Tafuta/Search This Blog

Monday, February 14, 2011

Kwanini CCM ilazimishe muungano wa wapinzani Bungeni?

Elias Msuya

MCHAKA mchaka umeendelea katika medani ya siasa wiki hii ambapo Bunge lilizizima pale wabunge wa Chadema walipotoka tena nje ya ukumbi wa Bunge kupinga azimio la kubadilisha kanuni za Bunge ili kuvishirikisha vyama vyote vya upinzani kuingia katika kambi rasmi ya upinzani.
Kikubwa kilichokuwa kikipiganiwa ni neno “kambi rasmi ya upinzani Bungeni” na ajabu ni kwamba wabunge wa CCM wakiongozwa na Spika Anna Makinda walikuwa mstari wa mbele kutaka wapinzani wote washirikishwe kwenye kambi hiyo.
Mabadiliko hayo yalitokana na barua iliyoandikwa na Mbunge wa Wawi Hamad Rashid (CUF) na Mbunge wa Kigoma kusini David Kafulila (NCCR Mageuzi) kwa Spika wa Bunge wakitaka kanuni zibadilishwe ili kambi rasmi ya upinzani Bungeni ivishirikishwe vyama hivyo badala ya kuiachia Chadema pekee kushikilia kambi hiyo.
Hamad Rashid ndiye aliyeshiriki kuingizwa kwa neno ‘kambi rasmi kwenye kanuni za Bunge kwenye mkutano wa tisa alipokuwa kiongozi wa kambi ya upinzani, leo baada ya kukosa uongozi wa kambi hiyo, amegeuka anataka kanuni hiyo ibadilishwe.
Kwa mujibu wa kanuni hizo, chama cha upinzani chenye asilimia 12.5 ya wabunge ndiyo chenye sifa ya kuunda kambo rasmi ya upinzani Bungeni. Chadema ndiyo chama pekee chee sifa hiyo ndiyo maana kiliunda kambi hiyo.
Hadi sasa Chadema kina wabunge wa kuchaguzliwa 25 na wa viti maalum 23. Hali hiyo imeonyesha kuitikisa CCM si majimboni tu bali hata Bungeni ambako kimebaini huenda maamuzi yake mengi yakapingwa hasa kama Chadema itashikilia kamati muhimu kama vile kamati ya Hesabu za mashirika ya umma, Kamati ya hesabu za serikali za mitaa na kamati ya Hesabu za serikali kuu.
Ndiyo maana mkakati ukasukwa na CCM ukivihusisha vyama ambavyo viliachwa na Chadema yaani CUF na NCCR Mageuzi ili kisipate nguvu zaidi.

Kwa muda mrefu, uhusiano kati ya Chadema, CUF, TLP na NCCR Mageuzi siyo wa kuridhisha. Vyama hivyo vimekuwa vikihitilafiana mara kwa mara hata kushindwa kuungana licha ya juhudi mbalimbali zilizofanyika ili kuunganisha nguvu ya vyama vya upinzani.
Mambo yalizidi kuwa mabaya zaidi kwa kadiri uchaguzi mkuu wa mwaka jana ulipokaribia, ambapo mpasuko kati ya vyama hivyo ulivyopendelea kupanuka.
Vyama hivyo vilifikia hata kushindania sehemu ambazo kama vingeungana vingekishinda CCM, lakini bado vikaendelea kuvutana.
Hata baada ya uchaguzi mkuu, kumekuwa na makovu mengi kati ya vyama hivyo. kwamfano NCCR Mageuzi kimekishitaki Chadema mahakamani kwa madai ya kuchezewa rafu katika uchaguzi wa ubunge katika jimbo la Kawe ambalo limechukuliwa Halima Mdee kwa kumbwaga mwenyekiti wa NCCR Mageuzi James Mbatia.
Chama hicho pia kimekuwa kikitoa maneno ya kejeli kwa Chadema na kuona afadhali kushirikiana na CCM kuliko Chadema.
Kama hiyo haitoshi, Mbunge wa Kigoma Kusini David Kafulila ni majeruhi wa siasa ndani ya Chadema, kwani alifukuzwa kazi baada ya kutokea kutokuelewana na uongozi wa chama hicho. kwa vyovyote vile hana uhusiano mzuri na Chadema.
Kwa upande mwingine maridhiano yaliyofikiwa Zanzibar kati ya CCM na CUF yamezidi kuichanganya kambi ya upinzani. CUF imejiweka njia panda kwani huko Zanzibar siyo chama cha upinzani tena kwakuwa kimeunda serikali ile ile ya CCM. Lakini kikija bara kinapingana na serikali. Hapo ndipo Chadema kinapata utata wa kukishirikisha kwenye kambi ya upinzani.
Hali zote hizi hazitoi fursa nzuri kuwa na kambi ya pamoja ya upinzani Bungeni. Lakini kwakuwa kina Hamad Rashid na Kafulila wamedai kushirikishwa kwenye kambi hiyo, CCM nayo ndiyo imepata pa kushikia na hapo ndipo kinatafuta kukibomoa Chadema kinachoonekana kuwa na nguvu.
Hoja ya kuwa na kambi ya pamoja ya upinzani ilishadidiwa na wabunge wa CCM wakitaka kubadilishwa kwa kanuni za Bunge ili kambi ya upizani ishirikishe vyama vyote na siyo Chadema pekee. Walitumia kila aina ya msamiati kubariki mabadiliko hayo, hali iliyokataliwa katakata na Chadema na hivyo wabunge wake kuamua kutoka nje ya ukumbi wa Bunge kama ishara ya kutokukubali.


Ni kweli vyama vya upinzani vinapaswa kushirikiana, lakini Napata wasi wasi na na ushawishi huu wa CCM. Tangu lini CCM ikaunga mkono muungano wa vyama vya upinzani?
Ni CCM hiyo hiyo iliyopinga mabadiliko ya Katiba yanayoviwezesha vyama vya upianzani kuungana bila kupoteza hadhi zake. Kwa maana hiyo ili vyama hivyo viungane ni lazima vife ili kiwe chama kimoja jambo ambalo wapinzani hawalitaki.
Huo ndiyo umekuwa mkakati mkubwa wa CCM kuhakikisha kuwa vyama hivyo haviungani ili visije vikashika dola. Ndiyo maana imekuwa vigumu kwa vyama vya upianzani kuungana miaka 19 tangu mfumo wa vyama vingi urudishwe.
Baada ya kuona hivyo kila chama kimekuwa kikicheza kivyake ili kujijenga. Ndipo katika uchaguzi wa mwaka jana Chadema kimejitahidi kupata wabunge wengi na kufikia kiwango cha asilimia 12.5 ya kuweka kuunda kambi rasmi bungeni.
CCM ile ile isiyotaka muungano wa wapinzani inakuja na kuutaka muungano huo Bungeni. Huu ni unafiki, CCM kinalia machozi ya mamba, hakina jema lolote na umoja wa wapinzani. Lengo ni kuua upinzani.
Hivi leo kama Mbowe atakuwa kiongozi wa kambi ya upinzani inayovishirikisha CUF yenye ushirikiano na CCM Zanzibar, huku NCCR Mageuzi iliyoishitaki Chadema, TLP ambayo pia haina uhusiano mzuri na Chadema, hiyo itakuwa kambi gani ya upinzani? Hapo ndipo malumbano yatazuka kwa wapinzani, huku CCM wakishangilia.
Lengo la wabunge wa CCM ni kuhakikisha kuwa Chadema chenye wabunge wengi kinakosa utawala wa kamati nyeti za Bunge na hivyo kuwakosesha nguvu ya kuhoji Bungeni.
Kwakuwa vyama vya upinzani mbali na Chadema vimepewa nguvu na CCM katika kuingizwa na kwenye kambi ya upinzani, vitashindwa kufurukuta hata kwenye maamuzi.

Lengo la baadhi ya viongozi wa CCM ni kuzima hata upinzani ndani ya CCM yenyewe kwa kushika kamati nyeti. Wanataka walidhibiti Bunge ili zile kelele za ufisadi safari hii zipungue, wajisafishie njia ya uchaguzi wa mwaka 2015. Rejea mchakato wa kuwapata wenyeviti wa kamati 16 za Bunge.

Matokeo yake Bunge litarudi kuwa la chama tawala, bunge linalotetea maslahi ya wachache wanaotuhumiwa kwa ufisadi huku chama kikiwalinda.

No comments: