Tafuta/Search This Blog

Thursday, March 16, 2017

FC BARCELONA NA GLENN CUNNINGHAM WANATHIBITISHA KUWA TANZANIA YA VIWANDA INAWEZAKANA



Nilipenda kukimbia tokea nikiwa mvulana. Ilikuwa ni kukimbia maili moja (sawa na kilomita 1.8). Glen alikuwa mvulana na hadithi yake ni ya kweli na kusisimua yenye mkasa unaotupa funzo la kuwa ukiwa na nguvu ya dhamira na kufanyia kazi kile unachoamini hakuna lisilowezekana chini ya jua.
Kwa kifupi hii ni hadithi ya Glenn Cunningham alezaliwa August 4, 1909 huko Kansas nchini Marekani.
Akiwa shule msingi na umri wa miaka 8, siku moja Glenn aliungua moto kufuatia mlipuko mkubwa darasani ulisababishwa na galoni la mafuta ya Petroli. Nyakati hizo kulikuwa baridi kali na kila siku wanafunzi walikuwa na jukumu la kuwasha jiko kwa kutumia mafuta ya taa ili kupasha chumba cha darasa joto. Siku moja, mtu asiefahamika aliweka petroli kwenye galoni badala ya mafuta ya taa. Glenn bila kujua aliwasha moto kama kawaida na kupatwa na mlipuko uliounguza mwili mzima na miguu yake kupoteza hisia kabisa kufuatia kufa kwa mifumo ya ufahamu.
Ushauri wa madaktari ni kuwa akatwe miguu kwani asingeweza kutembea kabisa maishani mwake. Mama wa Glenn aliekuwa anaitwa Rosa alikataa ushauri huo wa kumkata mwanae miguu ulitolewa na daktari. Glenn alikaa hospitali kwenye hali ya kutojitambua (in coma situation) na baada ya siku nyingi fahamu zilirudi na taratibu hisia za ufahamu zikaweza kuwa hai tena.
Baadae Glenn alipata ruhusa ya kwenda nyumban. Akiwa nyumbani alikuwa anawekwa juani na wazazi kwenye kiti cha magurudumu (wheel chair) kama mtu mwenye ulemavu. Kuifanya hadithi hii kuwa fupi kuna siku Glenn aliweza kutembea. Alipofanikiwa kutembea japo kwa kuanguka anguka, aliamini kuna siku anaweza kukimbia. Glenn alikuwa anatafakari na kukiri kitabu cha Isaya 40:31 “Lakini wote wanaomtumainia Mwenyezi-Mungu,watapata nguvu mpya.Wataruka juu kwa mabawa kama tai; watakimbia bila kuchoka;watatembea bila kuchoka."
Miaka kadhaa baadae Glenn aliweka rekodi kadhaa za dunia katika mchezo wa riadha. Ntaziweka rekodi chache hapa chini kwa ajili ya kumbukumbu.
Alimaliza mbio za riadha za Olimpiki ya majira ya joto mwaka 1932 na 1936. Akiwa njiani kurejea kutoka kwenye Olimpiki ya nchini Ujerumani, alipigiwa kura kama mtu maarufu kabisa huko Marekani na wana riadha wenzake wa Olympiki.
Mwaka 1933 Glenn alishinda medali ya Sullivan kwa mafanikio yake katika mbio za kati.
Mwaka 1932 kwenye Olimpiki alikuwa mtu wa 4 katika mbio za mita1500
Mwaka 1936 katika Olimpiki zilizofanyika huko Berlin Ujerumani, Glenn alishinda Medali ya fedha katika riadha, umbali wa mita 1500
Mwaka 1934, Glenn aliweka rekodi ya dunia kwa kukimbia maili moja kwa muda wa 4:06.8. Rekodi hii ilichukua miaka 3 kuvunjwa.
Mwaka 1936, Glenn aliweka rekodi ya dunia yam bio za mita 800.
Kwa kifupi Glenn aliweka rekidi nyingi sana. Tukumbuke, hakutarajiwa kutembea kwa vipimo vya kidaktari kutokana na hali aliyokuwa nayo kufuatia kuunguzwa vibaya na moto. Glenn alistaafu riadha mwaka 1940 akiwa na miaka 31.

Hadithi ya Glenn imenikumbusha mechi ya fainali ya mpira wa miguu kati ya Liverpool na AC Milan ya wakali wa wakati huo kama Andrey Shevchenko, Paolo Maldini, Kaka na Hernan Crespo na wengine wengi. Mpaka dakika 45 zinaisha vijana wa Anifield walikuwa nyuma kwa bao 3-0. Kipindi cha pili, Liverpool chini ya nahodha Steve Gerald walirudisha magoli 3 na kuingia katika changamoto za mikuwaju ya penati. Kwa wapenzi wa soka mnakumbuka, Liverpool chini ya kocha Raphael Benitez, walichukua kombe la klabu bingwa Ulaya 2005 kufuatia kuwashinda AC Milan kwa mikwaju ya penati.
Usiku wa jana kuamkia leo kati ya saa 4.45 usiku na kuendelea FC Barcelona ikiwa chini ya Luis Enrique imeleta historia ya kupindua goli 4-0 za mechi ya kwanza kwa kuibamiza PSG kutoka Ufarasa kwa bao 6-1. Kufuatia ushindi huo, naomba kunukuu maneno machache kutoka kwa wanakabumbu kutoka Calanonia.
Gerard Piqué alisama haya baada ya mchezo… “Tumeona matokeo mengi yakibadlishwa katika soka, ila si kama ushindi huu” akimaanisha kupidua magoli 4-0. Na kufunga mabao 6-1 ndani ya dakika 90. Pique aliendelea kusema….”Yeyote asie-amini, anatakiwa aende na aje tena”
Mtu mwingine ni nahodha wa FC Barcelona kiungo mchezeshaji, Andrés Iniesta, ambae alisema hivi…“Tumeshuhudia kitendo cha kihistoria” Iniesta alihitimisha kwa kusema “Hatukukoma kuamini – kiuhalisia ilikuwa haiwezekani isipokuwa imetendeka” (We never stopped believing — it was virtually impossible but it happened.)
Mpira wa jana kati ya FC Barcelona na PSG una mafundisho makubwa kwetu wanadamu, hususan sisi Watanzania. Tunawajibika kuamini na kutoacha kuamini kwa jambo jema tunalolipigania haijalishi uhalisia wa matokeo ya kushindwa huko nyuma ukoje.

Kwa akili tulizo nazo na tukiamua kuweka juhudi kubwa kuleta msukumo kwenye ujenzi wa Tanzania ya Viwanda hususani lenye nia njema kwa kutengeneza bidhaa zenye uhitaji katika soko. Tunaweza  kubadili maisha yetu  kiuchumi na kuwa sehemu ya kujenga daraja la kada la uchumi wa kati Tanzania
Rasilimali zipo, fursa zipo. Cha msingi tunatakiwa kuweka msukumo na jitihada kubwa ili kupata matokeo tunayotarajia.
Mkusanyiko wa jitihada (concentrated efforts) na imani ya kufanya kile unachokusudia bila kukata tamaa, kunaweza kubadili matokeo na historia ya maisha. Ni kweli Rais Magufuli ana muda wa miezi karibu 17 kati ya miezi 60 ya utawala wa awamu yake ya kwanza. Na matokeo yataonekana kwa wale watakao amua kuwa sehemu ya mchezo kubali matokeo na si kulalamika au kuwa watazamaji.
FC Barcelona wamevuka kwenda robo fainali ndani ya dakika 90. Tumbuke, goli 3 zimefungwa kuanzia dakika ya 87 ukijumlisha na muda wa ziada (extra time).
Watanzania, tuna nafasi ya kuwa sehemu ya kujenga uchumi wa viwanda ikiwemo kulima kilimo endelevu kwa kuangalia mahitaji ya soko ndani nan je ya nchi. . Kenya wametangaza, njaa kutokana na changamoto za mabadiliko ya tabia nchi. Somalia wametangaza njaa. Djibout na Sudan hali kadhalika. Wingi wa watu hawa wanahitaji chakula. Tanzania tuna fursa ya kufanya kilimo endelevu cha umwagiliaji. Tuna fursa ya kuvuna na kusindika mazao ya chakula na mazao malighafi kwa viwanda ili kukidhi mahitaji ya soko la ndani na nje.
Barcelona waliamini na kutumia jitihada zote ili kuweka historia. Nasi tuna nafasi ya kuamini na kufanya mambo ya maana. Glenn hakutarajiwa hata kutembea. Ushauri wa daktari ilikuwa ni kukatwa miguu. Miguu ya Glenn, maishani mwake iliweka rekodi kadhaa si za kukimbia kama mimi na wewe ambao tunaweza kukimbia si kwa mashindano, bali Glenn alivishwa medali katika mashindani makubwa kama Olimpiki ndani na nje ya nchi yake.

Watanzania tunawajibika kuamua. Tunaweza kuwa-prove wrong wale wasio amini na watazamaji. Nchi za Asia ya mbali miaka ya 60 zilikuwa kama sisi katika hali ya kiuchumi. Asia waliamua kwa juhudi zote na leo baadhi ya nchi hizo wanatusaidia kiutaalamu, kutuunzia vitu na mambo chungu mzima.

Ni wakati wa kuamini na kutenda kwa kupigana mpaka mambo yatokee. Barcelona hawakuwa na muda wa kumlaumu kocha Luiz Enrique. Wachezaji walicheza mpira ili kuleta matokeo. Watanzania tunawajibika kucheza mpira wa kuwa sehemu ya maendeleo ya Viwanda. Tukiweza kukuza kundi la wazalishaji bila shaka kundi la walipa kodi litakuwa na kuongeza makusanyo ya hazina.

Kwa pamoja tunaweza kujienga Tanzania.  

Fred Matuja
fmatuja@hotmail.com  
 



No comments: