Sekondari Dar wazichapa kavukavu, polisi yashikilia 20
KITUO cha daladala Tuangoma Wilaya ya Temeke jana kiligeuka uwanja wa mapigano baada ya wanafunzi wa Shule tatu za Sekondari tofauti kuamua kuonyeshana umwamba wa kupigana hadi kuumizana.
Wanafunzi hao ambao ni wa vidato tofauti katika shule za Sekondari Mikwambe, Tuangoma, Makongo na Changanyikeni zote za Wilaya ya Temeke walifanya tukio hilo muda mfupi baada ya kupanda katika daladala za kuelekea Tuangoma wakitokea Mikwabe.
Filamu hiyo iliyodumu kwa saa kadhaa ilisababisha wanafunzi 14, kujeruhiwa na kukimbizwa katika hospitali ya Wilaya ya Temeke kwa matibabu zaidi.
Akizungumzia tukio hilo, Kamanda wa Polisi Kanda Maalumu ya Dar es Salaam, (DCP) Suleiman Kova alisema, uchunguzi wa awali unaonyesha kuwa wanafunzi hao wana mgogoro wa muda mrefu unaotokana na masuala ya kimapenzi wakituhumiana kuchukuliana wasichana.
Kwa mujibu wa Kamanda Kova, ugomvi huo ulisababishwa na baadhi ya wanafunzi wa shule hizo tatu ambazo zipo karibu.
Alisema taarifa za awali zinaonyesha wanafunzi hao ni watukutu, watoro wa vipindi darasani na muda wote hushinda vichakani bila kuhudhuria vipindi.
Kova alisema ugomvi baina ya wanafunzi hao ulianza wakati wakiwa katika daladala wakitokea Mikwambe kuelekea Tunagoma na kwamba walianza kurushiana maneno na baada ya muda mfupi walianza kupigana.
Kova alisema wakati vurugu hizo zikiendelea mwalimu Mkuu wa Shule ya Tuangoma alitoa taarifa polisi na muda mfupi baadaye askari walifika katika eneo hilo na kufanikiwa kuwakamata wanafunzi 20 wanaosadikiwa kuwa chanzo cha vurugu hizo. Majina ya wanafunzi hao, yamehifadhiwa.
Alisema jeshi la polisi Kanda Maalumu ya Dar es Salaam kwa kushirikana na Ofisa Elimu wa Wilaya ya Temeke pamoja na viongozi wa shule hizo, wanaendelea na uchunguzi kuhusiana na mgogoro huo.
-Mwananchi.
Kwa mtazamo wangu hii ni aibu kwamba watoto wetu wanakwenda shule na kuanza kupigana kwa ajili ya mapenzi. Hii ni moja ya sababu ya under performance ambayo inaonekana kwenye shule zetu. Aibu sana!! wa kulaumiwa ni wanafunzi wenyewe na labda na wazazi wao kwa kushindwa kuwajengea misingi mizuri!!
No comments:
Post a Comment