Tafuta/Search This Blog

Wednesday, August 12, 2009

INATISHA...

Na Exuper Kachenje, aliyekuwa Nairobi

INAKADIRIWA kuwa vitendo vya kujamiiana 114 milioni vinafanyika duniani kila siku na kusababisha mimba 910,000 huku 520,000 kati ya hizo zikitolewa, nyingi kwa njia isiyo salama.
Aidha, vifo 70,000 vya wanawake vinatokea kila mwaka kutokana na utoaji mimba usio salama ambapo kwa takwimu za mwaka 2005, Tanzania inakadiriwa kuwa vifo 950 vya wajawazito huku 285 sawa na asilimia 30 ya vifo hivyo vikitokana na utoaji mimba usio salama.
Profesa Joseph Karanja wa Hospitali Kuu ya Nairobi Kenya alibainisha hayo alipokuwa akitoa mada katika semina ya uhamasishaji vyombo vya habari Afrika Mashariki kuhusu haki ya afya ya uzazi kwa wanawake na utoaji mimba usio salama iliyofanyika mjini Nairobi wiki iliyopita.
Akizungumza na Mwananchi baada ya semina hiyo Profesa Karanja alisema idadi hiyo ni matokeo ya tafiti mbalimbali na kuongeza kuwa katika ya vitendo hivyo vya kujamiiana watu 365,000 wanaambukizwa magonjwa mbalimbali ya zinaa pamoja na Ukimwi.
Profesa Karanja ambaye pia ni mtaalamu wa magonjwa ya wanawake na mshauri alifafanua kuwa, “Tafiti mbalimbali zinaonyesha kuwa kati ya mimba 910,000 zinazotungwa kwa siku ni watoto 390,000 pekee wanaozaliwa wakiwa hai.”
Profesa Karanja alisema,” Katika kila dakika, nchini Kenya wanawake 380 wanapata ujauzito, 190 zisizotarajiwa, 110 wanapata ujauzito wenye matatizo na wanawake 40 wanatoa mamba kwa njia zisizo salama na mmoja hufa kwa matatizo ya ujauzito.”
Naye Dk Eduardo Namburete ambaye ni Mkufunzi wa Chuo Kikuu cha Eduardo Mondlane cha Maputo Msumbiji alisema upo umuhimu kwa nchi za Afrika kuangalia upya katiba na sheria zake kuhusu haki za wanawake ikiwemo kuwezesha utoaji mimba salama.
Alisema utoaji mimba usio salama unafanyika kwa kiwango kikubwa katika bara hilo kutokana serikali za nchi hizo kuweka masharti katika utoaji mimba hivyo wahusika wanatekeleza azma zao kwa kificho na kuhatarisha maisha yao.
“Serikali zinajiangalia zenyewe hazifikirii watu, bali taasisi zinazoiunga mkono, lazima sasa serikali za Afrika zifunue zaidi uelewa kwa watu wake juu ya sheria na haki zao kwa maslahi na afya zao,”

-Mwananchi

No comments: