Tafuta/Search This Blog

Wednesday, June 24, 2009

Serikali inahitaji MAOMBI!!!!!!!!!!!!!!!!!!!

MBUNGE wa Kilindi mkoani Tanga (CCM), Beatrice Shelukindo jana alielezea kwa kifupi matatizo ya serikali, akisema inakabiliwa na ugonjwa ambao uhahitaji "makanisa na misikiti kuiombea."
Kombora lake limekuja katika kipindi ambacho mawaziri na baraza lao wamekuwa wakituhumiwa kwa ubinafsi, roho mbaya na kubariki mikataba yenye harufu ya ufisadi wakati Wabunge wakizidi kuicharukia serikali tangu kusomwa kwa bajeti ya makadirio ya mapato na matumizi ya serikali kwa mwaka 2009/10.
Jana mbunge huyo wa Kilindi alisema dawa ya ugonjwa huo wa serikali iko kwa Rais Jakaya Kikwete, makamu wake, Dk Ali Shein na Waziri Mkuu Mizengo Pinda.
Shelukindo alitoa kauli hiyo jana alipokuwa akichangia hotuba ya bajeti ya ofisi ya Waziri Mkuu iliyowasilishwa bungeni na Waziri Pinda juzi.
Shelukindo alisema: “Mheshimiwa Naibu Spika, sasa serikali ina ugonjwa. Ugonjwa huu ni mkubwa na dawa yake iko kwa rais, makamu wa rais na waziri mkuu pekee.”
Shelukindo alitaja ugonjwa huo kuwa ni kukosekana kwa utekelezaji sahihi wa mambo muhimu yenye manufaa kwa taifa kwa wakati sahihi, hali ambayo alisema inafanya mambo hayo kujirudia kila wakati.
“Ugonjwa huo ambao ni hatari ni kukosa utekelezaji sahihi kwa wakati sahihi. Hatuna hilo!” alisema.
“Baya zaidi ugonjwa huu umeingia mpaka makanisani na misikitini, mambo hayatekelezwi.”
Alitoa mfano wa baadhi ya hoja za wapinzani kujirudia akieleza kuwa ni sababu ya kukosa majibu ya moja kwa moja kutokana na ugonjwa huo.
"Kwa hali hiyo wabunge hawatanyamaza badala yake wataendelea kunyoosha vidole kwa kuwa kila siku mambo yanarudi yale yale; hayapatiwi majibu; hayatekelezwi kama hoja ya Dk. Slaa ya jana (juzi).
"Spika anamwambia asubiri, atanyamaza vipi wakati hajajibiwa? Hatuwezi kunyamaza tutaendelea kunyoosha vidole mpaka utekelezaji ufanyike kwa wakati sahihi,” alisema Shelukindo.
Alitetea hoja yake kwa kutoa mfano wa daktari aliyepewa nafasi ya kwenda kusoma nje ya nchi, lakini safari yake ilifutwa na katibu mkuu mpya wa Wizara ya Afya na Ustawi wa Jamii.
“Mwaka jana Wizara ya Afya na Ustawi wa Jamii iliteua daktari kwenda India. Alishaandaliwa kila kitu na watoto wake wamesimama shule wakisubiri safari hiyo. Anaingia katibu mkuu mwingine wa wizara, anasema daktari huyo hana sifa, ina maana yeye anajua zaidi ya wataalam aliowakuta?” alihoji.
“Cha ajabu anaenda kuteua mtu aliyestaafu, analazimisha mtu akubalike. Yaani ‘no control’ kila mtu anasema, ila ‘no control no maendeleo.”
Katika hatua nyingine Shelukindo jana alitoa shutuma nzito alizozielekeza kwa mmoja wa mawaziri, akidai kiongozi huyo na wengine kadhaa wamekuwa wakijipitisha maeneo mbalimbali na kugawa rushwa ya peremende kwa lengo la kushawishi wachaguliwe katika uchaguzi ujao.
Shelukindo alisema kuwa wakati serikali na Bunge vinahimiza utawala bora, wanaosimamia suala hilo wanaendelea kubomoa.
“Inashangaza kuona wanaosimamia utawala bora ndio wanaobomoa, Waziri Mkuu anajua ninachoongea, nilishamwona. Jamani tufuate taratibu."
"Nasema hivi kuwa wapo mawaziri tena wakubwa tu hawafuati taratibu, wapo watu wanajipitisha katika ofisi za mikoa na wilaya na kugawa pesa kama peremende,” alisema Shelukindo na kuongeza:
“Ndio wapo. Utakuta waziri tena mkubwa na gari ama lina namba za W au NW anapita katika mikoa au wilaya na kufanya hivyo, akijua kuwa hata ofisa wa Takukuru wilaya wanashindwa kumchukulia hatua. Jamani tufuate utaratibu, tukumbuke hatuna hati miliki ya uwaziri wala ubunge tupo hapa kwa ridhaa ya wananchi.”
Hoja hiyo ya Shelukindo ilishangiliwa na wabunge wengi na picha za televisheni zilimwonyesha mama huyo akionyesha alama ya kidole gumba kuelekea sehemu kadhaa ambazo kulikuwa na wabunge waliokuwa wakimpongeza kwa mbali, huku wale walio karibu wakimsogelea na kumpa mkono.
Naye mbunge wa Mbozi Mashariki (CCM), Godfrey Zambi, alielekeza moto huo kwa Waziri wa Miundombinu huku akihoji ukimya wa waziri huyo na serikali katika kuchukua hatua dhidi ya Wakala wa Mizigo Bandarini (Ticts) kwa zaidi ya mwaka mmoja licha ya kampuni hiyo kutotimiza ahadi.
“Mheshimiwa naibu spika, jingine ni suala ya Ticts. Kwa nini serikali haitoi majibu? Wengine wanasema ukizungumzia Ticts eti unaichukia. Naona hili limeingizwa katika siasa sasa. Mimi sina sababu ya kuichukia Ticts," alisema.
"Ukweli ni kwamba haijafanya iliyoyaahidi, kuna mambo mengi, si sawa, tunaomba serikali ichukue hatua.
"Hivi utawala gani bora huu, jambo moja mwaka mzima!!, Wananchi wataihofia serikali yao!”

-Mwananchi

No comments: