Hekaheka Busanda
• Helikopta ya Mbowe yaivuruga CCM
na Kulwa Karedia, Busanda
MWENENDO wa kampeni za uchaguzi mdogo katika Jimbo la Busanda, unazidi kuonyesha kila dalili za kuzidiwa kwa Chama Cha Mapinduzi (CCM), baada ya kuendelea kwa matukio ya viongozi wake waandamizi kuzomewa na kukimbiwa katika mikutano yao ya kampeni.
Sambamba na kuendelea kwa matukio hayo, kuwasili kwa Mwenyekiti wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), Freeman Mbowe jana na kuanza kampeni za lala salama dhidi ya chama chake, kumezidisha tambo na mikikimikiki ya kampeni hizo kwa chama hicho.
Mbowe ambaye aliwasili katika anga la Busanda kwa kutumia helikopta majira ya saa nane mchana, alifanya mkutano wake wa kwanza katika Kijiji cha Nyamigota ambako aliwataka wapiga kura kutomchagua mgombea wa CCM kwa sababu kufanya hivyo ni sawa na kutangaza janga la kitaifa dhidi ya Watanzania.
“Ndugu zangu wana Busanda, naomba niwaeleze kuwa kuichagua CCM ni sawa na kutangaza janga la kitaifa kwani kwa kipindi cha miaka 48 kilichokaa madarakani, kimeshindwa kupambana na umasikini, badala yake kimekuwa kikiuzalisha kila siku,” alisema Mbowe huku akishangiliwa na umati mkubwa wa wakazi wa eneo hilo.
Mbowe aliilaumu CCM kwa kumteua Makamu Mwenyekiti mstaafu wa chama hicho Tanzania Bara, John Malecela, anayefahamika zaidi kwa jina la Tingatinga kuwa, ni kumdhalilisha kwa sababu kwa umri wake na wadhifa wake hapaswi kufanya kazi ya kugawa chumvi na magodoro kwa wapiga kura ambao wamekwishaonyesha nia ya kutokichagua chama anachokitetea.
“Wabunge wa CCM siku zote wamekuwa mzigo, wameshindwa kusoma alama za nyakati, sasa masikini wangu wameamua kumtoa mzee Malecela kwa ajili ya kukiokoa chama chao… tunasema wamechelewa kwa hili.
“CHADEMA hivi sasa ina kazi moja tu ya kuhakikisha inarudisha heshima ya jimbo hili kwa vile ina uhakika wa kushinda katika uchaguzi unaotarajiwa kufanyika Jumapili ijayo.
“Nawaambia huyo Malecela waliyemleta hapa atavuna alichopanda na atabeba gunia lake la aibu… kwanini asitumie nyakati hizi kukaa nyumbani au kuwa mshauri wa chama badala ya kugeuka kuwa kinara wa rushwa?” alihoji Mbowe.
Alisema anachoamini ni kwamba, Malecela kwa uwezo alionao anastahili kuwa mshauri wa vijana wa chama hicho na kuwaachia vijana hao kazi ya kupambana na wanamapinduzi wa kweli wanaotaka kuing’oa CCM madarakani.
“Nilitegemea Malecela angekuwa kioo cha kukemea rushwa, ufisadi na matendo maovu ndani ya CCM, lakini sasa wameamua kumtupa vijijini kugawa magodoro… namheshimu sana kama mzee wetu, lakini sina budi kumwambia ukweli kuwa, wakati wa kupumzika umefika,” alisema.
Baadaye Mbowe aliruka kwa helikopta hadi Kijiji cha Lwamgasa, ambako baada ya kufika ilionekana dhahiri kubadilika kwa upepo wa kisiasa katika kijiji hicho ambacho wakazi wake wengi ni wachimbaji wadogo wadogo wa madini.
Kabla ya kuwasili helikopita hiyo, mamia ya wakazi wa eneo hilo walikuwa wamejitokeza kwa wingi kuhudhuria mkutano wa kampeni za Chama cha Wananchi (CUF), lakini baada ya kutua, mkutano huo ulishindwa kuendelea baada ya waliokuwa wamekusanyika kwa ajili ya kusikiliza sera za chama hicho kukimbilia katika mkutano wa CHADEMA.
Akiwahutubia wakazi wa eneo hilo, aliwataka kufanya mageuzi bila ya kushinikizwa na viongozi wa CCM.
Mbowe ambaye aliwasili kijijini hapo saa mbili baada ya mgombea wa CCM, Lolencia Bukwimba kumaliza kuhutubia mkutano wa kampeni, aliwasihi wananchi kutobabaishwa na vitendo vya CCM vya kupeleka nguzo za umeme kijijini hapo, kwani hiyo ni kutaka kufanya ujanja wa kuchaguliwa.
“Msibabaishwe na CCM kuwaletea nguzo za umeme hapa, huu ni uongo tu, wanataka kuwadanganya ili muwapigie kura katika uchaguzi ujao… mbona miaka yote hawakuja, leo hii ndiyo wanakuja hawa wakataeni,” alisema Mbowe.
Baadaye alikwenda katika Kijiji cha Kaseme ambako aliwataka wananchi kutobabaishwa na propaganda za CCM za kuletewa maisha bora.
Kuwasili kwa helikopita katika jimbo hili jana, kulisababisha hata baadhi ya viongozi wa CCM waliokuwa katika Hoteli ya Zacharia Lodge kuungana na wana CHADEMA kuipokea.
Kitendo hicho kilifanya viongozi hao kushangiliwa na umati mkubwa wa wananchi waliokuwa wakiimba ‘Kamanda wa Pori ametua kuondoka na mbunge’.
Aidha, kuwasili kwa helikopta hiyo inayotumiwa na Mbowe katika kampeni hizo, kulisababisha kusimama kwa shughuli nyingi za kijamii na barabara nyingi kufungwa kutokana na wingi wa watu waliokuwa wakifika kumuona mwenyekiti huyo wa CHADEMA.
Katika tukio ambalo halikutarajiwa na wengi, licha ya helikopita hiyo kutua karibu na Kituo cha Polisi Katoro na kufunga barabara, polisi hawakuchukua hatua yoyote ya kufukuza wananchi waliokuwa wakiishangilia CHADEMA baada ya Mbowe kushuka katika helikopta hiyo.
Katika hatua nyingine, hali ya mambo ndani ya CUF imeonekana kuwa mbaya baada ya uongozi wa chama hicho kuwafukuza wafanyakazi wake wawili kwa madai kuwa wanavujisha siri za chama hicho.
Tukio hilo limetokea jana ambapo iliwafukuza Haroun Mikole ambaye ni fundi mitambo na dereva Mazoe Chidide kwa maadai kuwa walikutwa wakiteta jambo na viongozi wa CHADEMA usiku wa kumkia jana.
Wakati hali ikiwa hivyo kwa vyama vya CHADEMA na CUF, kwa upande wa CCM, jana ilikuwa zamu ya kada wake kijana ambaye pia ni Waziri wa Nishati na Madini, William Ngeleja kukumbana na hasira za wapiga kura wa Busanda.
Kwa mara ya kwanza tangu alipowasili katika kampeni hizo kukiongezea nguvu chama chake, jana Ngeleja alijikuta katika wakati mgumu baada ya kukimbiwa na wachimbaji wadogo wadogo katika mkutano wa ndani wa chama hicho uliokuwa ukifanyika katika mgodi wa dhahabu wa Lwamgasa.
Hatua ya Ngeleja kukimbiwa na wachimbaji hao ilitokana na kauli yake kuwa, kama watashindwa kuichagua CCM watanyag’anywa leseni na kufutiwa usajili wa vitalu vyao.
Katika mkutano huo ambao ulifanyika katika Shule ya Msingi Mwenge, Ngeleja alisema CCM ndiyo yenye wezo wa kuchukua hatua zozote zinazostahili kuwaendeleza wachimbaji, wakiwamo wa migodi mikubwa kama vile Mererani, North Mara na Geita Gold Mine.
“Napenda kuwaambia ndugu zangu, leo nimewaita hapa kutaka kuwaambia kwamba, tuna kazi moja tu ya kuhakikisha mnachagua CCM katika uchaguzi ujao, sasa nawaambia kama hamtafanya hivyo, tutahakikisha tunawanyang’anya leseni kwani CCM ndiyo yenye serikali,” alisema Ngeleja.
Alisema wachimbaji wadogo wadogo wamekuwa na tabia ya kupinga sera za CCM eti kwa madai kuwa imekuwa ikiwakandamiza, jambo ambalo halina ukweli wowote.
Katika hali inayoonekana kuwa vitisho, Ngeleja alisema kama CCM itashindwa kwenye uchaguzi huo, wachimbaji hao watashukiwa kwa nguvu zote na Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) ili kuona kama kweli wanalipa kodi ya serikali.
“Moja ya mkakati ambao tumeandaa ni kwamba kama CCM haitashinda, TRA itakuja hapa kwa ajili ya kuhakiki kama kweli mnalipa kodi ya mapato, ikiwa ni kinyume chake mtashughulikiwa kwa mujibu wa sheria ya serikali,” alisema Ngeleja.
Kauli hiyo ilionekana kuwaudhi wachimbaji hao ambao walianza kuondoka mmoja mmoja ndani ya ukumbi na kumwacha Ngeleja na viongozi wa CCM aliokuwa ameambatana nao kwenye kikao hicho.
Baadhi ya wachimbaji hao waliiambia Tanzania Daima Jumatano kuwa, huo ni unyanyasaji mkubwa na ukiukwaji wa haki za binadamu unaofanywa na serikali.
Mmoja wa wachimbaji hao, Swedi Mussa alisema kama Waziri Ngeleja ataendelea na kauli hiyo, anaweza kusababisha mgawanyiko mkubwa ndani ya jamii inayozunguka machimbo na Watanzania ambao ndio wanayategemea kuendesha maisha yao ya kila siku.
“Tumeshangazwa na kauli ya Ngeleja na ndiyo maana tuliamua kumkimbia ndani ya ukumbi, kwa sababu inaonekana wazi kwamba sasa anataka kutufanya Watanzania ni wajinga wa kutupwa, kwanini kaja wakati wa kampeni kututisha hivi?” alihoji Mussa.
Aliongeza kuwa, hatua ya kuambiwa kwamba watanyang’anywa leseni inaonyesha wazi kwamba CCM imedhamiria kuongeza umasikini katika jamii tofauti na sera zake kwamba inaleta maisha bora kwa kila Mtanzania.
-kutoka Tanzania Daima
No comments:
Post a Comment