Mengi ana nia mbaya - Waziri Simba
• Mengi amjibu, asema hajui anenalo
na Tamali Vullu
WAZIRI wa Nchi Ofisi ya Rais (Utawala Bora), Sophia Simba, ameeleza kusikitishwa kwake na hatua ya Mwenyekiti Mtendaji wa Makampuni ya IPP, Reginald Mengi, ya kuwashambulia wafanyabiashara wenzake kwa kuwaita mafisadi papa.
Mbali ya hayo, Waziri Simba ambaye pia ni Mwenyekiti wa Taifa wa Jumuiya ya Wanawake Tanzania (UWT) alisema kitendo alichokifanya Mengi kinaonyesha namna alivyo na nia mbaya na wafanyabiashara wenzake.
Waziri huyo alisema, kitendo alichofanya Mengi ambaye alisisitiza kuwa hakuwa na mamlaka hayo, kinaonyesha namna anavyoingilia kazi zinazopaswa kufanywa na taasisi nyingine za dola.
“Alichofanya Mengi ni kosa, na kwa lugha ya vijana wa mjini, wanasema amechemsha. Kuna vyombo vingi vya serikali ambavyo angeweza kupeleka suala hilo, lakini kwa jinsi alivyofanya si mahala pake... Ana nia mbaya na wenzie,” alisema Simba ambaye kimsingi yeye ndiye waziri mwenye dhamana ya kusimamia utendaji wa kazi wa Taasisi ya Kuzua na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU) inayohusika na kesi zote zinazohusu ufisadi.
Simba alikuwa akijibu tuhuma zilizotolewa na Mengi mwishoni mwa wiki iliyopita, ambaye aliitisha mkutano wa waandishi wa habari na kuwataja wafanyabiashara watano, wanne wakiwa na asili ya Kiasia na mmoja Kiirani kuwa watuhumiwa wakubwa wa ufisadi aliowaita ‘mafisadi papa’.
Katika mkutano wake huo na waandishi wa habari, Mengi anayemiliki mtandao mkubwa wa vyombo vya habari yakiwamo magazeti, televisheni na redio, alikwenda mbele zaidi na kuwatuhumu wafanyabiashara hao kuwa watu wanaokwamisha juhudi za Rais Jakaya Kikwete za kupambana na rushwa.
Mbali ya hilo, Mengi alisema iwapo vyombo vya dola vitafanikiwa kuwadhibiti watuhumiwa hao wakubwa wa ufisadi, basi nchi itapona na kuondokana na matatizo mengi yanayoikabili sasa.
Mengi alikwenda mbele zaidi na kusema kwamba, watuhumiwa hao wa ufisadi, wamefikia hatua ya kuanza kuwatisha watu wachache waliojitoa mhanga kukabiliana na vitendo vya ufisadi nchini.
Katika orodha hiyo ya watuhumiwa, Mengi aliwataja Mbunge wa Igunga, Rostam Aziz (CCM), Yussuf Manji, Shubash Patel, Jeetu Patel na Tanil Somaiya.
Kama ilivyo kwa Mengi mwenyewe, mbali ya kuwa wafanyabiashara, baadhi ya watuhumiwa hao kama Rostam na Tanil wanahusishwa na umiliki wa baadhi ya vyombo vya habari nchini.
Waziri Simba ambaye jana hakueleza iwapo msimamo huo dhidi ya Mengi ulikuwa wake binafsi au wa serikali, alisema mfanyabiashara huyo hakuwa na mamlaka ya kisheria ya kufanya kile alichokifanya, cha kuwanyoshea vidole vya ufisadi wafanyabiashara wenzake.
Alitoa kauli hiyo wakati akizungumza na waandishi wa habari muda mfupi baada ya kufungua semina ya kujadili sheria ya maadili ya viongozi ya mwaka 1995, iliyoandaliwa na Kituo cha Demokrasia Tanzania (TCD) na kufanyika katika Hoteli ya Blue Pearl, jijini Dar es Salaam.
Pasipo kufafanua, Waziri Simba ambaye amekuwa kiongozi wa juu wa kwanza wa serikali kutoa kauli, tangu Mengi alipowashutumu wafanyabiashara watano kwa tuhuma za ufisadi, alisema kauli hiyo ya mfanyabiashara huyo inaonyesha namna alivyo na nia mbaya na wafanyabiashara wenzake.
“Kwanza yeye ni nani mpaka awataje? Mfano Jeetu (Patel) suala lake bado lipo mahakamani, hivyo bado ni mtuhumiwa tu mpaka mahakama itakapotamka vinginevyo.
“Mengi hana haki ya kuwaita wenzake mafisadi papa, na asitumie magazeti yake vibaya,” alionya waziri huyo.
Alipotafutwa kwa njia ya simu na Tanzania Daima jana na kuelezwa shutuma zilizoelekezwa kwake na Waziri Simba, Mengi alisema kwa ufupi kwamba, anamwombea Waziri Simba kwa Mwenyezi Mungu na kwa masikini Watanzania, wamsamehe kwa sababu hajui anenalo.
“Mimi namwombea kwa Mwenyezi Mungu na kwa masikini Watanzania, wamwombee kwa sababu hajui anenalo,” alisema Mengi kwa ufupi, akijibu kauli ya Waziri Simba.
-Tanzania Daima.
SBP hatupo upande wowote katika hawa ila kuna wakati tunasomasoma mambo ya siasa!
No comments:
Post a Comment