikali haichukui hatua thabiti kushughulikia ufisadi na udhaifu wa kiuongozi katika sekta ndogo ya gesi asili hivyo hatua za haraka zisipochukuliwa 23

katika mwaka wa fedha 2012/2013 na kuendelea rasilimali inaweza kuwa chanzo cha migogoro na kuhatarisha pia usalama wa nchi.
Mheshimiwa Spika, kwa muda mrefu sasa taifa letu limekuwa likitegemea mradi mkubwa wa Songosongo kwa shughuli za uendelezaji, uzalishaji, na usafirishaji ambao uko chini ya Kampuni ya Songas. Hata hivyo, kampuni ya Songas imeiajiri Kampuni ya PanAfrican Energy Tanzania (PAT), ambayo ni mshirika wa TPDC katika uzalishaji, usambazaji na ugavi wa gesi asili. Kambi Rasmi ya Upinzani ilieleza bungeni tarehe 15 Julai 2011 kuhusu tuhuma za ufisadi na ukiukwaji wa mikataba katika sekta ndogo ya gesi na kutaka kuundwa kwa kamati teule ya bunge kuchunguza suala hilo. Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Nishati na Madini ilifanya uchunguzi wa masuala husika na taarifa kuwasilishwa bungeni; hata hivyo mpaka sasa maamizio ya bunge kufuatia taarifa hiyo hayajatekelezwa kwa ukamilifu. Kambi Rasmi ya Upinzani inaitaka Serikali kueleza ni kwanini mpaka sasa kiasi cha dola milioni 20.1 zilizopunjwa kifisadi hazijareshwa na serikali iache kutumia kisingizio cha kuundwa kwa Timu ya Majadiliano (GNT) kuchelewesha utekelezaji wa maazimio.

Mheshimiwa Spika, mradi mkubwa wa maendeleo ambao umepangwa katika mwaka wa fedha ni ujenzi wa bomba la Gesi kutoka Mtwara mpaka Dar es salaam ambapo kwenye kasma 3162 24

umetengewa kiasi cha shilingi 93,000,000,000 huku kiwango kingine cha fedha za mradi huo kikitarajiwa kupatikana kutokana na mkopo kutoka nje. Kutokana na unyeti wa mradi huo kwa mustakabali wa nchi na maisha ya wananchi wa sasa na baadaye, Kambi Rasmi ya Upinzani inaitaka Serikali kuwasilisha bungeni na kuweka wazi kwa umma mkataba wa mradi husika ili bunge liweze kuishauri na kuisimamia serikali kuanzia katika hatua za awali kuhakikisha kwamba maslahi ya taifa yanalindwa katika hatua zote na pia wananchi wananufaika kutokana na fursa za uwekezaji huo mkubwa. Aidha, pamoja na ujenzi wa mitambo miwili ya kusafishia gesi asili Mnazi Bay na Songo Songo kama sehemu ya mradi huo; Kambi Rasmi ya Upinzani inaitaka Serikali kueleza ni miradi ipi inayoambatana na mradi huo ambayo imepangwa kuwanufaisha wananchi wa mikoa ya Lindi na Mtwara ikiwemo kuharakisha utekelezaji wa mradi wa kuzalisha umeme wa MW 300 Mtwara na MW 230 wa Somanga Fungu (Kilwa).
Mheshimiwa Spika, pamoja na ujenzi wa Bomba la Gesi, Kambi ya Rasmi ya Upinzani inasisitiza mradi wa kujenga kiwanda cha kujaza gesi kwenye mitungi (LPG) na mradi wa usambazaji wa gesi Dar es salaam pamoja na mradi wa matumizi ya gesi kwenye magari inayotekelezwa na Shirika la Petroli Nchini (TPDC) inapaswa kuongezewa rasilimali katika mwaka wa fedha 2012/2013. Kuanza kwa utekelezaji wa mradi kwa ajili ya viwanda vichache na Kaya 57 25

za eneo la Mikocheni ni hatua ndogo ukilinganisha na mahitaji; hivyo, utekelezaji kwa mwaka wa fedha 2012/2013 upanuliwe wigo ili kuhusisha pia kuwezesha taasisi zingine mathalani Chuo Kikuu cha Dar es salaam kuweza kuunganishwa katika mtandao wa matumizi ya gesi asili. Hatua hii itapunguza pia matumizi ya umeme katika maeneo yenye kuweza kutumia gesi na kubakiza umeme mwingine utakaoweza kutumika kwenye maeneo ikiwemo ya viwandani yenye upungufu wa nishati mbadala.
Mafuta

Mheshimiwa Spika,
taarifa za Hali ya Uchumi wa Taifa katika mwaka 2011 mfumuko wa bei ya nishati na mafuta umeongezeka kwa asilimia 41.0 kwa mwezi Disemba 2011 ikilinganishwa na asilimia 12.3 katika kipindi kama hicho mwaka 2010. Kambi Rasmi ya Upinzani inarejea kusisitiza kwamba (ukiondoa kupanda kwa bei ya chakula kunakotokana na kushuka kwa uzalishaji na udhaifu katika usambazaji) chanzo kikuu cha hali cha mfumuko wa bei ni ongezeko la bei ya nishati hususani mafuta, umeme na gesi, hali ambayo imeshindwa kudhibitiwa kwa mikakati makini ya haraka na kuelekea kuwa tishio kwa utulivu wa taifa kiuchumi, kijamii na kisiasa.

Mheshimiwa Spika, tarehe 15 Julai 2011 kwa niaba ya Kambi Rasmi ya Upinzani iliitahadharisha Serikali kwamba muswada wa Sheria ya Fedha uliopitishwa na bunge tarehe 22 Juni 2011 usingeweza 26

kupunguza ugumu wa maisha kwa wananchi kwa kuwa serikali haikupunguza mzigo mkubwa wa kodi badala yake iliweka kipaumbele katika kupunguza tatizo la uchakachuaji kwa kuongeza mzigo mkubwa wa kodi katika mafuta ya taa. Matokeo yake ni kwamba katika mwaka wa fedha 2011/2012 kiwango cha kodi kwenye bei ya mafuta ya petrol hakikupungua, kodi katika dizeli ilipungua kwa kiwango cha shilingi 99 huku mafuta ya taa yakiongezeka kodi kwa shilingi 358 kwa lita na kuongeza mzigo wa gharama za maisha kwa sababu ya udhaifu wa serikali na vyombo vyake katika kudhibiti uchakachuaji kwa kusimamia utawala wa sheria.
Mheshimiwa Spika, Kambi Rasmi ya Upinzani inataka Serikali ieleze ni hatua zipi ambazo Serikali imechukua dhidi ya athari za kupanda kwa bei ya mafuta ya taa kwa wananchi wa kipato cha chini na pia kwa hali ya mazingira nchini kutokana na ongezeko la matumizi ya kuni na mkaa. Aidha, ikiwa mkakati huu umeweza kudhibiti uchakachuaji Serikali inatoa maelezo gani kutokana na kuwepo kwa malalamiko ya kuendelea kwa aina nyingine za uchakachuaji, na ni kwa nini taifa liendelee kuingia gharama za vinasaba vinavyowekwa na EWURA wakati inaelezwa kwamba uchakachuaji umeweza kudhibitiwa baada ya kupandisha bei ya mafuta ya taa?

Aidha, kama sehemu ya mchakato wa kupunguza gharama za mafuta kufuatia mabadiliko ya kodi, tozo na mfumo wa uingizaji wa mafuta serikali ieleze imefikia hatua gani katika mwaka wa fedha 27

2011/2012 kufanya mapitio ya mkataba baina ya EWURA na kampuni ya Global Fluids International (T) Ltd kuhusu ufanisi na gharama za kuweka vinasaba na kuleta vifaa maalum vya kupima ubora (XRF).
Mheshimiwa Spika, ukiondoa kupanda kwa bei ya mafuta katika soko la dunia na ukubwa wa kodi zinazotozwa na serikali bei ya mafuta inakuwa juu kutokana na mfumo mzima wa uagizaji, usafirishaji, uingizaji, uhifadhi na usambazaji. Mfumo uliopo unanufaisha makampuni makubwa mengi yakiwa ya kigeni na wafanyabiashara wachache wa ndani pamoja na baadhi ya viongozi wa serikali wasiokuwa waadilifu kwa kulinyonya taifa na kuongeza gharama za maisha kwa Watanzania walio wengi.

Mheshimiwa Spika, hali hii ndiyo iliyokwamisha kwa miaka mingi kuanza kwa mfumo wa uagizaji na uingizaji wa mafuta ya pamoja (Bulk Procurement System) ili kupunguza gharama; hata hivyo hata baada ya kuanza kwa utaratibu husika katika mwaka wa fedha 2011/2012 tija ya kutosha ya mfumo huo haijapatikana kutokana na udhaifu wa kimfumo. Kambi Rasmi ya Upinzani inaitaka Serikali kueleza sababu za kutokurejesha hifadhi ya taifa ya kimkakati ya taifa ya mafuta (National Strategic Oil Reserve) pamoja na kutokukamilisha mchakato wote wa kufufua Kampuni ya Taifa ya Mafuta (COPEC) kinyume na ahadi ya Wizara ya Nishati na Madini ya mwaka 2011. Aidha, ni kwa nini serikali haikununua hisa za kampuni ya BP kwa kiwango cha kuwa na umiliki wa asilimia 100 28

(100%) ili kuongeza miundombinu ya uhifadhi na usambazaji wa mafuta kwa uchumi na usalama wa nchi. Kwa upande mwingine, Wizara ya Nishati na Madini ieleze hatua mahususi ilizochukua katika mwaka wa fedha 2011/2012 za kulinda maslahi ya nchi katika kampuni ya TIPER ambayo serikali ina hisa 50% katika hatua za uingizaji na uhifadhi wa mafuta.
Mheshimiwa Spika, Ili kuongeza tija na ufanisi wa TPDC, Kambi Rasmi ya Upinzani inaitaka Serikali itoe maelezo kuhusu hatua zilizochukuliwa kwenye mwaka wa fedha 2011/2012 za kulifanyia marekebisho shirika hilo ili kuwa na mamlaka itakayohusika na kutoa vibali kwenye leseni na kusimamia uchimbaji wa mafuta na gesi na kampuni itakayoshiriki katika biashara ya mafuta na gesi.

Madini

Mheshimiwa Spika,
kwa mujibu wa Ripoti ya Hali ya Uchumi wa Taifa katika mwaka 2011 thamani ya mauzo ya madini nje ilikuwa dola za kimarekani 1,965.23 milioni ikilinganisha na dola za kimarekani 1,536.93 milioni mwaka 2010, sawa na ongezeko la asilimia 27.9. Hii ilitokana na kupanda kwa bei ya dhahabu katika soko la dunia. Hata hivyo mchango kwenye pato la taifa umekuwa ni asilimia 3.3 tu miaka karibu mitatu toka kutungwa kwa sheria mpya ya madini mwaka 2010. Udhaifu wa Serikali katika kusimamia utawala wa sheria unapaswa kuondolewa kwa bunge kupitisha maazimio ya kuisimamia serikali kulinusuru taifa dhidi ya hali hii ambayo utajiri 29

wetu unaendelea kuondoka, kwa pamoja na hatua zingine, kuwezesha mwingiliano baina ya sekta ya madini na sekta nyingine za kiuchumi katika nchi.
Mheshimiwa Spika, Kambi ya Rasmi ya Upinzani inaitaka Serikali kueleza hatua iliyofikia katika kuzingatia ushauri tulioutoa wa kutaka Wizara ya Nishati na Madini ishirikiane na Wizara ya Fedha kuboresha mfumo wa utoaji wa taarifa za malipo ya kodi kwa kampuni za madini ili malipo ya kila kampuni na mchangunuo wake yafahamike kwa umma badala ya mfumo wa sasa ambapo hurundikwa pamoja katika takwimu za idara ya walipa kodi wakubwa.

Mheshimiwa Spika, Kambi Rasmi ya Upinzani inataka Serikali ieleze hatua ilizochukua kwenye mwaka wa fedha 2011/2012 katika kuongeza kiwango cha mapato ikiwemo ya kodi kutokana na uchimbaji wa madini kwa kutekeleza mikakati ya kupenya kuta za umiliki na mitaji (capital and ownership structures) zilizojengwa kwa muda mrefu na makampuni ya kimataifa kwa kutumia mianya ya udhaifu wa kisheria na ushawishi wa kifisadi uliosababisha mikataba mibovu katika sekta ya madini nchini.

Mheshimiwa Spika, wakati umefika sasa kwa Serikali kuwasilisha bungeni ripoti ya tathmini ya utekelezaji wa mapendekezo ya tume/kamati mbalimbali ambazo ziliundwa na serikali kwa nyakati 30

mbalimbali kwa kutumia fedha nyingi za walipa kodi lakini mapendekezo yake bado hayajatekelezwa kwa ukamilifu wake. Kwa miaka mingi Serikali inazo taarifa za makampuni makubwa ya madini kutumia sehemu kubwa ya uwekezaji wao kama mkopo (debt financing) na kutumia mianya hiyo ya kisheria na kimikataba kuwezesha wamiliki na wanahisa kupata faida mapema kuliko kuweka mtaji kwa kuwa riba ya mikopo huondolewa katika kukokotoa kodi.

Kambi Rasmi ya Upinzani inarudia tena kuitaka serikali iwaeleze Watanzania ni trilioni ngapi za mapato tumezikosa kati ya mwaka 1995 mpaka 2010 katika kipindi cha miaka 15 ya kuachia mianya ya upotevu wa mapato kwa kuruhusu asilimia kubwa ya mikopo kuwa mitaji. Aidha, ni hatua gani zimechukuliwa kwa waliohusika kuliingiza taifa katika mikataba mibovu iliyoruhusu makampuni hayo kujitangazia hasara kila mwaka huku yakipata faida kubwa.

Mheshimiwa Spika, katika nchi yetu tuna migodi mikubwa mbalimbali kati yake sita ilianzishwa kati ya mwaka 1998 -2009 kwa ajili ya kuzalisha dhahabu ambayo ni Golden Pride Mine (1998), Geita Gold Mine (2000), Bulyanhulu Gold Mine (2001), North Mara Gold Mine (2002), Buhemba Gold Mine (2002) na Tulawaka Gold Mine (2005), Buzwagi Gold Mine ( 2009). Buhemba Gold Mine walifunga uzalishaji mwaka 2006 31

Mheshimiwa Spika, migodi yote hii waliwasilisha upembuzi yakinifu serikalini kabla ya kuanza uzalishaji na kuonyesha kuwa watalipa kodi ya makampuni (Corporate tax) lakini mpaka sasa ni michache tu ambayo imeanza kulipa Shilingi Bilioni 32.18 kutoka Resolute Tanzania Limited na Shilingi Bilioni 145.52 kutoka Geita Gold Mine Limited tu , pamoja na makampuni haya kunufaika na kupanda kwa bei ya dhahabu kwenye soko la dunia kwa zaidi ya mara tatu kuanzia mwaka 2002, na wakati huohuo makampuni haya yakiendelea kuweka uwekezaji mkubwa kwenye miradi yao. Kutokana na umuhimu wa sekta hii nitaeleza japo kwa kifupi kuhusiana na baadhi ya migodi hiyo mmoja mmoja:

Mheshimiwa Spika, mgodi wa Bulyanhulu ambao mwanzoni ulitarajiwa kuwa na maisha ya miaka 15 na walitarajia kuzalisha ounces 400,000 za dhahabu kwa kila mwaka ila wamekuwa wakizalisha ounces 6.5 milioni za dhahabu kwa gharama ya kuzalisha ounce 1 kwa dola 130. Aidha walitegemea kuzalisha madini ya Shaba (Copper ) ounces 7.26 milioni na madini ya fedha ounces 5 milioni na kwa sasa umri wa mgodi ni miaka 25 , yaani muda umeongezeka kwa kipindi cha miaka 10 zaidi. Mgodi wa Bulyanhulu uliwekeza kiasi cha dola 550 milioni kwa mchanganuo wa kuwa dola 300 milioni kwa uwekezaji wa awali kabla ya kuanza uchimbaji na dola 250 milioni kwa shughuli za uendeshaji wa mgodi. Mgodi huu ulitegemea kuzalisha kiasi cha dola 900 milioni kutokana na uchimbaji na uuzaji wa madini ya shaba (copper) pekee na 32

mapato ya dhahabu yalikuwa yamewekewa ukomo wa dola 300 kwa ounce tuu pamoja na kuwepo kwa badiliko la bei kwa zaidi ya mara tatu yaani sasa ni dola 950 kwa ounce moja. Ilikadiriwa kuwa mrahaba wa asilimia 3 uliotegemewa kulipwa serikalini ni kiasi cha dola 58 milioni, na fedha zilizopaswa kulipwa moja kwa moja serikalini zilikadiriwa kuwa ni dola 64 milioni ( mrahaba dola 58 milioni,mrahaba wa moja kwa moja –direct dividend dola 2 milioni na kodi ya zuio ya dola 4 milioni). Mgodi wa Bulyanhulu kwa sasa umeweza kuongeza hifadhi ya dhahabu kutoka tani 13.64 milioni na kufikia kiwango cha tani 36.05 milioni mwaka 2007 kiwango ambacho ni asilimia 90 zaidi ya kiwango kilichokadiriwa wakati wa kusaini mikataba na kuanza uchimbaji. Mpaka mwaka 2007 mgodi huu ulilipa kiasi cha dola 26.54 milioni kama mrahaba kwa serikali, na hawajalipa kodi ya makampuni .
Mheshimiwa spika, kuhusu Mgodi wa Geita Gold Mine mgodi huu ulianzishwa kwa gharama inayokadiriwa kuwa dola 152 milioni kwa ajili ya uwekezaji wote ambao ulifanywa kabla ya kuanza shughuli za uchimbaji na gharama za kuendeleza uchimbaji kwenye mgodi husika. Mgodi hu ulikuwa umeweka malengo ya kifedha kwa bei ya dola 300 kwa ounce na kuwa thamani halisi (NPV) ni dola 100 milioni,Net cash flow dola 201 milioni, mrahaba dola 30 milioni,kodi ya makampuni dola 13 milioni,kipindi cha kurejesha gharama miaka 5 na gharama za uzalishaji ni dola 181 kwa ounce. Kwa mwaka 2000 mapato halisi yalikuwa dola 14 milioni na hii ilitokana na ukweli 33

kuwa kulikuwa na uzalishaji mdogo, na pia bei iliyokuwa imetarajiwa ya dola 350 kwa ounce haikupatikana ila ilikuwa dola 279.321 kwa ounce moja. Mwaka 2004 mapato halisi yalikuwa zaidi ya mara nne ya matarajio nah ii ilitokana na uzalishaji kuwa mkubwa na bei ya dhahabu kuongezeka kwani likikuwa dola 409.271 kwa ounce ikilinganishwa na ukadiriaji wa dola 350 kwa ounce uliokuwa umewekwa awali. Ila kwa ujumla ni kuwa mapato halisi ya mgodi huu kuanzia mwaka 2001 yamekuwa yakiongezeka mara dufu kutokana na kuongezeka kwa uzalishaji na bei ya dhahabu kuendelea kupanda kwenye soko la dunia. Mpaka mwaka 2007 mgodi huu ulikuwa haujalipa kodi ya makampuni pamoja na uzalishaji kuongezeka na kuwa mara mbili zaidi ya matarajio na bei ya dhahabu kuwa kubwa mara tatu zaidi ya matarajio kwenye soko la dunia na hii iliufanya mgodi huu mapato yake kuongezeka zaidi ya mara tatu na mgodi uliendelea kutangaza kuwa unapata hasara na haujaweza kurejesha uwekezaji uliofanywa.
Mheshimiwa Spika, kuhusu mkodi wa Tulawaka katika mgodi huu uwekezaji uliofanywa ulikadiriwa kuwa ni dola 34.6 milioni na gharama za uendeshaji zilitarajiwa kuwa dola 325 kwa uzalishaji wa ounce 1, thamani halisi (NPV) Dola 9.507 milioni,net cash flow dola 29 milioni, mrahaba dola 5.367 milioni na kipindi cha kurejesha gharama miaka 4(pay back period) na walitarajia kulipa kodi ya makampuni mwaka 2008 ya dola 2.8 milioni. Kwa mwaka 2004 hapakuwa na uzalishaji na hivyo hapakuwa na mapato yeyote ila 34

kwa mwaka 2004-2007 mapato halisi ya mgodi huu yamekuwa asilimia 72.5 ya zaidi ya makadirio ya awali yaliyowekwa. Mpaka mwaka 2007 mgodi huu haukuwahi kulipa kodi ya makampuni pamoja na ukweli kuwa uzalishaji ulikuwa asilimia 7 chini ya matarajio ila mapato halisi yaliongezeka kwa asilimia 72.5 zaidi ya matarajio yaliyowekwa.
Mheshimiwa Spika, kwa upande wa Mgodi wa North Mara mpaka disemba 2007 ilikadiriwa kuwa kuna ounce 3.6 milioni ukilinganisha na zilizokuwa zimetangazwa awali wakati mgodi unaanza uzalishaji kuwa ni 2.94 milioni ounce mwaka 2002 wakati wa ufunguzi rasmi wa mgodi. Mgodi huu mpaka mwaka 2007 ulikuwa umebadilisha wamiliki kwa zaidi ya wamiliki 3 tofauti tofauti na ii inafanya kuwa ngumu sana kuweza kupata taarifa halisi za mwenendo wa m,apato kutokana na kila mmiliki kuweka utaratibu wake na kuanza upya kama vile hapakuwa na kilichofanywa na mmiliki aliyemtangulia. Aidha wamiliki wa awali waliweza kuuza migodi hii na kunufaika moja kwa moja bila serikali kupata chochote kutokana na mauziano yaliyofanywa.

Mheshimiwa Spika, kwa taarifa hizi tunaweza kuelewa kuwa uzalishaji halisi wa dhahabu kwenye migodi hiyo mitano kuanzia mwaka 1999 -2007 ulikuwa 8.388 milioni ounces ukilinganisha na matarajio yaliyowekwa awali kuwa ni kuzalisha 6.882 milioni ounces ambacho ni asilimia 21.88 zaidi ya matazamio ya awali. Umri kwa 35

ajili ya uzalishaji wa migodi hii umeongezeka kwa wastani wa miaka 4 kwa kiwango cha chini na miaka 10 kwa kiwango cha juu, na hii ilitokana na kugundulika kwa machimbo mapya ya dhahabu pamoja na kuongezeka kwa teknolojia ya kisasa zaidi kwenye tasnia hii.
Mheshimiwa Spika, mapato halisi yaliyoweza kupatikana kutokana migodi hii mitano mikubwa kwa kipindi hicho cha kuanzia mwaka 1999-2007 ilikuwa dola 3.8 bilioni ambazo ni asilimia 64 juu zaidi ya matarajio yaliyowekwa wakati uwekezaji ukifanywa ambayo ni dola 2.3 bilioni .Pamoja na mapato hayo ni kuwa fedha iliyolipwa serikalini kama mrahaba ilikuwa dola 99.6 milioni tu kwa kipindi chote hicho. Kwa migodi yote hiyo matarajio ya bei yaliyowekwa yalikuwa kati ya dola 300-350 kwa ounce wakati uhalisia ni kuwa bei ilipanda na kufikia kiasi cha dola 950 kwa ounce 1.

Mheshimiwa wa Spika, mapitio yaliyofanywa na Mamlaka ya ukaguzi wa madini (TMAA) kuanzia mwaka 2004-2008 nchini yalionyesha kuwa mgodi wa TanzaniteOne Tanzanite Mine (TTM) umekuwa ukilipa mrahaba kwa kutumia viwango vya awali vya makadirio ambavyo viliwekwa wakati mgodi huu ukianzishwa nchini. Halikadhalika ripoti hiyo inaonyesha kuwa kampuni hii imekuwa ikitoa taarifa za zisizokuwa za kweli juu ya mauzo yaliyofanyika nchini na kwenye makampuni makubwa nje ya nchi ili kuweza kukwepa kulipa mrahaba stahiki serikalini. Tathmini hiyo ya ukaguzi 36

inaonyesha kuwa kwa kipindi hicho kiasi cha dola 42.7 milioni kiliongezeka zaidi kulingana na kiwango kilichotangazwa nchini na kampuni hiyo. Hii maana yake ni kuwa kiasi cha dola 2.1 milioni kilichopaswa kulipwa kama mrahaba serikalini hakikulipwa kama inavyotakiwa kwa mujibu wa sheria ya madini kifungu cha 93 (the Mining Act, Cap., 123) . Suala hili ni kwa mujibu wa barua iliyotumwa kwa Meneja wa kamapuni ya Tanzanite one iliyoandikwa tarehe 02.10.2009 yenye Kumb.Na DA23/168/01 iliyoandikwa na aliyekuwa Kamishina wa Madini Mhe.Dalali Kafumu akiwataka wawekezaji hao kulipa hata hivyo deni hilo halikulipwa kwa wakati. Kambi Rasmi ya Upinzani inaitaka Serikali kueleza hatua ilizochukua huu ya kampuni hiyo. Aidha, tunaitaka Serikali kutoa maelezo ya kina kuhusu kuhamishwa kwa umiliki wa kampuni hiyo kwa kuzingatia kwamba baada ya kutungwa kwa Sheria ya Madini ya mwaka 2010 Serikali iliahidi kwamba uchimbaji katika eneo hilo ungeachwa kwa wachimbaji wadogo wadogo.

Kambi ya Upinzani , inaitaka serikali kuweka hadharani ripoti na taarifa zote zilizowahi kutolewa kuhusiana na uwekezaji katika uchimbaji wa madini nchini kuanzia mwaka 1995 hadi 2010 na kama serikali imefaidika na nini kutokana na uwekezaji huo.

Pili , tunahitaji mikataba yote iwekwe hadharani kwani kutokana na taarifa hizi ni hakika kuwa mikataba yetu ni mibovu sana na tunalipotezea taifa mapato mengi na hivyo kuendelea kudidimiza uchumi wa taifa.
37

Tatu, Bunge liazimie kuwa mikataba yote mipya ya uchimbaji wa madini , mafuta na gesi lazima sasa iletwe Bungeni na kujadiliwa kwa maslahi ya watanzania , kwani kama tukiendelea na utamaduni wa kusaini mikataba husika kisirisiri taifa hili litaendelea kupoteza mapato kutokana na uzembe na ufisadi kwa wanaohusika na mikataba
Mheshimiwa Spika, kutokana na kuendelea kuporomoka kwa thamani ya shilingi ya Tanzania, Kambi Rasmi ya Upinzani inaitaka Serikali kueleza hatua iliyofikiwa katika kutekeleza mapendekezo yaliyotolewa ya kutaka Wizara ya Nishati na Madini ishirikiane kwa karibu na Wizara ya Fedha katika kuweka mikakati na usimamizi wa kuhusisha sekta ya madini katika kuimarisha fedha yetu. Wakati umefika sasa wa kuwezesha Benki Kuu kutunza sehemu ya hifadhi yetu ya fedha za kigeni katika mfumo wa madini ya dhahabu. Hivyo Wizara ya Nishati na Madini ishirikiane na Benki Kuu kuweka mfumo wa kununua dhahabu kwa wachimbaji wadogo wadogo na pia kutoza sehemu ya mrabaha wa dhahabu kwa ajili ya uhifadhi kama ilivyoshauriwa na Kambi Rasmi ya Upinzani pamoja na kamati mbalimbali za bunge. Kambi Rasmi ya Upinzani inasisitiza kwamba utaratibu huu uende sambamba na kusimamia mfumo wa kuhakikisha kwamba makampuni hayo yanatunza sehemu kubwa ya fedha za nje (walau 60%) kwenye benki za ndani ili kusaidia kudhibiti kuporomoka kwa shilingi ya Tanzania. 38

Mheshimiwa Spika, Sheria ya Madini ya mwaka 2010 imeipa majukumu muhimu STAMICO ya kuwa mwakilishi na msimamizi wa rasilimali za madini nchini kwa niaba ya serikali. Mapitio ya utekelezaji kwa mwaka wa fedha 2011/2012 yanadhihirisha kwamba majukumu haya muhimu ya kisheria hayajawekewa mazingira wezeshi yakutosha ya kimfumo, kirasilimali na kikanuni takribani miaka miwili tangu kutungwa kwa sheria husika. Kambi Rasmi ya Upinzani inaitaka Serikali kuharakisha marekebisho ya sheria ndogo (Establishment Order) iliyounda STAMICO ili kuendana na mahitaji ya sasa na kuongeza mtaji wake ikiwemo kurejesha rasilimali zilizochukuliwa ikiwemo majengo. Serikali izingatie kwamba sera mkakati katika sekta ya madini iwe ni kuhakikisha Watanzania wana umiliki katika miradi mikubwa ya madini ama kupitia hisa za makampuni hayo kuwekwa katika soko la ndani (DSE) au kwa kampuni ya umma kushikilia sehemu kubwa ya uwekezaji hasa katika madini nyeti ikiwemo urani.

Mheshimiwa Spika, wwa kuwa katika mwaka wa fedha 2011/2012 Wakala wa Jiolojia (GST) aliendelea na utekelezaji wa mradi wa kutambua maeneo ya madini, Wizara ya Nishati na Madini ieleze iwapo utekelezaji wa mradi huo ulienda sambamba na kufanya tathmini ya kina (mineral appraisal) ya madini yetu ili kupendekeza mabadiliko ya kisheria na kimikataba ambayo yatawezesha utajiri wa madini yetu kutumika kama mtaji na dhamana katika hatua ya kuhakikisha taifa letu linanufaika na rasilimali zake kama 39

ilivyopendekezwa na Kambi Rasmi ya Upinzani. Aidha, ni kiwango gani cha mapato kilichopatikana kwenye mwaka wa fedha 2011/2012 kutokana na kuiwezesha GST kutoza malipo kwa mujibu wa sheria ndogo (Establishment Order) iliyounda wakala husika. Ili kulinda maslahi ya taifa kuhusu matumizi ya ramani na ripoti za utafiti na uchunguzi huo katika mwaka wa fedha 2012/2013 ukaguzi maalum (Special Audit) ufanyike kuhusu mfumo wa utoaji leseni za utafutaji na uchimbaji wa madini nchini ili kudhibiti uporaji (grabbing) unaoendelea katika rasilimali muhimu za taifa.
Mheshimiwa Spika, tarehe 15 Julai 2011 tulitoa tahadhari juu ya maamuzi ya serikali ya kuendelea na hatua za mbele katika utafutaji na uchimbaji wa madini ya urani bila kukamilisha maandalizi ya kisera, kisheria, kikanuni na kitaasisi yanayohitajika suala ambalo linaachia mianya ya upotevu wa mapato kwa taifa kama ilivyokuwa kwenye madini mengine na pia linaweza kuhatarisha usalama. Aidha, Kambi ya Rasmi ya Upinzani ilitaka maelezo ya kina kuhusu mauzo na mabadilishano ya umiliki yaliyofanyika baina ya kampuni ya Australia (Mantra Resources) na Kampuni ya Urusi ya ARMZ Uranium Holding kampuni tanzu ya Rosato. Mauzo hayo yamehusisha kuhamishiana umiliki wa maeneo ya Tanzania Mkuju River (Mbamba Bay) na Bahi Kaskazini (Dodoma). Kambi Rasmi ya Upinzani inatambua kwamba Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) ilifanya ufuatiliaji juu ya suala hilo, hivyo Wizara ya Nishati na Madini inapaswa kueleza kiasi gani cha fedha kimefanikiwa kupatikana na 40

ni hatua zipi Serikali imechukua kwa makampuni mengine ya madini, mafuta na gesi asili yaliyofanya mauziano katika mwaka wa fedha 2011/2012.
Mheshimiwa Spika, licha ya ahadi ya serikali ya toka mwaka 2010 ya kumaliza migogoro katika sekta ya madini baina ya wachimbaji wakubwa na wachimbaji wadogo wadogo ikiwemo kudhibiti migongano kati ya wenye leseni kubwa na leseni ndogo, migogoro hiyo imeendelea katika mwaka wa fedha 2011/2012. Kambi Rasmi ya Upinzani inaitaka Serikali kuwasilisha bungeni orodha ya maeneo yote yenye migogoro ya madini nchini pamoja na ratiba ya utatuzi wa migogoro husika. Pia, pamoja na kuandaa Mkakati wa Kuwaendeleza wachimbaji wadogo ili mkakati huo usiwe maneno matupu; Serikali iwasilishe pia mpango kazi na bajeti ya utekelezaji wa mkakati husika. Aidha, Serikali ianzishe mfumo wa kisheria wa kuwezesha wananchi waliokuwa wakilimiki ardhi katika maeneo yenye madini kuweza pamoja na fidia ya mazao na maendelezo kuwa na hisa katika umiliki wa migodi husika.

Mheshimiwa Spika, kufuatia kushamiri kwa migogoro baina ya wafanyakazi na wawekezaji katika sekta ya madini, Kambi Rasmi ya Upinzani inapendekeza Wizara ya Nishati na Madini iweke mfumo wa mashauriano na Wizara nyingine ili kuharakisha utatuzi wa migogoro husika. Aidha, kumekuwepo na wimbi la malalamiko ya wafanyakazi walioachishwa katika migodi wa Bulyankulu, Kampuni ya Caspian katika mgodi wa Mwadui Shinyanga , masuala ambayo 41

yanahitaji ushirikiano wa wizara na mamlaka mbalimbali katika kuyashughulikia. Aidha, Wizara ya Nishati na Madini itoe maelezo kuhusu taarifa zilizotolewa bungeni tarehe 13 Aprili 2012 kuwa wafanyakazi ikiwemo wa migodini kupitia vyama vyao walihusishwa kutoa maoni yaliyopelekea kufutwa kwa fao la kujitoa (withdrawal benefits); suala ambalo Chama Cha Wafanyakazi wa Migodini (TAMICO) kimelikanusha. Kwa kuwa ufafanuzi uliotolewa Mamlaka ya Usimamizi na Udhibiti wa Hifadhi ya Jamii (SSRA) kwa barua yenye Kumb. Na. AE/164/334/Vol II/2 umekataliwa katika migodi mbalimbali, Wizara ya Nishati na Madini imechukua hatua gani kuepusha migogoro iliyoanza kujitokeza baina ya wafanyakazi wa migodini na serikali kufuatia kupitishwa kwa vifungu husika vya sheria vyenye kuagiza mafao kutolewa baada ya kufikisha umri wa hiyari wa kustaafu wa miaka 55 au umri wa lazima wa miaka 60.
Mheshimiwa Spika, Kambi Rasmi ya Upinzani ilihoji tarehe 15 Julai 2011 kuhusu tuhuma za Kampuni ya New Almasi (1963) Limited kuchimba almasi kwa miaka 35 Mkoani Shinyanga licha ya muda wa leseni yake Na. 224 kwisha na leseni yenyewe kufutwa katika rejesta ya leseni za madini. Taarifa zilizopo zinaonyesha kwamba mkataba kati ya New Almasi (1963) Ltd uliingiwa kinyemela kwa lengo la kuwezesha uchimbaji wa almasi kuendelea katika eneo hilo kinyume cha sheria na ili kuendeleza wizi wa rasilimali ya nchi yetu. Mamia ya wananchi waishio maeneo jirani na eneo la New Almas 42

wamekuwa wakinyanyaswa kwa miaka mingi na vyombo vya dola kama vile polisi, mahakama na vyombo vya utawala kwa madai kwamba ni wavamizi wa eneo la leseni ya New Almasi. Kambi Rasmi ya Upinzani inaitaka Serikali ieleze hatua ilizochukua kwenye mwaka wa fedha 2011/2012 kuichunguza kampuni hiyo, uhalali wa shughuli zake za uchimbaji almasi katika eneo la Luhumbo, kiasi cha almasi iliyochimbwa kwa kipindi chote tokea tarehe 1 Juni 1965 hadi tarehe 8 Mei 2000 na zilizokoenda fedha zilizotokana na mauzo ya almasi hiyo. Aidha, Serikali ifafanue utaratibu wa kisheria ambao uliiruhusu Williamson Diamond Ltd. kuendelea kuchimba almasi katika eneo la Luhumbo pamoja na utata juu ya uhalali wa leseni katika eneo hilo.
MAKADIRIO YA MATUMIZI YA WIZARA YA NISHATI NA MADINI KWA MWAKA WA FEDHA 2012/2013

Mheshimiwa Spika,
makadirio ya Matumizi na Mpango wa Bajeti ya Wizara ya Nishati na Madini kwa mwaka wa fedha 2012/2013, ni shilingi bilioni 641,269,000 ikilinganishwa na Shilingi 538, 514,071,000 zilizotengwa wa Wizara mwaka 2011/2012 baada ya kufanyika kwa uhamisho wa fedha. Bajeti hiyo imeongezeka kwa Shilingi 102,755,658,000 sawa na ongezeko la asilimia 19, hata hivyo ongezeko hili ni dogo ukilinganisha na mahitaji yaliyotajwa na Mpango wa Taifa wa miaka mitano. 43

Mheshimiwa Spika, makadirio ya mapato kwa upande wa makisio ya makusanyo ya maduhuli kwa mwaka 2012/2013 ni Shilingi 193,007,543,000. Kati ya makusanyo hayo, jumla ya Shilingi 173,702,263,000 zitakusanywa na Idara ya Madini, Shilingi 19, 217,277,000 zitakusanywa na Idara ya Nishati na Petroli, na Shilingi 88,003,000 zitakusanywa na Idara ya Utawala na Usimamizi wa Rasilimali Watu. Kambi Rasmi ya Upinzani inataka Wizara ya Nishati na Madini ichukue hatua zaidi za kuongeza mapato kwa kifungu cha 2001 cha Idara ya Madini Kasma 140101 ya Ada za Madini na Kasma 140353 ya Mrabaha kwa pamoja; maeneo hayo yakiongezewa usimamizi kwa mujibu wa matakwa ya Sheria ya Madini ya mwaka 2010 na kanuni zake yana uwezo wa kulipatia taifa kiasi kisichopungua bilioni 200 katika mwaka wa fedha 2012/2013. Aidha, Wizara ya Nishati na Madini itoe maelezo iwapo matarajio ya makusanyo katika Sekta ya Nishati na Petroli kifungu cha 3001 hususani kasma 140274 yanajumuisha marejesho ya mapato ya mauzo ya gesi asili yaliyopunjwa kati ya mwaka 2004 mpaka 2010. Kambi Rasmi ya Upinzani inaitaka Serikali izingatie kuwa mapato katika shughuli za TPDC za utafiti wa mafuta pamoja na mauzo ya gesi asili yanaweza kabisa kuongezeka ziada ya makadirio ya makusanyo ya bilioni 19 tu iwapo udhibiti katika gharama na ukaguzi wa mikataba utaongezeka katika mwaka wa fedha 2012/2013. Pia ili kuongeza mapato kwa serikali na TPDC Kambi Rasmi ya Upinzani inataka mrabaha wa asilimia 12 kwenye 44

gesi uanze kutozwa kwa mujibu wa sheria na isitishe mara moja utaratibu wa baadhi kuachiwa kutokulipa malipo husika kwa mujibu wa wa sheria. Mapitio ya kitabu cha mapato yameonyesha kwamba wakati kwenye kifungu cha 2001 cha madini kuna mrabaha hakuna kasma hiyo kwenye kifungu 3001 kinachohusika na gesi na mafuta.
Mheshimiwa Spika; Matumizi ya Kawaida yanaombewa Jumla ya Shilingi 110,078, 868,000 kati ya fedha hizo shilingi 17, 292, 347,000 ni kwa ajili ya mishahara (P. E) ya Wizara na Mashirika yaliyo chini yake na Shilingi 92,786, 521, 000 ni kwa ajili ya Matumizi Mengineyo (OC). Kambi Rasmi ya Upinzani inatoa rai kwa wabunge na bunge kuungana pamoja kabla ya kupitisha matumizi haya makubwa ya kawaida kwenye matumizi mengineyo pamoja na kuitaka Wizara ya Nishati na Madini kubana matumizi kwa kupunguza matumizi yasiyo ya lazima, Serikali itakiwe kutoa maelezo ya kina kuhusu matumizi ya kifungu cha 1005 cha Kitengo cha Sheria ambacho kina kasma ya 229900 ambayo kwa mwaka wa fedha 2012/2013 kimetengewa kiasi cha Shilingi 4,000,000,000 kama gharama za utetezi wa Serikali katika kesi ya IPTL ikiwemo kwa ajili ya kuilipa kampuni ya Mkono &Co. Advocates . Izingatiwe kwamba katika mwaka wa fedha 2011/2012 Serikali ilifanya uhamisho wa fedha wa kiasi cha Shilingi Bilioni 10 kwa ajili ya gharama za kuendesha kesi zilizopo mahakamani zinazoihusu Wizara. Kambi Rasmi ya Upinzani inaitaka Serikali kueleza jumla ya fedha zilizotumiwa na Wizara kati ya mwaka 45

1995 mpaka 2011 kwa ajili ya kulipa makampuni binafsi ya uwakili kwenye kesi kubwa za kitaifa na za kimataifa pamoja na kutaja orodha ya makampuni hayo. Aidha, Serikali ieleze mkakati wa kudhibiti ongezeko la gharama za kisheria ambazo ni mzigo mkubwa kwa mashirika ya umma na wananchi walipa kodi kwa kuwa yamekuwepo mazingira ya kesi kuendelezwa kwa muda mrefu na kugeuzwa kuwa vitega uchumi vya watu wachache. Mifano ya kesi zilizodumu kwa muda mrefu ni ya IPTL ambayo Serikali inawakilishwa na Mkono and Co. Advocates na ile ya Dowans ambayo Serikali imekuwa ikiwakilishwa kwa nyakati mbalimbali na Rex Attorneys.
Mheshimiwa Spika, mwaka 2011 Benki ya Standard Hong-Kong ambayo ni mdeni mkuu katika sakata la IPTL ilifungua kesi ya madai katika mahakama ya Kimataifa ya Usuluhishi (ICSID case Na. ARB/10/20) inayodai kiasi cha dola za Kimarekani milioni 225, pamoja na riba katika kuendesha kesi hiyo. Katika muendelezo wa Serikali kampuni ya uwakili ya Mkono ilipewa zabuni ya kuitetea Serikali katika shauri hilo, na kwa kujiamini iliishauri Serikali kuwa kesi hiyo kama Serikali tungeshinda pamoja na wanasheria wengine kuwa na maoni kinzani kuhusu suala hilo. Lakini kutokana na uroho na kutaka maslahi binafsi kwa Kampuni ya Mkono inaishauri Serikali isifanye usuluhishi nje ya mahakama ya ICSID wakati wadai kupitia kwa Mfilisi wa Mali na Madeni za IPTL wanakubali kusuluhishwa nje ya mahakama. 46

Mheshimiwa Spika, Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni inaliona hili kuwa ni mchezo wa kuihujumu Serikali ambao umekuwa ukifanywa na makampuni binafsi ya uwakili kuchelewesha kesi ili yeye aendelee kulipwa mabilioni ya fedha za walipakodi. Huu ni uhujumu wa kodi za wavuja jasho wa nchi hii.

Mheshimiwa Spika, katika muendelezo huo huo Kampuni ya Mkono &Advocates kwa sababu ya uzoefu wake wa kazi hiyo na ushawishi wake mkubwa kwa viongozi wa Serikali imekuwa ni kawaida kwa kampuni hiyo kuingia mikataba kuzitetea Kampuni za nje zenye kutiliwa shaka kama ilivyo Kampuni ya matangazo inayotoka bara Asia inayojiita Asia Business Channel inayodai kutengeneza matangazo ya biashara. Kampuni hiyo yenye mwelekeo wa kutaka kutapeli ilitambulishwa kwa Mtendaji Mkuu wa TMAA na Waziri wa Nishati kipindi hicho Mheshimiwa William Ngeleja kwa barua yenye Kumb. Na. AB 88/233/01 ya tarehe 8 Desemba, 2011. Lengo lilikuwa ni TMAA kuingia mkataba wa kutangaza sekta yetu ya madini nje ya nchi.

Katika biashara hiyo ya kulazimisha, kampuni hiyo iliitumia Kampuni ya Mkono &Advocates kuandika barua ya kusudio la kuishtaki TMAA kama itashindwa kuilipa kampuni ya ASIA BUSINESS CHANNEL kiasi cha paundi za Kiingereza 35,500 kwa kazi ambayo majadiliano yalikuwa hayajafikia hatua ya mwisho. Kambi ya Upinzani inajiuliza Kampuni hii kweli ni ya wazalendo au ni ya watu ambao wanasukumwa na dhamira ya kufilisi rasilimali za Watanzania? 47

Mheshimiwa Spika, Kambi Rasmi ya Upinzani inaitaka Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali ambayo ina mamlaka ya kuiwakilisha Serikali katika kesi zote zinazoihusu Serikali ieleze imechukua hatua gani kuhusu hali hii na ifungulie mashtaka Kampuni zote zenye kuonyesha uzembe na hujuma katika kuishauri serikali kwenye kesi mbalimbali za kitaifa na kimataifa zinazohusu nishati na madini.

Mheshimiwa Spika, aidha, kama Ofisi ya Mwanasheria Mkuu itashindwa kutekeleza hilo ni wazi Mshauri huyo Mkuu wa Serikali katika mambo ya sheria atakuwa na yeye ameshindwa kazi na hivyo ni bora awape nafasi watu wenye uwezo wa kuangalia na kusimamia maslahi ya umma.

Mheshimiwa Spika, Miradi ya Maendeleo imetengewa Jumla ya Shilingi 531, 190, 861,000 kati yake Shilingi 431,190, 861,000 ni fedha za ndani na Shilingi 100,000,000,000 ni fedha za nje. Kati ya hizo kifungu cha 2001 cha Madini kimetengewa katika Kasma 3152 Shilingi 240,000,000 tu tena za nje kwa ajili ya Uwazi katika Tasnia ya Uziduaji (Tanzania Extrative Industries Transparency Initiatives –TEITI) hivyo kutokana na umuhimu wa asasi hiyo katika kuweka mfumo wa uwazi katika usimamizi na uvunaji wa rasilimali za madini, mafuta na gesi asili ni muhimu kiwango cha fedha kikaongezwa na kuhakikisha kwamba Sheria ya TEITI inatungwa katika mwaka wa fedha 2012/2013. Aidha, Taarifa zote tatu za TEITI (Reconciliation Reports) ziwasilishwe na kujadiliwa bungeni. Kwa upande mwingine, bunge lisikubali kupitisha kiasi cha Shilingi 40,000,000,000 kinachoombwa 48

kwenye Kasma 3160 kwa ajili ya kulipia madeni ya Kiwira (KCPL) mpaka uhakiki ufanyike juu ya uhalali wa viwango vya madeni husika kwa kuwa mradi mzima uligubikwa na tuhuma za ufisadi na matumizi mabaya ya madaraka.
Mheshimiwa Spika, kwa upande wa Miradi ya Maendeleo ya Nishati na Petroli kifungu cha 3001, Kambi Rasmi ya Upinzani inaitaka Serikali itoe maelezo kuhusu sababu za kutekelezwa taratibu kwa mradi wa TEDAP (Kasma 3132) ambao iwapo utaharakishwa utakuwa na mchango katika kuboresha mfumo wa gridi pamoja na kuhamasisha matumizi ya nishati jadidifu kama vyanzo mbadala katika uzalishaji umeme nje ya gridi. Aidha, pamoja na nyongeza ya fedha za miradi ya maendeleo kwa ajili ya Wakala pamoja na Mfuko wa Umeme Vijijini (REA/REF) (Kasma 3113); Kambi Rasmi ya Upinzani inasisitiza umuhimu wa kuongeza kiwango cha fedha za ndani ili kufikia bilioni 150 ili kuharakisha kasi ya uzalishaji na usambazaji wa umeme vijijini. Pia, kutokana na kasi ndogo ya usambazaji wa umeme, pamoja na kuondoa kodi katika vifaa vya umeme wa jua, serikali ieleze hatua ilizochukua katika kuweka mazingira wezeshi kwa vifaa vya umeme wa dharura kuweza kupatikana kwa urahisi mathalani vifaa vya kuhifadhia umeme (invertors). Kupitia Kasma 3147 Wizara ya Nishati na Madini inaomba 47,959,861,000 kwa mwaka wa fedha 2012/2013 kwa ajili ya kununua mafuta ya kuendesha mitambo ya dharura, hivyo ni muhimu maelezo yakatolewa kuhusu matumizi ya fedha za mafuta ya 49

mitambo ya dharura kwa mwaka wa fedha 2011/2012 ili kujenga uhalali wa matumizi ya mwaka huu wa fedha.
Mheshimiwa Spika, Wizara ya Nishati na Madini inaomba shilingi 62,000,000,000 kwa ajili ya Mradi wa Kuboresha Mifumo ya Umeme Katika Jiji la Dar es salaam (Kasma 3154). Pamoja na mradi huo kuweka mkazo katika kufunga transfoma kubwa zaidi na njia kubwa za umeme za msongo wa kV 33 kwa ajili ya wateja wakubwa wa katikati ya Jiji; mradi uweke mkazo pia katika usambazaji wa umeme pamoja na kuongeza nguvu ya umeme katika maeneo ya pembezoni ya Jiji la Dar es salaam. Izingatiwe kwamba matatizo ya miundombinu ya umeme katika Jiji la Dar es salaam kutoendana na kasi ya ongezeko la mahitaji ya umeme hayapo katikati ya jiji pekee bali pia yapo maeneo ya pembezoni yenye ongezeko la wakazi na vitega uchumi mbalimbali. Baadhi ya maeneo hayo ni pamoja na Malambamawili, Kwembe, Goba Matosa, Msakuzi, King’ongo na mengineyo katika Manispaa mbalimbali za Jiji la Dar es salaam. Aidha, Wizara ieleze iwapo kiasi cha 10,000,000,000 kilichotengwa ajili ya kulipa fidia wananchi wanaoishi katika maeneo hatarishi yanayozunguka mitambo ya kuzalishia umeme ya Ubungo kitatosha kukamilisha kazi hiyo kwa mwaka wa fedha 2012/2013 ili kuepusha uwezekano wa gharama kuongezeka kutokana na riba ya kuchelewa kufanya malipo kama ilivyotokea kwa miaka iliyopita. 50

Mheshimiwa Spika, katika mwaka wa fedha 2012/2013 na kutokana na Mpango wa Dharura wa Umeme uliopitishwa bungeni tarehe 13 Agosti 2011 Serikali imepanga kuanza utekelezaji wa miradi ya MW 240 Kinyerezi ambao umetengewa shilingi 5,000,000,000 katika Kasma 3163 na MW 150 Kinyerezi ambao umetengewa shilingi bilioni 13,000,000,000 katika Kasma 3164. Hata hivyo, kwa miradi yote hiyo Serikali iko katika hatua ya majadiliano na kufunga mikataba ya mikopo na Kampuni za SUMITOMO na Jacobsen wakati ambapo michakato ya miradi hiyo ilianza toka mwaka 2009. Kambi Rasmi ya Upinzani inarejea kuitaka Serikali kutangaza matatizo ya nishati ni janga la taifa ili kuweka mfumo wa dharura wa kushughulikia kwa haraka kwa usimamizi wa uongozi mkuu wa nchi tofauti na sasa ambapo miradi hiyo inachukuliwa kuwa ni ya kawaida chini ya Wizara ya Nishati na Madini. Aidha, Kambi Rasmi ya Upinzani inataka uhakika toka kwa Serikali iwapo mitambo hiyo inayotarajiwa kutumia gesi itakamilika lini na iwapo itapata nishati husika kwa wakati na kwa uhakika kwa kuzingatia kuchelewa kuanza kwa ujenzi wa bomba la gesi. Pia, Serikali itaje miradi mingine ya nyongeza ambayo utekelezaji wake unakusudiwa kuanza katika mwaka wa fedha 2012/2013 ili kufidia pengo la mwaka wa fedha 2011/2012 na kuhakikisha kwamba kila mwaka wastani wa MW 360 za mitambo isiyokuwa ya kukodi zinaingia katika Gridi ya Taifa katika kipindi cha utekelezaji wa Mpango wa Taifa wa Miaka Mitano.

Mheshimiwa Spika, Mpango wa Taifa wa miaka mitano (2011/2012-51

2015/2016) umelenga kuongeza uzalishaji wa umeme mpaka kufikia MW 2780 kwa kuongeza MW 1788 kwa mujibu wa miradi iliyotajwa kwenye mpango kipengele A.1.3 kuhusu nishati. Lengo hili ni dogo ukilinganisha na rasilimali ambazo zipo katika taifa letu; hivyo Kambi Rasmi ya Upinzani inaitaka Serikali kueleza imefikia hatua gani katika kufanya mapitio ya mpango huo na kuongeza miradi mingine mikubwa ukiwemo wa Stiggler Gorge ambao una uwezo wa kuzalisha MW 2100 kama nilivyopendekeza bungeni tarehe 14 Juni 2011 na kuingiza pia makadirio ya ujumla ya MW zinazotokana na miradi midogo midogo itakayoanzishwa katika maeneo mbalimbali kama tulivyoshauri tarehe 15 Julai 2011.
Mheshimiwa Spika, ili kutekeleza miradi iliyosalia kwa wakati Kambi Rasmi ya Upinzani inarudia kuitaka Wizara ya Nishati na Madini kueleza mazingira wezeshi ambayo yanakusudiwa kuandaliwa ili miradi ifuatayo iweze kupata rasilimali kwa wakati na makubaliano kukamilishwa mapema: Iringa-Mchuchuma na Ngaka (Makaa ya Mawe-300), Kiwira (MW 200) , Singida (Upepo) na Morogoro/Iringa- Ruhudji (Maji- MW 358).

Mheshimiwa Spika, ni aibu kwa taifa kuendelea kutegemea vyanzo ambavyo vilianzishwa na Serikali ya Awamu ya Kwanza iliyoongozwa na Hayati Mwalimu Nyerere, na awamu zilizofuata sio tu zimeshindwa kuongeza kasi ya kuzalisha umeme bali pia 52

zimeshindwa kukarabati mitambo hiyo na hivyo kuzalisha chini ya kiwango. Taarifa ya Hali ya Uchumi ya mwaka 2010 ilionyesha kwamba vituo vya kuzalisha umeme vilikuwa vikifua umeme kwa wastani wa 53.5 tu ya uwezo wake; hivyo Kambi Rasmi ya Upinzani inaitaka pia Serikali kueleza imechukua hatua gani kwa mwaka 2011/2012 na inapanga kuchukua hatua gani za dharura kwa mwaka wa fedha 2012/2013 kuhakikisha uwezo wa vyanzo vilivyopo kuzalishaji unaongezeka sanjari na kupunguza upotevu wa umeme kutokana na ubovu wa mifumo ya usafirishaji na usambazaji.
Mheshimiwa Spika; ili kujiandaa kitaalamu kama taifa kwa mipango kabambe ya gesi wakati nchi ikisubiri Sera ya gesi, Sheria ya Gesi na Mpango Kabambe wa Gesi (Gas Master Plan) vinavyopaswa kuwasilishwa katika Mkutano wa Tisa wa Bunge. Pia Kambi Rasmi ya Upinzani inataka Wizara ya Nishati na Madini ieleze hatua iliyofikiwa katika kukamilisha mtaala wa uhandisi wa gesi na mafuta ili fani hizo ziweze kutolewa kwenye Chuo Cha Madini Dodoma. Aidha, wakati wa kuhitimisha mjadala wa mpango wa mpango wa taifa wa miaka mitano tarehe 14 Juni 2011 serikali ilikubali pendekezo la kuanzisha Chuo Kikuu cha Mtwara. Hata hivyo hicho hakijaingizwa kwenye Mpango wa Taifa wa Miaka Mitano toleo la mwezi Juni 2012 kifungu cha A.1.5. Kambi Rasmi ya Upinzani inaitaka Serikali kueleza ni hatua zipi zitaanza kuchukuliwa kwenye mwaka wa fedha 2012/2013 na Wizara ya Nishati na Madini kwa kushirikiana na mamlaka nyingine zinazohusika kuwezesha kuanzishwa kwa Chuo 53

Kikuu hicho muhimu ambacho kitatoa mchango mkubwa kwa taifa katika masuala ya mafuta na gesi na bidhaa zitokanazo na gesi na mafuta.
Mheshimiwa Spika, katika kuimarisha sekta ya gesi na sekta kuwa na manufaa kwa nchi yetu, narudia tena mapendekezo kama tulivyoyatoa katika hotuba ya Kambi Rasmi ya Upinzani kama ilivyowasilishwa na Kiongozi wa Kambi ya Upinzani katika hotuba yake Ofisi ya Waziri Mkuu nanukuu kama ifuatavyo:

"Mheshimiwa Spika, Kambi ya Upinzani inatoa mapendekezo yafuatayo katika kuimarisha na kuboresha sekta ya gesi na mafuta hapa nchini ili kuitayarisha nchi kwa utajiri huu mkubwa:

i. Wananchi wanaozunguka maeneo yanayopatikana au yanayopitia gesi asili wawe sehemu ya mipango ya maendeleo ya gesi asili na hivyo kunufaika na matumizi ya gesi badala ya kuachwa, hali inayoleta manunguniko na tishio la uendelevu wa sekta husika na haswa ikizingatiwa kuwa uwekezaji unaofanywa katika sekta hii kama wananchi hawataona kuwa na wao ni wafaidika ni rahisi sana kuweza kuhujumu miundombinu hii na kuhatarisha usalama na hata uhai wa wananchi wengine .

ii. Ujenzi wa miundombinu ya gesi uwe unazingatia mahitaji ya muda mrefu ili kupunguza gharama na kuondokana na uhaba na uharibifu wa maliasili, mfano bomba la Songosongo liliwekwa bila kuzingatia mahitaji asili ya gesi na

54  

hivyo kujikuta kuwa wanashindwa kusafirisha gesi ya kutosha kutumiwa na wahitaji wote; iii.
Tuwekeze kwenye kuwapa elimu na maarifa vijana wa Kitanzania na haswa kwenye Sekta ya gesi ili waweze kupata utaalamu wa jinsi ya kusimamia sekta hii kama ambavyo nchi majirani zetu wa Uganda na Msumbiji wamefanya kwa kuwapeleka vijana wao nje ya nchi ili kupata utaalamu juu ya uendeshaji wa sekta hii.

iv. Serikali iliahidi kwa Shirika la Fedha la Kimataifa kwamba Sheria ya usimamizi bora wa Fedha za Mafuta na Gesi (Petroleum Revenue Management act) italetwa Bungeni mnamo mwezi Novemba. Kambi ya Upinzani inasisitiza kwamba Sheria hii iletwe haraka ili kuweka wazi mapato yatokanayo na utajiri huu na namna bora ya kutumia fedha hizi ili kuzuia uchumi kuathiriwa na pia kuzuia ufisadi. Hatutaki Tanzania iwe kama nchi nyingine za Kiafrika ambazo utajiri wa Mafuta na Gesi umekuwa ni laana badala ya Neema.

v. Serikali iweke mazingira bora ya kujenga uwezo wa Watanzania kutoa huduma kwenye kila hatua ya utafutaji wa Mafuta na Gesi. Hivi sasa kuna zaidi ya wageni 1200 kwenye Meli za kutafuta Mafuta na Gesi katika Pwani ya Mtwara, Lindi na Pwani. Kwa masikitiko makubwa sana wageni hawa wanakula hata nyanya, mchicha na vitunguu kutoka nje ya Tanzania.

55 vi.
Vile vile tudhibiti makampuni ya Ulinzi kutoka nje kuwa na silaha kali kali kwa kujenga uwezo wa Jeshi letu la Majini (Navy) ili liwe na kikosi maalumu kwa ajili ya kulinda meli za kutafuta mafuta na Gesi na Makampuni haya yatozwe tozo maalumu. Ni hatari sana makampuni ya kigeni kuwa na masilaha makubwa ndani ya ramani ya nchi yetu".

Mheshimiwa Spika, Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni inaendelea kusisitiza kwamba muswada wa sheria ya fedha wa mwaka 2012 uhakikishe misamaha wa kodi ya mafuta kwa kampuni za utafutaji wa mafuta na Gesi inaondolewa. Izingatiwe kuwa uzoefu kutokana na misamaha ambayo imekuwa ikitolewa kwa makampuni ya madini unadhihirisha kwamba makampuni mengi yanatumia mwanya huo kuleta mafuta yasiyo na kodi na kuyaingiza kwenye soko la ndani la reja reja. Hivyo, misamaha hii haina maslahi kwa taifa na ni mianya mingine ya uhujumu uchumi kwa kuwa kampuni za utafutaji mafuta na gesi zinayo fursa kwa mujibu wa mikataba (PSA) kurejeshewa gharama zao mara baada ya mafuta kupatikana. Aidha, uamuzi huu uhusishe pia kampuni za madini bila kujali mikataba (MDA) kwa kuwa imethibitika kampuni hizi zote hutengeneza faida nono bila kulipa kodi inavyostahili.

Mheshimiwa Spika, ili kudhibiti hali hii ya ukwepaji kodi na kuongeza mapato ya serikali katika mwaka wa fedha 2012/2013 Kambi Rasmi ya Upinzani inarudia kuitaka Wizara ya Nishati na Madini ieleze 56

hatua mahususi ambazo itazichukua kutekeleza mapendekezo yafuatayo: kutunga Sheria ya kuhakikisha kwamba mikopo kwenye makampuni ya uwekezaji wa madini katika mahesabu ya kodi isizidi 60% ya mtaji; kutunga Sheria kuhakikisha kwamba riba ya mikopo kwenye makampuni yanayohusiana haitaondolewa kwenye mahesabu ya kodi; kufanya marekebisho ya sheria kuhakikisha kwamba kodi ya mtaji (capital gains) inatozwa katika mauziano ya makampuni yote ya madini ambayo mali zake au uwekezaji wake uko nchini hata kama mauziano hayo yamefanyika nje ya nchi kwa kuzingatia kuwa mapendekezo yaliyoingizwa kwenye muswada wa sheria ya fedha wa mwaka 2012 hayakuzingatia kwa ukamilifu msingi wa mapendekezo yaliyotolewa na Kambi Rasmi ya Upinzani mwaka 2011. HITIMISHO

Mheshimimiwa Spika;
kambi rasmi ya upinzani inapenda kuhitimisha kwa kusisitiza kwa mara nyingine kwamba kwa sehemu kubwa matatizo katika sekta za nishati na madini yamechangiwa na sababu za kibinadamu za kutowajibika ipasavyo kisera, kimaamuzi, kiusimamizi na kiutendaji kwa viongozi wa kiserikali wenye dhamana na watendaji wengine na hivyo kusababisha ugumu wa maisha kwa wananchi na kuathiri uchumi wa nchi. 57

Mheshimiwa Spika, mabadiliko ya kimfumo yanahitajika ili kuwezesha hatua za haraka za kusimamia sera sahihi, uongozi makini na taasisi thabiti katika sekta nyeti za nishati na madini sanjari na kuchukua hatua kali dhidi ya ufisadi uliofanyika katika sekta hizi, kufanya mapitio ya mikataba na kuharakisha utekelezaji wa mipango kwa ushirikiano kati ya serikali na sekta binafsi.

Mheshimiwa Spika, nimalize kwa kuwashukuru wananchi wa Ubungo kwa ushirikiano wao katika kazi nifanyazo za kuwawakilisha kwenye vyombo vya maamuzi na kuhamasisha maendeleo Jimboni. Kwa namna ya pekee nitambue mchango wa madiwani wote tunaoshirikiana katika kipindi ninachokuwa kwenye majukumu mengine ya ujenzi wa taifa. Nawashukuru viongozi wa dini washauri wangu wa kiroho na wanafamilia yetu ya Dalali kwa upendo na kuniasa kuendeleza ujasiri na uadilifu katika kusimamia ukweli, haki na ustawi wa Jamii.

Mheshimiwa Spika,
natambua kwa shukrani mchango wa viongozi wenzangu wa Chama Cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) makao makuu, Mkoa wa Kinondoni Kanda Maalum Dar e salaam, Jimbo la Ubungo na wa Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni katika wajibu wa kuwatumikia Watanzania na kuhamasisha mabadiliko katika taifa letu. Hali tete na tata ya sasa inatutaka tuwe na mshikamano zaidi mpaka kieleweke. 58

Mheshimiwa Spika;
nawashukuru baadhi ya viongozi katika mamlaka mliotambua kwamba "siasa siyo uadui" na kunipa ushirikiano kwenye serikali kuu, Wizara ya Nishati na Madini, Manispaa ya Kinondoni, katika kamati ya nishati na madini na wabunge wengine kwa ujumla katika kutekeleza majukumu ya kibunge kwa manufaa ya taifa letu na watu wote.

Mheshimiwa Spika
, baada ya kusema hayo naomba bunge lako lijadili mapitio ya utekelezaji wa bajeti ya mwaka wa fedha 2011/2012 na makadirio ya matumizi ya Wizara ya Nishati na Madini kwa mwaka wa fedha 2012/2013 kwa kuzingatia maoni tuliyoyatoa ya kuongeza bajeti ya wizara husika; kupokea mapendekezo ya kuzingatiwa katika muswada wa sheria ya fedha wa mwaka 2012 na kupitisha maazimio mahususi ya kuhakikisha sekta za nishati na madini zinachangia kikamilifu katika kuinua uchumi wa nchi na kuboresha maisha ya wananchi;

Mheshimiwa Spika; kwa niaba ya Kambi Rasmi ya Upinzani naomba kuwasilisha

John Mnyika (Mb)
Msemaji Mkuu wa Kambi Rasmi ya Upinzani
Wizara ya Nishati na Madini
27/07/2012
kwa hisani ya http://www.http//www.mnyika.blogspot.com/