Tafuta/Search This Blog

Friday, December 30, 2016

UZALENDO NI KUTEKELEZA WAJIBU WETU KWA MAMA TANZANIA - SEHEMU II

Mtafiti wa tabia za wanadamu Viktor Frankil anatujengea uwezo kujifahamu kuwa tunaweza kuyakabili mazingira kwa kutimiza wajibu wetu. Dhana ya wajibu inatokana na neno la kingereza “responsibility” ni sawa na “response – ability”. Tafsiri yake ni mwitikio wa ndani ya mtu kuonesha uwezo wake kwa kuchukua hatua ya kubadili mazingira yake ili kupata matokeo tarajali kwa ajili yake na jamii inayomzunguka. Tuendelee na sehemu ya pili...
Ukitamka wajibu na kutimiza majukumu jeshini, wanajeshi wanakuelewa vyema. Mifumo ya taasisi za kijeshi huwa imefanikiwa “kuwatengeneza” watu wanaotafuta suluhisho hata nyakati ngumu na zenye changamoto katika nchi zao. Mtazamo wa kifikra kwa kila mwanajeshi huwa ni kushinda bila kujali ukubwa wa jeshi la adui au changamoto ili mbele yake. Tukitoa mfano kwa hapa nchini, unaweza kukumbuka nyakati za majanga kama vile mafuriko na uharibifu wa madaraja, kazi hizi hupewa wanajeshi na mara wakiingia kazini, suluhisho la muda mfupi hupatikana ili magari yaendelee huku suluhisho la kurejesha daraja kama limekatika ikifanyika.
“Hakunaga” kulaumu au kulalamika jeshini dhidi ya hali ngumu au mazingira magumu. Bali kutimiza wajibu kwa kupingana dhidi ya hali isiyoridhisha kwa kuiondoa na kufanya mazingira wezeshi yanayoifanya mipaka ya nchi iwe salama au mahala wanapolinda amani panakuwa salama kuishi na kufanya shughuli za uzalishaji ili kukuza uchumi wa mtu mmoja moja anaetimiza wajibu wake na nchi nzima kwa ujumla.
Watanzania, hatuna budi kuishi kama wapiganaji ili lengo ya kuyadhibiti mazingira na kusimika aina ya maisha tunayoyataka kwa ajili yetu na vizazi vijavyo. Tafiti kutoka kwa wataalamu wa tabia za wanadamu zinaonesha kuwa, lawama na manung’uniko huondoa uwezo wa kuona fursa ya kutatua matatizo. Mtu akifanikiwa kutatua matatizo yanayomzunguka, hufanyika kuwa ni shujaa kwa familia, jamii yake hali kadhalika taifa lake. Na jinsi tatizo linavyozidi kuwa kubwa, ndivyo, thamani ya mtu anaetatua tatizo itakuwa mara suluhisho likipatikana na hali yake kimaisha au jamii ikibadilika kutokana na jitihada zake.
Ukisoma habari ya Daudi na Goliathi ambayo huzungumzwa na kuandikwa mara kwa mara kwa falsafa mbalimbali kutegemeana na mkutadha inazungumzwa. Mathalani, ikitokea hata timu ndogo ya mpira (underdog) inakabiliana na timu kubwa (giant) zinapambana, uchambuzi mwingi hufananisha kama vita ya Daudi na Goliathi.
Daudi amekua shujaa mpaka leo si tu kwa taifa lake Israel baada ya kumpiga Mfilisti Goliathi, aliekuwa shujaa wenye uzoefu wa vita. Daudi amekuwa mfano wa kuiga (role model) kwa watu mbalimbali kupitia mifumo mbalimbali ya mafunzo kufuatia hatua yake ya kuchukua hatua (taking initiative) ya kuamua kupigana na adui yake na taifa lake na kufanikiwa kuondoa fedheha kwa taifa lake . Daudi alileta suluhisho kwa jamii yake na mpaka leo kajijengea historia na kuacha alama (legacy)
Kuna nyakati inasikitisha kusikia habari au kusoma kutoka vyanzo mbalimbali vya habari hapa nchini na kukutana na habari za matatizo na huoni muandishi akija na njia mbadala au mkakati wa kutatua tatizo au hali ngumu jamii inapitia. Kitakwimu, asilimia kubwa ya vyumba vya habari vimepoteza uweledi. Tulitegemea waandishi wa habari kuja na taarifa za kuleta fikra mbadala kwa kuonesha namna kutatua matatizo yanayoizunguka jamaii mbalimbali hapa nchini, kuna baadhi vinajikita kuonesha matatizo na madhaifu ya huku na kule na kuwajaza Watanzania hofu. Kumbuka habari mbaya kama haina taarifa za mbadala za suluhisho, huleta hofu badala ya matumaini kwa wasomaji.
Kuna taarifa wiki jana ziliandikwa kupitia magazeti kadhaa kuonesha kuwa viwanda kadhaa vya maziwa na samaki vimefungwa kanda ya ziwa. Kuna maswali mengi ya kujiuliza, je, Watanzania wameacha kunywa maziwa? Soko la samaki wa Tanzania limeanguka huko ughaibuni? Kwanini kuna maziwa kutoka Kenya, Uganda, Afrika Kusini na Uholanzi yanauzika sokoni? Nini kimesababisha viwanda kufungwa? Nini kikifanyika viwanda hivyo vyaweza kurejea na kuendelea na kazi. Sijaona wanahabari wakifanya “homework” ili kuipa jamii majibu ya fursa ya kuzalisha chakula na kusindika ili kuendelea kuuza ndani na nje ya nchi kutokana na ongezeko la watu duniani.
A.R. Bernard anasema kwa kila kisababishi kuna athari yake (to every cause there is effect), kama hupendi athari au matokeo, una wajibu wa kubadili kisababishi (if you do not like the effect, change the cause)
Rais Magufuli alitoa ahadi kutoa fedha kwa wanahabari siku ya tarehe 4.Novemba kama wataanzisha kampuni. Je, kuna wanahabari wamepeleka andiko lenye kuonesha tatizo na kuja na njia-mdadala ya kuondoa tatizo hilo katika jamii? Au kuna kampuni limekuja na mpango-mkakati mbadala kuongeza uzalishaji katika sekta ya mahindi ili kuwa na uhakika wa chakula cha kutosha ili kudibiti ongezeko la bei ya unga wa sembe na dona?
Na kama andiko limekataliwa, ni mara ngapi hatua zimefanyika ili kupigia debe wazo mbadala.
Nanukuu falsafa ya sheria ya pili kani mwendo kutoka kwa Newton. “The rate of change of momentum, is directly proportional to the force applied”. Kiwango cha kubadilika kwa kani-mwendo ni uwiano sawa na nguvu iliyotumika. Tunatumia nguvu kubwa kiasi gani kuandika kutatua matatizo ya nchi hii ukiwa ni wajibu wetu sisi wazalendo wa nchi hii?
Itaendelea...
Fredrick Matuja

