Tafuta/Search This Blog

Tuesday, September 29, 2009

Hii nimeipenda!!

Serikali kuagiza matrekta 10,000 kutoka India

Hussein Kauli

SERIKALI imesema inatarajia kuagiza matrekta 10,000 kutoka India ikiwa ni hatua ya kuboresha sekta ya kilimo kupitia sera ya Taifa ya Kilimo Kwanza .
Hayo yalisemwa na Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu, (Sera na Bunge), Philip Marmo, alipokuwa akizungumza kupitia kituo cha televisheni cha Star Tv jana asubuhi.
Kauli hiyo ya Marmo ilikuwa ikijibu hoja ya mtaalamu aliyealikwa katika kipindi hicho, kueleza kuwa kuna haja kwa serikali kuifanya sera hiyo kuwa hai kwa kuitekeleza kivitendo.
"Kama kweli serikali imeamua kuboresha sekta ya kilimo inatakiwa itekeleze kivitendo kwani hatujawekeza kutekeleza haya, hivyo tunahitaji kufanya sera hii kuwa hai" alisema mtaalamu huyo.

Akijibu hoja hiyo Marmo alisema, “katika kutekeleza sera ya Kilimo Kwanza serikali ina mipango thabiti. Kuna mambo mengine si vizuri kuyazungumza sasa” alisema Marmo na kuongeza.
"Kuna matrekta elfu kumi tunatarajia kuyaagiza kutoka India ambayo tutayapeleka Kibaha kwa ajili ya wakulima, hii ni kuonyesha jinsi serikali inavyojipanga kutekeleza Kilimo Kwanza."
Hata hivyo,Marmo alipinga dhana iliyoelezwa na mwananchi mmoja kutoka Dar es Salaam, kuwa Kilimo Kwanza ni sera ya Uchaguzi wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), akisema hiyo ni sera ya Taifa.

"Sera ya Kilimo Kwanza siyo sera ya uchaguzi ya CCM, bali ni sera ya Taifa ambayo iliandaliwa kwa ushirikiano na vyama vya mbalimbali na wataalamu wa serikali", alisema Marmo.
Kuhusiana na hali ya upungufu wa chakula uliopo nchini, Marmo alisema, karibu nusu ya nchi inakabiliwa na tatizo hilo, lakini serikali imejipanga vyema kukabiliana nalo.
"Hali ya chakula si nzuri, lakini si mbaya kiasi cha kutangaza hali ya hatari.Kwa sasa tunahamisha chakula kwenda kwenye mikoa yenye upungufu na tumeruhusu wafanyabiashara kununua vyakula kutoka sehemu zenye chakula kwenda maeneo yenye upungufu, ili kukabiliana na tatizo hilo,"alisema Marmo.

Akizungumzia mvua za El nino zilizotabiriwa kutokea hivi karibuni, Marmo alisema utabiri huo ni sahihi na tayari wameshaunda kamati za maafa kuanzia ngazi ya kijiji hadi mkoa kukabiliana nayo.

Katika kipindi hicho ilielezwa kuwa, mvua hizo zimeshaanza kunyesha mkoani Mwanza na Marmo amesema serikali inashirikiana na JWTZ pamoja na Msalaba Mwekundu kutoa msaada kwa wale watakaoathirika na mvua hizo. "Kwa wale wanaoishi mabondeni Serikali haiwezi kuwatoa kwa nguvu bali inawaelimisha juu ya athari zake.
"Lakini kuna dosari katika kutekeleza sera ya maafa sehemu za vijijini" alisema Marmo na kuongeza: "Pamoja na uharibifu utakaoletwa na mvua za el-nino, ningependa tuzitumie vizuri kuimarisha mabwawa yetu ili tuwe na maji ya kutosha baadaye."

-Food for the thought

No comments: