The beginning of every government starts with the education of
our youth.
(Mwanzo wa kila serikali unaanza na kuwapatia elimu vijana wetu)
—Pythagoras
Katika kitabu chake cha “Think Like a Champion” yaani fikiria
kama mshindi, mwandishi Donald J. Trump ambae kwa sasa ni Rais na Amri Jeshi
mkuu wa taifa tajiri na nguvu za kijeshi la Marekani, amenukuu falsafa ya
Pythagoras.
Muandishi Donald Trump, amehimiza umuhimu kwa kujifunza na
kuoanisha aina ya kujifunza kama mwanzo mpya kwenye kila zama ambayo mtu
unaingia. Katika kitabu hicho Donald Trump ameonesha jinsi Pythagoras aliekuwa
nguli wa falsafa hususani katika somo la hisabati, mara nyingi alitafsiri mambo
mengi kwa kuoanisha au kuwakilisha na tarakimu au nambari.
Donald Trump yeye kama mfanya biashara nyakati ameandika na
kupiga chapa kitabu kicho yaani mwaka 2009 ameonesha kuwa kuna muunganiko wa
moja kwa moja kati ya elimu inayompa mtu mmoja mmoja maarifa hali kadhalika
jamii nzima kupata maarifa kupitia mifumo mbalimbali ya elimu.
Mie ninaendika makala hii kwa uzoefu na ujuzi niliopata wakati
nasoma chuo cha ualimu na baadae kupata mafunzo ya taaluma nyingine, naweza
kurejea jambo ambao nimewahi kuandika huko nyuma kuwa sisi wanadamu, tuna namna
ya kujifunza shule au vyuoni (formal education), kuna namna ya tunajifunza kwa
malengo maalum ili kupata ujuzi tunaoutaka (non-formal education). Vilevile
tunaweza kujifunza kwa kupitia vitabu, majarida, mitandao ya kijamii, program
za radio, televiseni n.k na hii inaitwa (informal education). Vyovyote vile,
maarifa tunayoyapata yanatakiwa kutubadilisha namna ya kufikiri na kuzalisha
mabadiliko ya kitabia.
Trump, alijikita katika kusisitiza kila mtu anapoanza jambo
jipya, kuna umuhimu wa kujifunza au kujiongezea maarifa mapya kuhusiana na
mambo mapya anayotaka kuyafanya. Mwandishi ambae ni Rais wa awamu ya 45 kwa
sasa ya Marekani amejielezea kwa uzuri namna ambavyo amekuwa katika kujifunza
ujenzi wa nyumba na hoteli ili anapokuwa na wahandisi-wajenzi walau asiachwe
nyuma na lugha za kimsingi za kiufundi hasa katika ujenzi.
Kuna nyakati alijikita katika uendelezaji wa viwanja vya gofu,
ilimlamlazimu pia atafute kundi la wataalamu wa kucheza mchezo wa gofu na
wajenzi wa viwanja wa gofu. Lengo lake, ilikuwa ni kukaa na wataalamu kwa lengo
la kupata taarifa za msingi kutoka kwenye uzoefu wa sekta au biashara ambayo
alikusudia kuifanya.
Donald Trump aliamini na anaamini sana katika hisia mpya huwa
zinajengwa katika misingi ya mwanzo mpya na mwanzo mpya umeunganishwa na
maarifa mapya yanayopelekea namna mpya ya kufikiri na namna mpya ya kutenda ili
kupata matokeo mapya.
Haina tofauti na msemo wa kibiblia wa umuhimu wa divai mpya katika
chupa mpya ili kupata matokeo tarajiwa. Tofauti na divai mpya unaweka katika
chupa ya zamani. Inapelekea kupoteza divai na chupa hali kadhalika.
Natamani kununua au kuazima uzoefu wa falsafa ya Donald Trump
katika muktadha wa Tanzania ya Rais John Pombe Magufuli na Watanzania walio
wengi.
Kuna namna Mheshimiwa Rais ameingia darasani kama mwalimu na
anatoa mafunzo kwa chaki ubaoni. Wakati Mwl. Magufuli anafundisha kwa mujibu wa
mungozo mpya wa somo (new syllabus) kwa upande mwingine wanafunzi ambao ni
Watanzania wanakumbuka mafunzo na malezi ya Mwl. Jakaya Mrisho Kikwete ya awamu
ya 4. Na wengi wakitaka kuishi kama awamu ya 4.
Falsafa ya Mwl. Kikwete ilikuwa 1+ ( ) = 5. Wanafunzi ambao ni
Watanzania tulikuwa na jukumu la kufikiri ni namba ngapi ikijumlishwa na moja
tunapata 5. Kwa muongozo wa kujifunza haukuhitaji njia ya kuonesha jibu ambalo
ni 4 umelipataje. Na kwa muongozo wa mafunzo yale, ukiweka 4 mwalimu atakupa
vema kwa kuwa jibu ililoweka ni sahihi.
Mara hii ameingia Mwl. Magufuli ambae ana swali kama lile la
mwalimu wa awamu ya nne, isipokuwa badala ya parandesi, wakati swali lina
herufi X
1+X = 5.
Mwalimu Magufuli anataka utafute thamani ya X kwa njia za
kihisabati za jiometri.
Sote tunakubaliana kuwa thamani ya X ni 4, isipokuwa njia ya
kuifikia 4 ni tofauti na muongozo wa mafunzo ya Mwl. Kikwete.
Awamu ya 5 anatutaka ili kupata jibu, sisi Watanzania ambao ni
wanafunzi darasani, tuna wajibu wa kujua kwamba tunatakiwa kuonesha njia ya
kulifikia jibu ambalo ni 4.
Kwa lugha rahisi inatakiwa kuchukua swali 1+X = 5 na kutoa 1
kila upande
1+ (-1)+ X = 5 – 1
Jibu litakalopatikana litakuwa wazi kabisa kuwa
0 + X = 4
Hivyo basi kumbe thamani ya X = 4.
Huu ndiyo mfumo wa muongozo wa mafunzo anayotumia mwalimu wa
awamu ya 5. Kuna uwezekano kutokana na wepesi wa masomo awamu ya 4, kuna
nyakati mwalimu alihitaji tuimbe nyimbo kama sehemu ya kujifunza.
Isipokuwa muongozo wa kujifunza na kufundishia uliopo sasa
watutaka tujue namna tofauti ya kutafuta thamani ya X. Muongozo wa mwalimu
hautupi fursa ya kuimba kama namna ya kujifunza kama kule nyuma. Na hapa ndipo
tofauti inapoanza kuonekana kwani baadhi ya wanafunzi bado wanatamani uji kumbe
tupo katika zama za kula ugali na nyama ya mifupa. Tunawajibika kutumia meno
yetu kutafuna kuitoa nyama katika mifupa.
Wanafunzi darasani (yaani Watanzania wengi) bado wanataka mwl.
Magufuli afundishe kama mwl. Kikwete na kutumia njia za zamani kuja na jibu la
thamani ya X.
Nitoe rai kwa Watanzania wenzangu ambao ni wanafunzi katika
darasa la mwalimu wa awamu ya 5; chonde chonde, tuna jukumu moja kubwa la
kufanywa upya namna ya kufikiri. Namna pekee ya kufikiri na kukubaliana na
ukweli, mfumo mpya wa muongozo wa mafunzo ndivyo unavyotaka, na mwalimu tulie
nae, muongozo wa masomo na mbinu zake za kujifunzia si kuimba (nibebe
nibembeleze kama wimbo mmoja uliowahi kutamba katika nyimbo za injili).
Tukiji-position kwa kujua tupo awamu ya 5 na kuamua kujikita
katika mbinu mpya za kukokotoa ili kupata majibu; tukifanya hivyo bila shaka
lawama na manung’uniko yataisha. Na tutajikuta tunawajibika na kujituma kwa
kutumia mbinu halali na njia halali ya kufikia jibu.
Tukigoma kujifunza, tunajiweka katika hali ya kutokua kiufahamu
hususani kwenye kukabiliana na changamoto zinazotuzunguka.
Tunaweza kupata jibu la changamoto nyingi ikiwemo kutengeneza
hela kihalali bila kutumia njia za mkato pale tu tunapojua, awamu hii na muhula
huu, unahitaji mtanzamo mpya katika utatuzi wa matatizo yanayotuzunguka.
Na utatuzi unapofanyika, maana yake njia ya kufikia jibu
inatakiwa kuwa wazi ili mtu yeyote anaekagua namna mwanafunzi alivyopata jibu,
bila maswali ya ziada aone jibu lilivyopatikana.
Ili tufaulu hisabati za mwl. Magufuli hatuna budi kumpenda na
kumkubali kuwa ndiye mwalimu wetu na tunawajibika kukubaliana na mbinu zake za
kufundishia na kujifunza ili kupata matokeo tunayotarajia.
Wataalamu wa saikolojia wanaonesha kuwa, wanafunzi hufaulu vyema
pale wanapokuwa na uhusinaano mzuri na mwalimu huhusani kwa kumpenda na
kushirikiana nae hata nje ya saa za darasa kwa kwa nia njema ya kujifunza ili
kutatua mafumbo kwa lengo la kupata majibu.
Chuki kwa mwalimu hupelekea kuchukia somo vilevile, na hatimaye
kushindwa kukabili changamoto za masomo. Ufaulu wa masomo ni faida ya
mwanafunzi kupata daraja zuri au alama nzuri. Ufaulu wa kutatua changamoto
zinazotuzunguka, sisi wanafunzi (Watanzania) ni wafaidika wa kwanza.
Hii yanikumbusha siku chache zilizopita nilipata kuhudhuria
mafunzo yaliyokuwa yakifanywa na maafisa wa kijeshi. Moja ya kitu nilichopata
katika mafunzo yale, ni namna wapiganaji hao wanavyofikiri ili kupata majibu ya
utatuzi wa maswali magumu au changamoto mbele yao.
Afisa mmoja akatoa mfano, ukikutana na mto wenye mamba wakali na
unatakiwa kuvuka upande wa pili wa mto; Je utapita katikati ya maji ili mamba
wakutafune au utafanya nini. Afisa yule wa kijeshi akaweka wazi kuwa, kuna
namna ya kuishughulisha akili ili kupata suluhisho la kusonga mbele na
kuendelea na safari ili kufika kule unakotaraji.
Moja ya suluhisho lililotolewa na mpiganaji yule ni kurusha
kamba upande wa pili wa mto na kuifunga kamba nyingine kwenye kipago au mti
mubwa na kisha kuvuka kwa kutambaa kwa miguu na mikono kwenye kamba huku mamba
wakikukodolea macho unapopita juu yao.
Kwa mtu mwingine angeweza kurudi alikotoka, mwingine angeweza
kutupa lawama ooh… kuna mamba kwenye mto, na mie siwezi kuvuka. Tofauti ya
kufikiri kwenye tatizo lile lile ndilo linawafanya Wanajeshi kujiona washindi
na akili zao zimejiengwa kusonga mbele hata pale mambo yanapokuwa magumu. Hivyo
kurusha kamba upande wa pili na kisha, anavuka kwa kamba ni moja ya mbadala
katika mbinu mpya ya kutatua tatizo la mto wenye mamba.
Katika nyakati hizi, tuna wajibu wa kufikiri kwa kiwango sawia
na muongozo wa somo la awamu ya 5. Moja ya assignment (homework) aliyoitoa
mwalimu Magufuli wakati mmoja akiongea na wahariri, ni waandishi kufungua
kampuni ili kujenga viwanda au kuwa na shughuli ya uzalishaji mkubwa unaotoa
ajira kwa vijana na kuongeza thamani ya malighafi hasa za mazao ya kilimo na
mifugo. Nae Mheshimiwa Rais alitoa ahadi ya kusaidia mchakato ili kampuni hilo
lipate mkopo kutoka benki ya ukekezaji. Je kuna, mtu au waandishi wameshapeleka
andiko la mradi wa kampuni na mwalimu wetu wa darasa la awamu ya 5 akashidwa
kutoa msaada? Au ndiyo wengi wanatumia kalamu na keyboard za social media
kulalamika tu?
Kumbe tunaweza pia kungusha mti na kuulaza upande mmoja wa mto
kwenda upande mwingine na kuvuka kwa kutambaa juu ya gogo la mti na kuendelea
na safari ya maisha pasi kulalamika kwanini mwalimu anatuelekezea njia ngumu za
kupata matokeo.
Mungu ibariki Tanzania. Tuna jukumu la kumkubali mwalimu wetu
ili tufaulu mitihani katika zama za mafunzo mapya ili kupata alama nzuri na
kusonga mbele katika hatua ijayo.
Fred Matuja
fmatuja@hotmail.com
No comments:
Post a Comment