UZALENDO NI KUTEKELEZA WAJIBU WETU KWA MAMA TANZANIA - SEHEMU I

Kwa mara nyingine tunaendelea na mfululizo wa makala za kudadavua dhana ya uzalendo na wajibu wetu kwa nchi na yetu Tanzania, ambae kupitia maziwa tuliyonyonya na misingi aliyotujengea, leo hii tunaweza kujumuika na wanadunia wengine kupitia teknolojia ya habari na mawasiliano.
Leo, hii tuangalie dhana ya wajibu wetu kwa nchi yetu ni nini hususan, katika wakati huu wa mpito wa mageuzi ya kiuchumi na kiutawala mara baada ya kuingia madarakani mzawa wa chato na mbobezi wa kemia na hisabai Rais John Magufuli.
Viktor Frankl ni mtafiti wa wa tabia za wanadam kutafuta furaha (pursuit of happiness) na kupitia majarida kadha wa kadha ame-eleza kwa ufasaha ramani au michoro katika akili ya mwanadamu. Mtafiti huyu ameweka wazi namna akili inaweza kuendelezwa na kumfanya mtu kuwa na kitabia ya aina flani. Na tabia hiyo huwa ni mfumo wa maisha ya watu na hali kadhalika katika jamii husika.
Mathalani, jamii za Korea, Japan hata Malaysia mtu akishindwa kutimiza azma yake ya kutoa mchango kwa maendeleo ya jamii, huishia kujua. Wengi hujiua kwa kushindwa kukubaliana na uhalisia wa nje kama vile kufilisika, kuachishwa kazi ghafla hasa kama ulikuwa ni wadhifa mkubwa serikalini au kampuni za sekta binafsi. Tabia hii ilikuwa dhahiri sana nyakati za anguko la kiuchumi duniani ambalo pia liliathiri uchumi wa nchi hizo na makampuni yao kibiashara.
Kwa upande mwingine, mtafiti Frankil alikusudia kutufunulia na kutujuza matokeo ya kitabia ili kupata tija ya hali ya juu (highly effective) kutoka kwa mtu katika mazingira yoyote yale. Tija katika muktadha huu ni uwezo wa kuona na jicho la kutafuta jibu au suluhisho katika mazingira magumu au wakati tete katika jamii.
Kwa maana nyingine, “jicho la tatu” laweza kuitwa “proactivity”. Proactive kwa tafsiri rahisi ni hali ya kuwa na fikra ya kuanzisha jambo lenye kutatua tatizo linaloinzunguka jamii au nchi ya mhusika.
Dhana inayojengwa na inayotazamwa ni hali ya kumtaka mwanadamu kunawajibika na maisha yake kwa kuyakabili mazingira au changamoto za mazingira yanayomzunguka. Tukumbuke, tabia ya kila mwanadamu ni mwitikio wa maamuazi (behavior is a function of decision of an individual). Ni namga gani mtu anayakabili mazingira au hali inayomzunguka.
Tanzania inapitia katika changamoto ya kimtazamo na kifikra tokea Rais John Magufuli achukue hatamu ya kutuongoza. Rais Magufuli amekuja na mfumo wake wa kudhibiti matumizi ya serikali na kuziba mianya ya “kupiga dili” ndani ya serikali na katika sekta binafsi; ambayo ilikuwepo kupitia mambo kadha wa kadha kama wafanyakazi hewa, wanafunzi hewa ambao walipelekea malipo hewa kupigwa na wezi wachache.
Kufuatia kusudio lake la kusimika mfumo mpya, kuna namna baadhi ya shughuli za kibiashara zimeathirika kutegemea na misingi ya wenye biashara walivyokuwa wamejenga mifumo yao ya kuziendesha.
Tukichukua wajibu wetu ili kujipanga upya namna ya kuendana na mfumo mpya wa awamu ya tano, tunawajibika kuamua namna ya kufanya biashara kwa kuzingatia misingi halali ya kulipa kodi na kufuata sheria na msingi ya kufanya kibiashara ili kukidhi uhitaji wa soko au walaji.
Pengine, tupate maana ya neno wajibu. Wajibu lilitokana na neno la kingereza responsibility -- "response-ability" – nguvu ya mwitikio au uwezo na maamuzi ya kuchagua kutenda ikisukumwa na nguvu iliyo ndani ya mtu. Huo ndiyo wajibu au kuwajibika.
Hivyo basi, wajibu ni mwitikio na uwezo na kufanya maamuzi kuyatawala au kuyadhibiti mazingira, au kulia na kulalama dhidi ya hali iliyopo. Kama tunakumbuka, Rais Obama wakati ameingia madarakani mwaka 2009, Marekani na dunia ilikuwa na anguko kubwa la kiuchumi (global economic crisis). Obama na wenzie hawakulia na kumlaumu Bush na kukumbuka miaka nane ya Bill Clinton uchumi ulikuwa mzuri, walitimiza wajibu wao wa kujipanga na kujenga mfumo mpya na leo hii uchumi wa Marekani umeimarika tofauti na miaka 8 iliyopita.
Itaendelea…
Fredrick Matuja
fmatuja@hotmail.com