Tafuta/Search This Blog

Saturday, December 12, 2009

Hii nayo kali...

Hayati Tassos Papadopoulos


WEZI wamefukua kaburi la aliyekuwa rais wa Cyprus, Tassos Papadopoulos na kuiba maiti yake usiku wa kuamkia jana, siku moja kabla ya kumbukumbu ya mwaka mmoja tangu kifo chake.
Televisheni ya Cyprus, ambayo ililalazimika kukatiza vipindi vyake kwa muda, ilieleza jana kuwa wezi hao waliuiba mwili huo na kutokomea nao kusikojulikana.


Tassos Papadopoulos alifariki dunia Desemba 12, 2008 na alizikwa katika eneo lililo nje kidogo ya mji mkuu wa nchi hiyo, Nicosia. Mamlaka nchini humo zilieleza kuwa walikuta kaburi likiwa wazi na mwili wa rais huyo wa zamani ukiwa haupo.
Mmoja wa mashuhuda alieleza kuwa jeneza lililokuwa limeuhifadhi mwili huo lilikutwa likiwa wazi baada ya kufunguliwa. Polisi na wanafamilia wa rais huyo wa zamani walikuwa wamezagaa katika eneo hilo la tukio.


Msemaji wa polisi, Michalis Katsounotos alisema inaaminika kuwa mwili huo ulichukuliwa usiku wa kuamkia jana, lakini bado haijajua nia ya uhalifu huo.
"Kilichotokea ni kitendo cha kustaajabisha na kinatakiwa kulaaniwa. Ninaendelea kutafakari kuwa ni watu wenye mitizamo ya namna gani hadi wakaamua kufanya jambo kama hili... hili ni tukio linaloistua jamii nzima ya Cyprus na ulimwengu," alisema Andros Kyprianou, ambaye ni kiongozi mkuu wa chama tawala cha kikomunisti cha AKEL.


Kiongozi mkuu wa AKEL, Andros Kyprianou alieleza kushangazwa kwake na taarifa hizo ambazo zimetapakaa baada ya mwili wa kiongozi huyo kuibwa siku moja kabla ya kumbukumbu ya mwaka mmoja wa kifo chake. "Sijui ni watu wa aina gani wanaoweza kufanya uhalifu wa ajabu namna hii. Kwa mimi bado sina la kusema," alisema.


Papadopoulos alikuwa rais wa Cyprus kuanzia mwaka 2003 hadi Februari 2008, alipopoteza nafasi hiyo baada ya kushindwa katika uchaguzi mkuu na nafasi yake kuchukuliwa na Demetris Christofias. Miezi michache baadaye aligundulika kuwa na ugonjwa wa saratani ya mapafu na alifariki dunia Desemba 12, 2008 akiwa na umri wa miaka 74.

No comments: