Tafuta/Search This Blog

Friday, December 30, 2016

UZALENDO NI KUTEKELEZA WAJIBU WETU KWA MAMA TANZANIA - SEHEMU II

Mtafiti wa tabia za wanadamu Viktor Frankil anatujengea uwezo kujifahamu kuwa tunaweza kuyakabili mazingira kwa kutimiza wajibu wetu. Dhana ya wajibu inatokana na neno la kingereza “responsibility” ni sawa na “response – ability”. Tafsiri yake ni mwitikio wa ndani ya mtu kuonesha uwezo wake kwa kuchukua hatua ya kubadili mazingira yake ili kupata matokeo tarajali kwa ajili yake na jamii inayomzunguka. Tuendelee na sehemu ya pili...
Ukitamka wajibu na kutimiza majukumu jeshini, wanajeshi wanakuelewa vyema. Mifumo ya taasisi za kijeshi huwa imefanikiwa “kuwatengeneza” watu wanaotafuta suluhisho hata nyakati ngumu na zenye changamoto katika nchi zao. Mtazamo wa kifikra kwa kila mwanajeshi huwa ni kushinda bila kujali ukubwa wa jeshi la adui au changamoto ili mbele yake. Tukitoa mfano kwa hapa nchini, unaweza kukumbuka nyakati za majanga kama vile mafuriko na uharibifu wa madaraja, kazi hizi hupewa wanajeshi na mara wakiingia kazini, suluhisho la muda mfupi hupatikana ili magari yaendelee huku suluhisho la kurejesha daraja kama limekatika ikifanyika.
“Hakunaga” kulaumu au kulalamika jeshini dhidi ya hali ngumu au mazingira magumu. Bali kutimiza wajibu kwa kupingana dhidi ya hali isiyoridhisha kwa kuiondoa na kufanya mazingira wezeshi yanayoifanya mipaka ya nchi iwe salama au mahala wanapolinda amani panakuwa salama kuishi na kufanya shughuli za uzalishaji ili kukuza uchumi wa mtu mmoja moja anaetimiza wajibu wake na nchi nzima kwa ujumla.
Watanzania, hatuna budi kuishi kama wapiganaji ili lengo ya kuyadhibiti mazingira na kusimika aina ya maisha tunayoyataka kwa ajili yetu na vizazi vijavyo. Tafiti kutoka kwa wataalamu wa tabia za wanadamu zinaonesha kuwa, lawama na manung’uniko huondoa uwezo wa kuona fursa ya kutatua matatizo. Mtu akifanikiwa kutatua matatizo yanayomzunguka, hufanyika kuwa ni shujaa kwa familia, jamii yake hali kadhalika taifa lake. Na jinsi tatizo linavyozidi kuwa kubwa, ndivyo, thamani ya mtu anaetatua tatizo itakuwa mara suluhisho likipatikana na hali yake kimaisha au jamii ikibadilika kutokana na jitihada zake.
Ukisoma habari ya Daudi na Goliathi ambayo huzungumzwa na kuandikwa mara kwa mara kwa falsafa mbalimbali kutegemeana na mkutadha inazungumzwa. Mathalani, ikitokea hata timu ndogo ya mpira (underdog) inakabiliana na timu kubwa (giant) zinapambana, uchambuzi mwingi hufananisha kama vita ya Daudi na Goliathi.
Daudi amekua shujaa mpaka leo si tu kwa taifa lake Israel baada ya kumpiga Mfilisti Goliathi, aliekuwa shujaa wenye uzoefu wa vita. Daudi amekuwa mfano wa kuiga (role model) kwa watu mbalimbali kupitia mifumo mbalimbali ya mafunzo kufuatia hatua yake ya kuchukua hatua (taking initiative) ya kuamua kupigana na adui yake na taifa lake na kufanikiwa kuondoa fedheha kwa taifa lake . Daudi alileta suluhisho kwa jamii yake na mpaka leo kajijengea historia na kuacha alama (legacy)
Kuna nyakati inasikitisha kusikia habari au kusoma kutoka vyanzo mbalimbali vya habari hapa nchini na kukutana na habari za matatizo na huoni muandishi akija na njia mbadala au mkakati wa kutatua tatizo au hali ngumu jamii inapitia. Kitakwimu, asilimia kubwa ya vyumba vya habari vimepoteza uweledi. Tulitegemea waandishi wa habari kuja na taarifa za kuleta fikra mbadala kwa kuonesha namna kutatua matatizo yanayoizunguka jamaii mbalimbali hapa nchini, kuna baadhi vinajikita kuonesha matatizo na madhaifu ya huku na kule na kuwajaza Watanzania hofu. Kumbuka habari mbaya kama haina taarifa za mbadala za suluhisho, huleta hofu badala ya matumaini kwa wasomaji.
Kuna taarifa wiki jana ziliandikwa kupitia magazeti kadhaa kuonesha kuwa viwanda kadhaa vya maziwa na samaki vimefungwa kanda ya ziwa. Kuna maswali mengi ya kujiuliza, je, Watanzania wameacha kunywa maziwa? Soko la samaki wa Tanzania limeanguka huko ughaibuni? Kwanini kuna maziwa kutoka Kenya, Uganda, Afrika Kusini na Uholanzi yanauzika sokoni? Nini kimesababisha viwanda kufungwa? Nini kikifanyika viwanda hivyo vyaweza kurejea na kuendelea na kazi. Sijaona wanahabari wakifanya “homework” ili kuipa jamii majibu ya fursa ya kuzalisha chakula na kusindika ili kuendelea kuuza ndani na nje ya nchi kutokana na ongezeko la watu duniani.
A.R. Bernard anasema kwa kila kisababishi kuna athari yake (to every cause there is effect), kama hupendi athari au matokeo, una wajibu wa kubadili kisababishi (if you do not like the effect, change the cause)
Rais Magufuli alitoa ahadi kutoa fedha kwa wanahabari siku ya tarehe 4.Novemba kama wataanzisha kampuni. Je, kuna wanahabari wamepeleka andiko lenye kuonesha tatizo na kuja na njia-mdadala ya kuondoa tatizo hilo katika jamii? Au kuna kampuni limekuja na mpango-mkakati mbadala kuongeza uzalishaji katika sekta ya mahindi ili kuwa na uhakika wa chakula cha kutosha ili kudibiti ongezeko la bei ya unga wa sembe na dona?
Na kama andiko limekataliwa, ni mara ngapi hatua zimefanyika ili kupigia debe wazo mbadala.
Nanukuu falsafa ya sheria ya pili kani mwendo kutoka kwa Newton. “The rate of change of momentum, is directly proportional to the force applied”. Kiwango cha kubadilika kwa kani-mwendo ni uwiano sawa na nguvu iliyotumika. Tunatumia nguvu kubwa kiasi gani kuandika kutatua matatizo ya nchi hii ukiwa ni wajibu wetu sisi wazalendo wa nchi hii?
Itaendelea...
Fredrick Matuja

No comments: